Ijumaa 17 Julai 2026 - 16:00
Mahakama ya Bahrain na Kuwakusudia Waislamu wa Madhehebu ya Shia

Hawza/ Haijalishi utawala wa Bahrain utajaribu kwa kiasi gani kuficha kufungwa kwa makumi ya wanazuoni na maulamaa wa Kishia kwa kuwabandika tuhuma za "uhaini" ili kuharibu heshima na hadhi yao, kuwakamata watu hao kutabaki kuwa moja ya uhalifu mkubwa zaidi wa kidini na kisiasa nchini humo.

Kwa mujibu wa Kitengo cha tarjama cha Shirika la Habari la Hawza, licha ya juhudi za utawala wa Bahrain kufunika kukamatwa kwa makumi ya wanazuoni wa Kishia kwa madai ya "uhaini", hatua hiyo inaendelea kutazamwa kama uhalifu mkubwa wa kidini na kisiasa ambao hauwezi kukanushwa.

Ingawa idadi ya wanazuoni mashuhuri walioko gerezani imezidi watu 40, serikali imeamua kuanza kwa siri kesi dhidi ya wanazuoni 19, bila kutangaza rasmi mwenendo wa mashauri hayo.

Wanazuoni wanaokabiliwa na kesi hizo ni:
Sayyid Majid al-Mash'al, Sheikh Ali al-Saddadi, Sheikh Muhammad Sanqur, Sheikh Fadhil al-Zaki, Sheikh Muhammad al-Kharsi, Sheikh Isa al-Mu'min, Sayyid Musa al-Wada'i, Sheikh Muhammad Jawad al-Shahabi, Sheikh Mirza al-Ma'tuq, Sheikh Hamid Ashour, Sheikh Ayyub al-Bahrani, pamoja na wanazuoni wengine wanane walioko nje ya nchi.

Kwa mujibu wa wataalamu wa haki za binadamu nchini Bahrain, faili hili lina ukiukaji mkubwa na wa wazi wa sheria, ukiwemo: Kesi zinaendeshwa kwa siri.

Washtakiwa hawajaruhusiwa kukutana na mawakili wao wala familia zao. Upande wa utetezi umezuiwa kuona jalada la kesi pamoja na nyaraka zake rasmi.

Mawakili wametishiwa kuchukuliwa hatua za kinidhamu iwapo wataomba kukutana na wateja wao au kupata nakala ya jalada la kesi. Tangu kukamatwa kwa washtakiwa, mawakili hawajawahi hata mara moja kuruhusiwa kukutana na watu wanaowatetea.

Washtakiwa hawajafikishwa binafsi mbele ya jaji, bali wamefikishwa kwa njia ya mawasiliano ya video. Mawasiliano ya washtakiwa na familia zao yako chini ya uangalizi mkali, na kila wanapojaribu kuzungumzia maelezo ya kesi zao, mawasiliano hukatwa mara moja.

Mamlaka zimewalazimisha washtakiwa kupokea mawakili waliowachagua wenyewe, na zimewaagiza mawakili hao kutokujiondoa katika kesi hata kama washtakiwa watawakataa.

Mbali na hayo, taarifa zilizokusanywa na wanaharakati wa haki za binadamu zinaonesha kuwa baadhi ya wanazuoni waliokamatwa wamefanikiwa kuwafahamisha familia zao kupitia simu fupi kwamba: "Tumelazimishwa kusaini tuhuma zinazotuhusisha."

Kwa mujibu wa wachambuzi, jambo hili lina tafsiri moja tu; kwamba kinachoendelea ni kesi ya kidini, kisiasa na hata ya kimadhehebu, bila kificho chochote. Tuhuma zinazowakabili waliokamatwa zinahusiana tu na itikadi za madhehebu ya Shia na utekelezaji wa ibada zao za kidini, na hazitegemei kitendo chochote kinachotambulika kisheria kuwa ni uhalifu.

Ripoti hiyo inaongeza kuwa suala hili haliwezi tena kuvumiliwa, kwa kuwa mwenendo rasmi wa serikali katika kesi hii umeonesha wazi kuwa kesi hiyo si ya haki, bali ni kesi ya maonesho inayolenga kuupa uhalali wa kisheria uamuzi wa kisiasa uliokwisha kufanywa kabla. Hitimisho lililo wazi ni kwamba kuwalenga wanazuoni wa Kishia – akiwemo Ayatullah Sheikh Issa Qassim – imekuwa sera rasmi ya serikali, huku mhimili wa mahakama ukitumika kuhalalisha hatua hiyo.

Leo hii, suala hili si kesi ya wanazuoni 11 au hata maulamaa zaidi ya 40 walioko gerezani pekee, bali ni mtihani wa utawala wa sheria nchini Bahrain. Pale ambapo dhamana za msingi za haki ya kusikilizwa kwa haki zinaponyang'anywa, upande wa utetezi unazuiwa kutekeleza wajibu wake, na mwenendo wa kesi unafichwa dhidi ya umma, basi kinachoendelea hakiwezi tena kuitwa mchakato wa kawaida wa mahakama, bali ni dalili ya mgogoro mkubwa wa kuaminiana kuhusu namna kesi hiyo inavyoendeshwa na athari zake za kisheria, kikatiba na kisiasa.

Kwa hiyo, kesi yoyote inayokosa dhamana za msingi za haki itaendelea kutiliwa shaka ndani na nje ya nchi, jambo linaloimarisha mtazamo kwamba mgogoro huu hauwahusu watu wanaoshtakiwa pekee, bali unahusu asili ya uhusiano kati ya dola na sehemu kubwa ya raia wake.

Mwishowe, haki haipimwi kwa hukumu inayotolewa, bali hupimwa kwa uadilifu na usahihi wa mchakato unaoifikisha hukumu hiyo.

Lebo

Maoni yako

You are replying to: .
captcha