Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Hawza, semina hiyo iliwakutanisha washiriki kutoka makundi mbalimbali ya jamii, wakiwemo wanafunzi wa madrasa, vyuo na shule za sekondari, walimu wa madrasa, masheikh, pamoja na kina mama na kina baba kutoka Wilaya za Mjini, Magharibi “A”, Magharibi “B”, Kaskazini “A”, Kaskazini “B” na Kati. Ushiriki huo uliifanya semina hiyo kuwa jukwaa muhimu la kuzungumzia nafasi ya elimu, malezi na maadili katika kuijenga jamii yenye mustakabali bora.
Miongoni mwa wageni waliohudhuria alikuwa Dkt. Shaaban Al-Battashi, aliyemwakilisha Mufti Mkuu wa Zanzibar. Dkt. Al-Battashi, ambaye ni Mkuu wa Division ya Utatuzi wa Migogoro katika Ofisi ya Mufti, Mjumbe wa Baraza la Maulamaa, Ulamaa wa Mahakama Kuu, Mtafiti wa Kuzuia Udhalilishaji (DPP), pamoja na Mshauri wa Kidiplomasia na Kijamii, aliewasilisha salamu za Mufti Mkuu wa Zanzibar na kutoa nasaha zilizosisitiza umuhimu wa kujenga na kudumisha maadili mema katika jamii.
Aidha, semina hiyo ilihudhuriwa na SP A’Rahman Omar na SP Salum Amir kutoka Makao Makuu ya Jeshi la Polisi Mkoa wa Mjini Magharibi, waliomwakilisha Kamanda wa Polisi wa Mkoa. Viongozi hao waliwasilisha salamu kutoka Jeshi la Polisi na kutoa mada iliyolenga kueleza baadhi ya vyanzo vya kuporomoka maadili miongoni mwa vijana, sambamba na kueleza mbinu za kukabiliana na changamoto hizo kwa ushirikiano kati ya familia, taasisi za elimu, viongozi wa dini na jamii kwa ujumla.
Mada kuu ya semina hiyo, iliyobeba kaulimbiu “Vijana, Uongozi na Maadili,” iliwasilishwa na Sheikh Othman Maulid Juma, ambaye alieleza kwa kina nafasi na wajibu wa vijana katika uongozi, huku akisisitiza umuhimu wa vijana kushikamana na misingi na maadili ya Kiislamu katika safari yao ya kuijenga jamii na taifa.
Semina hiyo haikubaki ndani ya ukumbi pekee, kwani ilirushwa mubashara kupitia Shirika la Utangazaji Zanzibar (ZBC), hatua iliyowezesha ujumbe wa Maulidi, maadili na malezi kuwafikia watu wengi zaidi ndani na nje ya ukumbi huo.
Kupitia semina hiyo, Bilal Muslim Mission Tanzania imeendelea kusisitiza umuhimu wa kuwekeza katika malezi ya vijana na kuimarisha maadili katika jamii, huku ikitoa nafasi kwa viongozi wa dini, taasisi za serikali, walimu, wazazi na vijana kushirikiana katika kukabiliana na changamoto za kimaadili na kujenga kizazi chenye elimu, uwajibikaji na misingi imara ya Kiislamu.


Maoni yako