Ijumaa 30 Oktoba 2026 - 02:00
Hukumu ya Kifo dhidi ya Sheikh Al-Matouq ni Sehemu ya Vurugu Kubwa Zinazowalenga Mashia katika Nchi za Ghuba ya Uajemi

Hawza/ “Muungano wa Vijana wa Mapinduzi ya Februari 14” umelaani vikali, kupitia taarifa yenye maneno makali, hukumu ya kifo iliyotolewa na Mahakama ya Jinai ya Kuwait dhidi ya Sheikh Hussein Abdullah Al-Matouq na wenzake.

Kwa mujibu wa ripoti ya Idara ya tarjuma ya Shirika la Habari la Hawza, “Muungano wa Vijana wa Mapinduzi ya Februari 14” umelaani vikali, kupitia taarifa yenye maneno makali, hukumu ya kifo iliyotolewa na Mahakama ya Jinai ya Kuwait dhidi ya “Sheikh Hussein Abdullah Al-Matouq” na wenzake. Muungano huo umeielezea mahakama ya Kuwait kuwa ni chombo cha kisiasa kinachofuata maagizo ya vyombo vya usalama. Pia umeitaja hukumu hiyo kuwa ni ukiukaji wa wazi wa haki na sehemu ya vurugu zilizopangwa dhidi ya Mashia katika eneo lote la Ghuba ya Uajemi.

Maandishi ya taarifa hiyo ni kama ifuatavyo:

Kwa jina la Mwenyezi Mungu, Mwingi wa Rehema, Mwenye Kurehemu.

Tunalaani na kupinga vikali hukumu ya dhuluma iliyotolewa na Mahakama ya Jinai ya Kuwait (Kitengo cha Usalama wa Taifa), ambayo imehukumu kunyongwa kwa “Sheikh Hussein Abdullah Al-Matouq” pamoja na ndugu zake waumini walioandamana naye.

Kwa hakika, hukumu hii haikutolewa na mahakama huru na isiyopendelea upande wowote, bali imetokana na mfumo wa mahakama wa kisiasa unaofuata kikamilifu maagizo ya vyombo vya usalama na wanasiasa. Hukumu hii inatumiwa kama chombo cha kueneza hofu na vitisho, pamoja na kulipiza kisasi kwa misingi ya kimadhehebu. Hali hii inakinzana kabisa na misingi ya haki na uadilifu, na inahesabika kuwa ni ukiukaji wa wazi kabisa wa viwango vya haki, haki za uraia na utu wa binadamu.

Tunatangaza mshikamano wetu kamili na Sheikh Hussein Al-Matouq, wenzake waliodhulumiwa na kuhukumiwa isivyo haki, pamoja na Mashia wote wa Kuwait ambao wamelengwa na sera za dhuluma zinazowalenga kwa makusudi. Sera hizo zinalenga uwepo wao, nafasi yao katika jamii, pamoja na taasisi zao za kidini na kijamii, huku zikikusudia kuwanyamazisha na kukandamiza uhuru wao.

Tunaamini kwamba ukandamizaji unaoendelea kutekelezwa na vyombo vya usalama na mahakama nchini Kuwait ni sehemu ya kampeni kubwa zaidi iliyoratibiwa dhidi ya Mashia katika eneo lote la Ghuba ya Uajemi, kuanzia Kuwait na Bahrain hadi Hijaz na Umoja wa Falme za Kiarabu. Vurugu hizi zinaambatana na sifa kama vile kuwalenga Mashia kwa utaratibu maalumu, kuwanyang’anya haki zao na kutumia mashtaka ya kiusalama yaliyotungwa mapema ili kuimarisha sera za ubaguzi na ukandamizaji dhidi yao.

Sisi, katika “Muungano wa Vijana wa Mapinduzi ya Februari 14,” tunatoa wito wa kufutwa mara moja hukumu hizi, kusimamishwa hatua zote zinazohusiana nazo, kurejeshwa haki kwa wenye haki hizo na kufidiwa dhuluma walizofanyiwa. Aidha, tunataka mikono hii miovu izuiwe isiendelee kuwadhuru.

Muungano wa Vijana wa Mapinduzi ya Februari 14

Jumatano, tarehe 28 Oktoba 2026 .

Lebo

Maoni yako

You are replying to: .
captcha