Kwa mujibu wa Kitengo cha Kimataifa cha Shirika la Habari la Hawza, Osama Hamdan, mmoja wa viongozi wa Harakati ya Hamas, katika mahojiano na mtandao wa Al Mayadeen, amesema kuwa; kuchaguliwa Khalil al-Hayya kuwa Mkuu mpya wa Ofisi ya Kisiasa ya Hamas ni dalili ya uhai wa harakati hiyo na kwamba mradi wa Muqawama bado unaendelea kuwa hai.
Alisema kuwa; uchaguzi huo unaonesha azma ya Hamas ya kutekeleza wajibu wake kwa wananchi wa Palestina pamoja na washirika wake.
Hamdan aliongeza kuwa; kuchaguliwa kwa Khalil al-Hayya kwa makubaliano ya pamoja ndani ya harakati hiyo kunatuma ujumbe kwamba, bila kujali ni nani anayeshika nafasi ya juu ya uongozi wa Hamas, harakati hiyo itaendelea kushikamana na njia ya Muqawama.
Akikumbushia kuwa Khalil al-Hayya ana uzoefu mkubwa katika ngazi mbalimbali za Hamas na amekuwa mmoja wa wahusika wakuu katika mchakato wa mazungumzo, alisema kuwa; uzoefu huo unaweza kutumika katika juhudi za kumaliza vita vya mauaji ya kimbari vinavyoendelea dhidi ya Ukanda wa Ghaza.
Kiongozi huyo wa Hamas alisisitiza kuwa Muqawama si njia fupi zaidi ya kurejesha haki za wananchi wa Palestina, bali ndiyo njia pekee ya kufanikisha lengo hilo. Aidha, alibainisha kuwa Khalil al-Hayya kwa zaidi ya miaka 20 amesimama imara mbele ya vitisho na juhudi za adui za kutaka kumuua na kumlenga.
Hamdan pia alisema kuwa; baada ya kuuawa kishahidi baadhi ya viongozi wa Hamas, harakati hiyo imechukua hatua muhimu za kuupanga upya muundo wake wa ndani, kuandaa upya hali ya uwanja wa mapambano, na kuendelea na njia ya Muqawama.
Alisema; mshikamano wa ndani wa Hamas ni miongoni mwa nguzo muhimu zaidi za nguvu ya viongozi wa harakati hiyo, na akaongeza kuwa katika mazingira ambayo vita vya mauaji ya kimbari dhidi ya wananchi wa Palestina vinaendelea, nafasi ya uongozi imekuwa muhimu zaidi kuliko wakati mwingine wowote na yenye athari kubwa katika kufanya maamuzi.
Katika sehemu nyingine ya mazungumzo yake, Hamdan akizungumzia mahusiano ya ndani ya Wapalestina, alisema kuwa; Hamas imefanikiwa kujenga msimamo wa kitaifa, unaowajumuisha wote na unaounga mkono Muqawama, lakini Mamlaka ya Ndani ya Palestina imebaki nyuma katika mchakato huo.
Hata hivyo, alisisitiza kuwa; Hamas bado imeendelea kuzinyooshea mkono pande zote kwa ajili ya kushinda migawanyiko ya ndani na kuunganisha msimamo wa Wapalestina mbele ya makubaliano ya utawala wa Kizayuni wenye lengo la kulifuta suala la Palestina.
Kiongozi huyo wa Hamas pia alisema kuwa; Marekani na utawala wa Kizayuni wanalenga kuifanya Israel kuwa mhimili mkuu wa eneo la Mashariki ya Kati, lakini Hamas itaendelea kutafuta na kuimarisha uungwaji mkono kwa harakati ya Palestina.
Mwishoni mwa mazungumzo yake, Hamdan aliwashukuru wale wanaounga mkono Muqawama wa Palestina na kusisitiza kuwa; Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, Yemen na Muqawama wa Lebanon ni miongoni mwa wahusika muhimu zaidi ambao hawakuishia kuonesha uungwaji mkono wa kisiasa pekee, bali walisimama pamoja na Muqawama hadi kufikia kiwango cha kuingia moja kwa moja katika uwanja wa makabiliano.
Maoni yako