Kwa mujibu wa mwandishi wa Shirika la Habari la Hawza, kutoka Bushehr, Ayatullah Sayyid Hashim Husseini Bushahri, Mwenyekiti wa Jumuiya ya Walimu wa Hawza ya Qom, jana adhuhuri katika mazungumzo yake na waandishi wa habari amesema kuwa; njia ya Muqawama itaendelea kwa nguvu zote, na kuuawa kishahidi makamanda hakutaisimamisha harakati hii.
Alisema: "Kulipiza kisasi damu ya Kiongozi Shahidi wa Umma, makamanda na wana wa Mhimili wa Muqawama hakutabaki bila jibu. Ahadi ya kulipiza kisasi dhidi ya wahusika wa vitendo hivi ni ahadi ya hakika, na kama ambavyo Kiongozi Mkuu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesisitiza mara nyingi, adui pamoja na wanaomuunga mkono hawana budi kulipa gharama kubwa kwa jinai hii."
Mwenyekiti wa Jumuiya ya Walimu wa Hawza ya Qom pia akizungumzia hafla kubwa za mazishi ya Kiongozi Shahidi alisema: "Sherehe hizi kubwa ni ishara ya nafasi ya juu ya Kiongozi Shahidi wa Umma miongoni mwa mataifa yanayopenda uhuru duniani. Ushiriki wa mamilioni ya watu nchini Iran, Iraq na katika nchi nyingine kwenye hafla za kumbukizi unaonesha uhusiano wa kina wa mataifa haya na malengo ya Muqawama pamoja na uaminifu wao katika njia hii."
Makamu Mwenyekiti wa Baraza la Wataalamu wa Uongozi aliongeza kuwa: "Ushiriki huu wa kipekee umevuruga hesabu zote za maadui, mabeberu walidhani kwamba kwa kuwaondoa viongozi wenye ushawishi wa Muqawama, mhimili huu ungekuwa dhaifu, lakini mwitikio mkubwa wa wananchi katika hafla za kuwaenzi mashahidi umeonesha kuwa utamaduni wa kujitolea mhanga na Muqawama bado uko hai na una athari kubwa."
Ayatullah Husseini Bushehri katika sehemu nyingine ya hotuba yake alizungumzia propaganda zinazohusishwa na mikoa ya kusini mwa nchi na kusema: "Watu ambao hapo awali hawakuwa na wasiwasi wowote kuhusu masuala ya wananchi na usalama wa taifa, sasa kupitia madai mbalimbali wanajaribu kueneza fikra kwamba viongozi hawajali wala hawazingatii hali ya mikoa ya kusini mwa nchi."
Imamu wa Swala ya Ijumaa wa Qom alisisitiza: "Baadhi ya hatua na propaganda hizi hazitokani na kuwahurumia wananchi, bali zinalenga kuzusha mifarakano, kuigawa jamii katika makundi mawili na kupunguza mtaji wa kijamii wa mfumo. Huu ni mwendelezo wa vita vya vyombo vya habari na operesheni za kisaikolojia za adui dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran."
Makamu Mwenyekiti wa Baraza la Wataalamu wa Uongozi, akirejelea utendaji wa vikosi vya ulinzi katika vita vya siku arobaini, alisema: "Nguvu, mipango sahihi na majibu madhubuti ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran vimezifanya njama za adui kushindwa, na kwa busara ya viongozi pamoja na umakini wa makamanda, mipango mipya ya adui pia haitafanikiwa."
Mwenyekiti wa Jumuiya ya Walimu wa Hawza ya Elimu ya Dini ya Qom aliwataja watu wa kusini mwa Iran kuwa ni watu waaminifu, wa kimapinduzi na wenye kushikamana na Wilayah. Alikumbusha kwamba; kusini mwa Iran daima kumewalea watu mashuhuri kama Rais Ali Delvari, Kamanda Alireza Tangsiri na Shahidi Nader Mahdavi. Aidha, sambamba na watu hawa wanaojulikana, kuna idadi kubwa ya wanajeshi na walinzi wa sekta nyingine za ulinzi ambao kwa moyo wa kujitolea mhanga na kujitoa wanalinda usalama na mipaka ya Iran.
Ayatullah Husseini Bushehri alisisitiza: "Ingawa adui, kwa kuelekeza nguvu zake katika Mlango wa Bahari wa Hormuz, ameelekea kwenye maeneo ya kusini mwa nchi, mashambulizi haya hayakuishia kusini pekee, bali yamegusa pia maeneo mengine ya nchi.
Hata hivyo, historia inaonesha kwamba watu wa kusini mwa Iran daima wamekuwa bega kwa bega na vikosi vya ulinzi na walinzi wa usalama wa taifa katika nyakati nyeti, kuanzia kipindi cha Vita vya Kujihami Vitakatifu hadi leo, na katika vipindi mbalimbali wameacha mchango mkubwa na wa kudumu kupitia kujitolea, mshikamano na Muqawama."
Mwenyekiti wa Jumuiya ya Walimu wa Hawza ya Qom pia akirejelea tajiriba za zamani alisema: "Madola ya kibeberu mara nyingi yameonesha kwamba hayashikamani na makubaliano wala ahadi zao, na historia yao imejaa visa vya kuvunja ahadi na kukiuka makubaliano."
Makamu Mwenyekiti wa Baraza la Wataalamu wa Uongozi alisema: "Jamhuri ya Kiislamu ya Iran siku zote imeonesha nia njema katika mahusiano ya kimataifa, lakini kila mara ambapo upande wa pili umeona maslahi yake yako hatarini, umekataa kutekeleza ahadi zake, mwenendo huu umeifanya fikra ya umma duniani kutambua zaidi uhalisia wa nchi hizo."
Ayatullah Husseini Bushehri, akisisitiza umuhimu wa mshikamano, kujiepusha na mifarakano na kusonga mbele kwa kuzingatia maelekezo ya Kiongozi Mkuu wa Mapinduzi ya Kiislamu, alisema: "Kulinda mshikamano na umoja wa kitaifa ndilo hitaji muhimu zaidi la nchi kwa sasa. Taifa la Iran, kwa umakini wake, halitaruhusu adui kutumia madai ya wananchi kama njia ya kuibua mpasuko wa ndani au kudhoofisha nguvu na mamlaka ya taifa."
Maoni yako