Kwa mujibu wa Kitengo cha Kimataifa cha Shirika la Habari la Hawza, Ayatullah Jawad Marawi, Katibu wa Pili wa Baraza Kuu la Hawza nchini Iran, ambaye alisafiri kwenda Iraq kwa ajili ya kushiriki katika hafla ya mazishi ya mwili wa Imam Shahidi, alisema katika mkutano wa wanazuoni na maulamaa wa Hawza uliofanyika Najaf Ashraf kwa kuhudhuriwa na ujumbe wa Hawza ya Qum:
"Kundi la wanazuoni kutoka Hawza Tukufu ya Qum, kutoka jirani na haram ya Karimat Ahlul-Bayt (amani iwe juu yake), pamoja na baadhi ya walimu na wawakilishi wa ofisi za Marajii wakuu wa Taqlid mjini Qum, limekuja Najaf Ashraf baada ya kupata fursa ya kuzuru kaburi tukufu la bwana wetu, Amirul-Muuminin Ali bin Abi Talib (as), ili kuwaletea salamu za Marajii wa Taqlid wa Hawza ya Qum kwa wanazuoni wakubwa, Marajii wakuu, wanafikra, wasomi na vijana mujahidina wa Iraq."
Aliongeza kwamba; jambo hili linathibitisha undani wa mafungamano ya udugu, imani na umoja wa kauli kati ya Hawza hizi mbili tukufu na mataifa haya mawili ndugu, akasema: "Salamu na maamkizi yetu yawafikie watu ndugu wa Iraq, taifa ambalo Kiongozi Shahidi alisema kulihusu: Taifa la Iraq ni taifa kubwa, taifa tukufu, taifa lenye ustaarabu, taifa lenye heshima na lenye azma thabiti."
Mwalimu wa Hawza ya Qum aliendelea kusema: "Baada ya kuwasalimia na kuwapa maamkizi, tumekuja tukiubeba mwili wa Kiongozi wetu Shahidi ili kuukabidhi kwenu, ili ndoto yake ya muda mrefu ya kuzuru kaburi tukufu la Bwana wa Waumini wa Mungu Mmoja na Bwana wa walimwengu wawili, Amirul-Muuminin Ali (as), pamoja na kaburi la Imam Abu Abdillah Al-Hussein (as), itimie."
Mjumbe wa Jumuiya ya Walimu wa Hawza aliendelea: "Tumekuleteeni mwili wake mtukufu, lakini ukiwa umetapakaa damu na ukiwa na viungo vilivyokatwa. Kama mnavyojua, Imam na Kiongozi wetu Shahidi alisimama imara na kwa uthabiti katika njia ya shule ya Abu Abdillah Al-Hussein (as). Na ikiwa mara nyingi katika ziara ya bwana wake alikuwa akikariri kuwa ataitoa mhanga nafsi yake, familia yake na mali yake katika mwezi wa Ramadhani akiwa amefunga na mwenye kiu kwa ajili yake, basi alilidhihirisha hilo kwa vitendo. Aliitoa mhanga nafsi yake, familia yake na mali yake katika njia ya Abu Abdillah Al-Hussein (as), baada ya kusema katika hotuba yake ya mwisho: Mfano wa mimi hauwezi kumpa bai'a mtu kama Yazid. Pia alikuwa akisema: Sisi tupo chini ya bendera ya Abul-Fadhl Al-Abbas (as), na kamwe hatutajuta."
Ayatullah Marawi aliendelea kusema: "Ewe Bwana wetu Shahidi, ewe Bwana wetu Shahidi! Mara nyingi katika hotuba zako ulikuwa ukisema: Ninalishukuru kwa dhati taifa tukufu la Iraq kwa ukarimu wake na mapokezi yake mazuri kwa Umma wa Kiislamu katika siku za Arubaini. Ewe Bwana wetu Shahidi! Leo tazama, kabla ya Arubaini ya Abu Abdillah Al-Hussein (as), jinsi taifa la Iraq, wanazuoni wa Hawza, wasomi, vijana na makabila yake mashujaa walivyounda safu moja na wanavyotamani kukupokea na kukukaribisha."
Alisema: "Mazishi haya makubwa yanayoshuhudiwa na uwepo wa wanazuoni wakubwa, Marajii wakuu, wasomi wa fikra, viongozi wa kisiasa na vijana mashujaa wa Iraq, hayamaanishi tu kumuaga shahidi mkubwa, bali ni ujumbe ulio wazi kwa ulimwengu mzima.
Mazishi haya yanauthibitishia ulimwengu kwamba; mataifa ya Iraq na Iran ni roho moja katika miili miwili, ambayo yameunganishwa kwa itikadi, umoja wa njia na udugu wa kiimani. Kama alivyokuwa akisisitiza Kiongozi Shahidi, Iran na Iraq ni mataifa mawili ambayo miili yao imechangamana, nyoyo zao zimezoeana, na roho zao zimeunganishwa kwa ahadi ya kumwamini Mwenyezi Mungu, kuwapenda Ahlul-Bayt na kufuata mwenendo wa Abu Abdillah Al-Hussein (as)."
Katibu wa Pili wa Baraza Kuu la Hawza alihitimisha kwa kusema: "Uhusiano huu unapaswa kuendelea kuimarika na kuwa imara zaidi siku baada ya siku. Tunamuomba Mwenyezi Mungu awaangamize maadui wa mataifa haya mawili, ayafanye yawe na nguvu zaidi, yenye umoja zaidi na mshikamano mkubwa zaidi, na amuangamize adui Mzayuni mvamizi. Hakika Yeye ni Mwenye kusikia na Mwenye kujibu maombi.
Mola wetu! Tunatamani kutoka kwako dola tukufu ambayo kupitia kwake Utaisimamisha kwa heshima Uislamu na watu wake, na kuwadhalilisha unafiki na watu wake, na utujaalie tuwe miongoni mwa wanaowalingania watu kwenye utiifu Wako na wanaofuata njia Yako. Mola wetu! Miminia subira juu yetu, imarisha nyayo zetu, na utupe ushindi dhidi ya watu makafiri.
Na amani iwe juu yenu na rehema za Mwenyezi Mungu. Ewe Mwenyezi Mungu, mrehemu Muhammad na Aali Muhammad.
Maoni yako