Kwa mujibu wa SShirika la Habari la Hawza, matini kamili ya ujumbe wa Kiongozi Mkuu wa Mapinduzi ya Kiislamu ni kama ifuatavyo:
Kwa Jina la Mwenyezi Mungu, Mwingi wa Rehema, Mwenye Kurehemu.
السَّلامُ علیکَ یا ثاراللهِ وَ ابنَ ثاره وَ الوِترَ المَوتور. السَّلامُ علیکَ وَ علی جَدِّکَ وَ اَبیکَ وَ اُمِّکَ وَ اَخیکَ وَ المَعصومینَ مِن وُلدِک.
Amani zimshukie Imam ambaye wito wenye uhai wa mapinduzi yake ulieneza mwangwi mkubwa na wenye nguvu wa utume wa Mtume Muhammad (saww) hadi katika vilindi vya historia, na kutokana na athari zake yakazaliwa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran. Mapinduzi ambayo tangu msingi wake yalikuwa ya Kihussein, yakajengwa na kukua kwa kaulimbiu na mwenendo wa Imam Hussein (as). Bwana Shahidi wa Iran naye alikulia katika njia hiyo hiyo. Alikuwa wa Kihussein; alifikiri kwa fikra za Kihussein, alitembea kwa mwenendo wa Kihussein, alipigana jihadi na kusimama kidete kwa njia ya Kihussein, aliishi maisha ya Kihussein, na akaimimina damu yake katika njia ya madhehebu ya Hussein (as) hadi akapata daraja ya shahada.
Miongoni mwa wafuasi wa Hussein (as) wapo wale ambao damu yao inapomwagika kwa dhulma katika njia ya Hussein na kwa ajili ya madhehebu na mwenendo wa Hussein (as), Umma wa Kiislamu husimama na kuamka. Wakati huo, zama hizo huunganishwa na Ashura, na mahali hapo huunganishwa na Karbala. Leo pia hamasa hiyo hiyo ya Kihussein imelifufua taifa letu na kulipa sura mpya shule ya fikra ya Imam Khomeini Mkuu na Khamenei Shahidi, huo ndio msisimko wenye kuhuisha unaotokana na mwangwi wa kilio cha kudhulumiwa cha Imam Hussein (as) na wito wake wa «هَل مِن ناصرٍ یَنصُرُنی», ambao umeiamsha Iran, kisha Iraq na baadaye nchi nyinginezo, na kuutikisa msingi wa batili.
Kwa mnasaba huu, napenda kutoa shukrani zangu za dhati kwa mahudhurio ya kushangaza, ya kuvunja nguvu za maadui na ya kihistoria ya mamilioni ya wananchi katika miji na vijiji vya Iran na Iraq, hususan Tehran, Qom, Najaf, Karbala na Mashhad.
Taifa letu ni mtafutaji wa kisasi cha damu ya Hussein (as), kwa miaka mingi taifa hili kubwa limewatoa wanawe muhanga katika njia ya Hussein (as) na katika vita dhidi ya maadui wa Hussein na mwenendo wake. Na sasa pia linatafuta kisasi cha damu yake na cha Hussein wa zama hizi.
Sasa namwelekea Kiongozi wetu Shahidi na kusema: Ewe uliyeuawa kwa dhulma! Ewe mwenye kudhulumiwa lakini mwenye utukufu! Ewe mja mwema wa Mwenyezi Mungu! Sasa tunapokuaga kwa macho yaliyojaa machozi na nyoyo zilizovunjika, tunakuahidi kwamba tutailinda shule yako ya fikra, na tutaifuata kwa uthabiti njia iliyonyooka uliyoichora. Hatutaogopa magumu katika njia hii, na kama ulivyokuwa wewe, tutashikamana na bishara na ahadi za Mwenyezi Mungu.
