Ijumaa 17 Julai 2026 - 14:00
Mashia Hawatakuwa Chombo cha Fitna; Lebanon Haina Njia ya Wokovu Isipokuwa Umoja wa Kitaifa

Hawza/ Hujjatul Islam Sayyid Ali Fadlullah, Imamu wa Ijumaa wa Beirut, amesema kuwa, Mashia hawatakuwa chombo cha kuchochea fitna, akisisitiza kwamba Lebanon haina njia nyingine ya kuokoka isipokuwa kudumisha umoja wa kitaifa.

Kwa mujibu wa Kitengo cha tarjuma cha Shirika la Habari la Hawza, Hujjatul Islam Sayyid Ali Fadlullah, mwanazuoni mashuhuri na Imamu wa Ijumaa wa Beirut, alitoa mhadhara katika kikao cha mazungumzo kilichofanyika katika Kituo cha Utamaduni wa Kiislamu kilichopo eneo la Haret Hreik, chini ya anuani "Misimamo Yenye Ujumbe wa Kimsingi Katika Maisha ya Imam Zayn al-Abidin (as)", ambapo alizungumzia pia maendeleo ya hivi karibuni nchini Lebanon na katika eneo la Mashariki ya Kati.

Akisisitiza kuwa Mashia hawatakuwa kamwe mafuta ya kuwasha fitna, wala hawataifuata wala kuiunga mkono, alisema: "Lebanon haina njia ya wokovu isipokuwa kupitia umoja wa kitaifa."

Mwanzoni mwa kikao hicho, Hujjatul Islam Fadlullah alieleza baadhi ya vipengele vya shakhsia ya Imam Zayn al-Abidin (as), huku akibainisha kuwa msamaha, ustahimilivu na kujibu uovu kwa wema ni miongoni mwa sifa kuu za mwenendo wake. Aliongeza kuwa leo Umma wa Kiislamu unahitaji zaidi kuliko wakati mwingine wowote kuiga na kuhuisha maadili hayo katika maisha halisi.

Imamu wa Ijumaa wa Beirut alisema kuwa; misimamo ya Imam inaonesha mbinu ya Ahlul-Bayt (as) katika kuwashughulikia wapinzani wao; kwa sababu wao hawakutenda kwa misingi ya udhaifu wala hisia za ghafla, bali waliongozwa na roho ya utume iliyolenga kuwageuza maadui kuwa marafiki, au angalau kupunguza kiwango cha uadui. Hili, alisema, linaafikiana na amri ya Mwenyezi Mungu ya kuliondoa ovu kwa kufanya mema.

Hujjatul Islam Fadlullah aliongeza kuwa; kushikamana na mtazamo huu katika kujilea nafsi, kujenga jamii na kuwafanyia wema wale wanaofanya maovu au wenye dhana mbaya, ni dhamana ya kuondoa misuguano kutoka ndani ya nyoyo, na huenda hata kumgeuza adui kuwa rafiki.

Alifafanua kuwa wale wanaodhani kuwa njia hii ni ishara ya udhaifu au kwamba inawahamasisha waovu kuendelea na maovu yao ni hali za kipekee, si kanuni ya jumla.

Hujjatul Islam Fadlullah alisisitiza kuwa; Uislamu unahimiza mazungumzo kwa njia iliyo bora zaidi, pamoja na kutumia maneno mazuri na lugha ya utulivu katika kutatua tofauti za ndani, mbali na matusi, kejeli na dharau, kwa sababu mbinu hizo huongeza tu migawanyiko na kuchochea chuki.

Aidha alisisitiza kuwa, mazungumzo ndiyo njia bora zaidi ya kutatua migogoro na kujenga madaraja ya kuaminiana kati ya wananchi wa taifa moja. Hivyo akatoa wito wa kuachana na fitna kwa aina zake zote na kufanya kazi ya kuondoa sababu zake ili kulinda amani ya ndani na kuimarisha umoja wa kitaifa.

Imamu wa Ijumaa wa Beirut pia aliwataka viongozi wa Lebanon kufanya juhudi za dhati za kuimarisha umoja wa wananchi na kuimarisha makubaliano ya kitaifa, bila ubaguzi, kutengwa au kuwekwa pembeni kwa sehemu yoyote ya jamii ya Lebanon. Vilevile alionya dhidi ya kukubali mashinikizo na maagizo kutoka nje, ambayo hayatafuti isipokuwa maslahi yao binafsi.

Mwishoni mwa hotuba yake, Hujjatul Islam Fadlullah alisisitiza kuwa: "Lebanon haina njia ya wokovu isipokuwa kupitia umoja wa watoto wake wote, kufanya mazungumzo kuwa njia ya kutatua migogoro, kuunganisha juhudi za kurejesha ardhi zinazokaliwa kwa mabavu na utawala wa Israel, na kutanguliza maslahi ya taifa mbele ya maslahi ya makundi na mitazamo finyu."

Pia alionya kwamba; iwapo hatari zitaendelea kuongezeka, hakuna mtu atakayesalimika nazo, na athari za kusambaratika kwa taifa zitawakumba wananchi wote wa Lebanon bila ya ubaguzi.

Lebo

Maoni yako

You are replying to: .
captcha