Ijumaa 30 Oktoba 2026 - 01:30
Wananchi nchini Bahrain Waitisha Maandamano Makubwa

Hawza/ Kufuatia wito mkubwa wa kufanya maandamano tarehe 8 Novemba (17 Aban), vikosi vya usalama vya Bahrain vimeingia katika hali ya tahadhari ya juu katika maeneo nyeti, yakiwemo barabara ya Al-Budaiya. Mvutano huu unatokea wakati huo huo ambapo Mahakama Kuu ya Jinai imepanga tarehe ya kutolewa hukumu katika kesi ya kuwahukumu wanazuoni wa dini. Hali hii imeifanya anga ya kisiasa nchini humo kukabiliwa na uwezekano wa kutokea machafuko makubwa na hali kuwa ngumu zaidi.

Kwa mujibu wa ripoti ya Idara ya tarjuma ya Shirika la Habari la Hawza, vikosi vya usalama vya utawala wa Aal Khalifa vimeingia katika hali ya tahadhari ili kukabiliana na wito  unao ongezeka wa kufanya maandamano tarehe 8 Novemba, ulioanzishwa na Muungano wa Vijana wa Mapinduzi ya Februari 14. Hata hivyo, wito huo ulianza awali kusambazwa na mitandao ya habari ya kikanda.

Mamlaka za usalama, kwa lengo la kukabiliana na vuguvugu hili, zimeviomba vyombo vya habari na kurasa za habari kuchapisha ujumbe wa tahadhari na kuelezea wito huo kuwa ni “ya uchochezi, unaotetea vurugu na unaokiuka sheria.” Wakati huohuo, vikosi vya utawala vimeongeza uwepo wao katika maeneo mapya ya kiusalama, hasa kwenye milango ya maeneo yanayoelekea barabara ya “9 Machi” (Al-Budaiya), ili kuzuia uwezekano wa kutokea makabiliano.

Wito huo unalenga kuitangaza tarehe 8 Novemba kuwa “Siku ya Hasira ya Wananchi.” Tarehe hiyo inasadifiana na siku ambayo Mahakama ya Jinai imeipanga kwa ajili ya kutangaza hukumu katika kesi ya kuwahukumu wanazuoni wa dini. Kulingana na hasira za wananchi dhidi ya kesi hizo, kuingiliana kwa matukio haya kunatoa ishara ya uwezekano wa kuongezeka mvutano na kuwa tata zaidi kwa hali ilivyo.

Katika taarifa iliyochapishwa tarehe 26 Oktoba, Muungano wa Vijana wa Mapinduzi ya Februari 14 ulitangaza kuunga mkono kamilifu vuguvugu hili la wananchi na kueleza kuwa utashiriki kikamilifu katika mipango ijayo.

Katika taarifa hiyo, muungano huo uliahidi kuugeuza uhalifu wa kuwakamata na kuwafungulia mashtaka wanazuoni wa dini—ambao wanashikiliwa kana kwamba ni mateka—kuwa kitanzi cha kuning’inizia utawala huo shingoni; kitanzi ambacho kitameza mabaki ya kiburi na ukatili wake. Aidha, muungano huo ulisisitiza kuwa una imani kamili na uwezo wa wananchi wa Bahrain wa kugeuza mizani ya dhuluma na kuibadilisha, pamoja na changamoto na matatizo, kuwa fursa zenye mafanikio makubwa.

Katika muktadha huohuo, makundi ya kimapinduzi, yakiwemo Al-Wifaq, Al-Wafaa, Ahrar Bahrain, Haq, Al-Itilaf na Amal, yalitoa taarifa ya pamoja yakisema kuwa: “Kesi za maigizo zisizo na uhalali zinazofunguliwa dhidi ya wanazuoni wa dini zinaliweka kila tabaka la wananchi mbele ya wajibu wake wa kihistoria wa kulinda mafanikio ya kidini na kitaifa.”

Makundi hayo, huku yakilaani vikali msimamo wa serikali wa kung’ang’ania kuwakamata na kuwafungulia mashtaka wanazuoni wa dini kwa kutumia visingizio vinavyolenga kuzuia uhuru wa kidini, yalibainisha kuwa muda uliochaguliwa kwa ajili ya hatua hizo una misukumo ya kimadhehebu na umeathiriwa na maagizo kutoka nje ya nchi.

Vyanzo vya kimapinduzi vinaamini kuwa utawala huo, kwa kuzingatia uwezekano wa kurejea mvutano katika ngazi ya kikanda — hasa kutokana na uchaguzi wa katikati ya muhula wa Bunge la Congress la Marekani tarehe 3 Novemba — unajaribu kutumia mazingira hayo ya kimataifa kupunguza ukali wa hatua zake dhidi ya wanazuoni wa dini. Aidha, unajaribu kuzuia miitikio inayoweza kutokea ndani na nje ya nchi kwa kuweka udhibiti wa vyombo vya habari.

Lebo

Maoni yako

You are replying to: .
captcha