Tunatoa ahadi kwamba tutalipiza kisasi cha damu yako takatifu na damu ya mashahidi wote wa vita hivi viwili kutoka kwa wauaji wahalifu na waliopoteza heshima. Kisasi hiki ni matakwa ya taifa letu, na bila shaka ni lazima kitekelezwe. Wahalifu hawa, ambao orodha yao kamili kuanzia viongozi wao hadi walio chini yao ipo, wataondoka na matumaini yao ya kufa kwa utulivu kitandani yakiwa yamezikwa pamoja nao.
Wanapaswa kujua kuwa jambo hili halitegemei uwepo wangu binafsi au wa viongozi wengine, tuwepo au tusiwepo jambo hili litatimia, na si muda mrefu watu huru kutoka pembe mbalimbali za dunia watatekeleza kila mmoja sehemu ya jukumu hili la Mwenyezi Mungu.
Ewe Baba Shahidi wa Umma! Na iwe tamu kwako sharbati ya shahada ambayo maisha yako yote ulikuwa ukiitamani, hongera kwa kuvaa vazi la shahada kwa mwili ambao umebeba alama za Mama yako Zahra al-At'har, babu yako Aba Abdillah al-Hussein na Aba al-Fadhl al-Abbas (as).
Na nyinyi enyi maswahaba wake waliodhulumiwa, mliofanyiwa shambulio la kushtukiza na adui mkapata shahada; hongereni, kwani sasa mmekuwa wageni wa yule Bwana ambaye huenda mara nyingi mlionja huruma na upole wake. Yule Bwana ambaye ni mlango wa rehema za Mwenyezi Mungu kwa wote, na hasa kwa watu wa ardhi hii, sasa ndiye mwenye kuwakaribisha, na jirani yake salama yamekuwa makazi yenu.
Na wewe ewe Bwana mwenye cheo cha juu! Ewe mtukufu! Ewe Imam mwenye huruma! Ewe Aba al-Hasan ar-Ridha al-Murtadha, ambaye rehema bora kabisa za Mwenyezi Mungu ziwe juu yako! Sasa mwili uliokatwakatwa vipande vya mmoja wa watumishi wa huduma yako na wa Ahlul-Bayt watoharifu, baada ya miaka mingi ya juhudi na mapambano yasiyokoma, pamoja na miili ya mashahidi wa familia yake ambao kila mmoja anamkumbusha mmoja wa mashahidi wa Karbala, inapumzika katika ardhi hii takatifu hadi siku ambayo, kwa amri ya Mwenyezi Mungu, Jua linaloangaza ulimwengu, Hadhrat Baqiyyatullah (aj), litakapojitokeza kutoka nyuma ya mawingu ya ghaiba na kuuangazia ulimwengu nuru ya rehema za Mwenyezi Mungu.
Siku hiyo, ambayo tunatumaini ifike hivi karibuni sana, nyota miongoni mwa wakweli, mashahidi na mawalii zitamsindikiza. Nasi tunatumaini kwamba Bwana Shahidi wetu atakuwa mmoja wao, na kwa mara nyingine ataonesha mandhari yenye kung'ara ya jihadi na kutimiza ahadi ya «أَلَسْتُ», na huenda hawa maswahaba wake pia wakawa pamoja naye siku hiyo.
Ewe Mola mwenye huruma! Tunamkabidhi kwako Bwana wetu ambaye alitumia kila alichokuwa nacho katika njia yako, pamoja na maswahaba wake mashahidi, ili waendelee kunufaika na rehema, fadhila na uangalizi wako kama walivyokuwa duniani, bali kwa kiwango kikubwa zaidi na cha juu zaidi.
Mwishoni, kwa mara nyingine tunatoa mkono wa pole kwa Bwana wetu Hadhrat Baqiyyatullah (aj), na tunamuomba mtukufu huyo azielekeze dua zake takatifu kwa Bwana Shahidi wa Iran, maswahaba wake na mashahidi wote. Pia tunamuomba Mwenyezi Mungu Mtukufu awape mashahidi wote daraja za juu, awajalie walioachwa nyuma subira na malipo mema, na kwa taifa lililodhulumiwa la Iran alipe ushindi na nusura ya hakika iliyo karibu, Inshaallah.
Sayyid Mujtaba Husseini Khamenei
Maoni yako