Ijumaa 17 Julai 2026 - 21:00
Mchambuzi wa Kijeshi wa Yemen: Kushambuliwa kwa Uwanja wa Ndege wa Sana'a Kumemaliza Hatua ya Kupunguza Mvutano na Kurudisha Mzozo Katika Hatua ya Mwanzo

Hawza/ Mchambuzi wa masuala ya kijeshi wa Yemen, Meja Jenerali Khalid Ghurab, amesema kuwa kulengwa kwa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Sana'a ni maendeleo hatari katika mwenendo wa matukio, akieleza kuwa hatua hiyo imemaliza kipindi cha kupunguza mvutano na kuurudisha mzozo katika hatua yake ya mwanzo.

Kwa mujibu wa Kitengo cha tarjuma cha Shirika la Habari la Hawza, Meja Jenerali Khalid Ghurab, mchambuzi wa kijeshi wa Yemen, alisema Jumanne katika mahojiano na televisheni ya Al-Masirah kwamba; kushambuliwa kwa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Sana'a ni mabadiliko hatari katika mwenendo wa matukio. Alisema anaamini kuwa Saudi Arabia kwa vitendo imehitimisha kipindi cha kupunguza mvutano kilichoanza mwaka 2022 (1401 Hijria Shamsia), na kwamba jibu la Yemen, lililoanza kwa kulenga Uwanja wa Ndege wa Abha na kutangaza marufuku ya safari za ndege katika anga ya Saudi Arabia, linaashiria mwanzo wa hatua mpya ya operesheni za kuvunja mzingiro.

Alionya kwamba iwapo Riyadh itaendelea na sera yake ya kuongeza mvutano, hatua zitakazofuata zitakuwa pana zaidi na zenye athari kubwa zaidi.

Ghurab alisema taarifa ya kijeshi iliyotolewa na Jeshi la Yemen haikuwa tangazo la operesheni ya kijeshi pekee, bali ilikuwa na ujumbe wa kimkakati unaovuka mipaka ya medani ya vita. Miongoni mwa ujumbe huo ni kutangazwa kwa marufuku ya safari za ndege katika anga ya Saudi Arabia pamoja na onyo kwa mashirika ya kimataifa ya ndege kutotumia viwanja vya ndege vya Saudi, kwa kuwa viwanja hivyo vinachukuliwa kuwa maeneo ya operesheni za kijeshi hadi itakapotangazwa hatua nyengine.

Alieleza kuwa, kwa mtazamo wa kijeshi, hilo ndilo lilikuwa jambo muhimu zaidi katika taarifa hiyo, kwani linaonesha kuwa mzozo umeingia katika hatua mpya inayolenga kuweka mizani mipya ya kuzuia mashambulizi. Pia linatoa ujumbe wazi kuwa uamuzi wa kuvunja mzingiro umeanza kutekelezwa na kwamba Jeshi la Yemen litaendelea na hatua hizo hadi malengo yaliyokusudiwa yatakapofikiwa.

Ghurab aliongeza kuwa; kulengwa kwa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Sana'a kumeondoa kwa vitendo makubaliano yaliyokuwa msingi wa kipindi cha kupunguza mvutano na kuurudisha mzozo katika hatua ya mwanzo. Alifafanua kuwa makubaliano yaliyofikiwa baada ya operesheni za kuvunja mzingiro mwaka 2022 yalitokana na mashambulizi yaliyolenga miundombinu ya mafuta na vituo muhimu ndani ya Saudi Arabia, jambo lililoilazimu Riyadh kutafuta upatanishi ili kusitisha mvutano.

Alisisitiza kuwa; kipindi cha kupunguza mvutano katika miaka iliyopita hakikufanikisha utekelezaji wa ahadi zozote kuhusu kumaliza mzingiro wala kutekeleza vipengele vya ramani ya makubaliano. Aliishutumu Saudi Arabia kwa kutumia sera ya kuchelewesha na kuahirisha maamuzi, jambo lililodumisha hali ya "si vita wala si amani," hali ambayo imeongeza mateso ya wananchi wa Yemen na kuchelewesha suluhisho la kweli.

Aidha alisema kuwa; Jeshi la Yemen kwa sasa lina uwezo wa kijeshi ambao unatofautiana kwa kiwango kikubwa na ule wa mwaka 2022. Kwa mujibu wake, maendeleo hayo ni ya kiwango na ubora, yakijumuisha kuingizwa kwa mifumo ya kisasa ya makombora, makombora ya mwendo wa kasi wa juu (hypersonic), silaha zenye usahihi mkubwa, pamoja na kuongezeka kwa uzoefu wa kioperesheni wa vikosi vya Yemen katika miaka ya hivi karibuni.

Meja Jenerali Ghurab alikumbusha kuwa operesheni zilizowahi kulenga vituo vya Abqaiq na Khurais, mitambo ya kusafisha mafuta ya Riyadh na Jeddah, pamoja na bandari za Yanbu, Ras Tanura na Shaybah, zilifanywa kwa uwezo mdogo kuliko ule ambao Jeshi la Yemen linamiliki sasa. Alisema kuwa mzozo wowote mpya utatokea katika mazingira ya mizani tofauti kabisa ya nguvu za kijeshi.

Mchambuzi huyo wa kijeshi pia alisema kuwa uamuzi wa Saudi Arabia kuongeza mvutano haujajengwa juu ya tathmini sahihi ya kijeshi wala kisiasa.

Aliongeza kuwa; Riyadh inafahamu kiwango cha maendeleo ya uwezo wa Yemen katika miaka ya mapambano, pamoja na maendeleo yaliyoonekana kupitia operesheni za kuiunga mkono Ghaza katika mifumo ya makombora, ndege zisizo na rubani na uwezo wa kupanga na kutekeleza operesheni.

Akiendelea, alisema kuwa; hali ya jumla nchini Yemen, baada ya miaka ya kusuasua kwa mchakato wa kisiasa na kuendelea kwa vikwazo dhidi ya nchi hiyo, imefikia kiwango cha juu cha kuunga mkono chaguo la kuvunja mzingiro. Alisema pia kuwa wito wa uhamasishaji wa wananchi na hali ya tahadhari ya umma katika miezi ya hivi karibuni umeonesha kuwepo kwa mwafaka mpana kuhusu ulazima wa kurejesha haki halali za wananchi na kumaliza mzingiro.

Aliongeza kuwa; kuendelea kwa mzingiro, kufungwa kwa viwanja vya ndege, kuzuiwa kwa wagonjwa kusafiri kwa matibabu, pamoja na madhara ya kibinadamu na vifo vinavyotokana na hali hiyo, ni miongoni mwa sababu kuu zilizoongeza madai ya kuchukuliwa hatua kali zaidi baada ya njia zote za kisiasa na kidiplomasia kuonekana kushindwa.

Mwishoni, Meja Jenerali Khalid Ghurab alisisitiza tena kuwa; maendeleo ya hivi karibuni yanaonesha kwamba; mzozo umeingia katika hatua mpya ambayo, kwa asili na kiwango chake, ni tofauti na hatua zilizotangulia. Alisema kuwa kuendelea kwa hatua zozote za kuongeza mvutano kutoka upande wa Saudi Arabia kutajibiwa kwa hatua zinazolingana kutoka kwa Jeshi la Yemen, katika mfumo wa mapambano ya kuvunja mzingiro na kuweka mizania mpya ya kuzuia mashambulizi katika kipindi kijacho.

Lebo

Maoni yako

You are replying to: .
captcha