Kwa mujibu wa Kitengo cha tarjama cha Shirika la Habari la Hawza, kukutana na Ayatullah al-Udhma Imam Sayyid Ali Khamenei daima imekuwa ndoto iliyoshughulisha fikra za watu wengi; si tu kwa sababu ya kukutana na shakhsia ya kidini na kisiasa, bali kwa sababu ya kukutana na Imam mkuu katika uongozi, uchamungu, fiqhi na ijtihadi, kama alivyokuwa akimwelezea Sayyid Shahidi, Sayyid Hassan Nasrallah.
Watu wengi walimfahamu Imam kutoka mbali kupitia maneno yake, misimamo yake na hotuba zake zilizodumu kwa miongo kadhaa. Ingawa walikuwa mbali naye kijiografia, walikuwa karibu naye kimawazo, na hivyo ndani ya fikra zao ukajengeka mfano wa uongozi ambao ni nadra kupatikana katika historia.
Katika muktadha huo, katika mahojiano ya awali kwenye podikasti "Ala al-Ahd", Luteni Jenerali Abbas Ibrahim, aliyekuwa Mkurugenzi Mkuu wa Usalama wa Umma wa Lebanon, alisimulia kwa kina mkutano wa kuvutia uliobeba maana nyingi za kisiasa na kiroho.
Anasema: "Nilikuwa na kikao na Sayyid Shahidi Hassan Nasrallah. Katika mazungumzo yetu nilimwambia kwamba nilikuwa nimealikwa kusafiri kwenda Iran, kisha nikamuuliza ikiwa kuna jambo lolote alilokuwa akihitaji kutoka huko. Akanijibu kwa kuniuliza: 'Wewe mwenyewe unahitaji nini?' Nikasema: 'Natamani kukutana na Hadhrat Sayyid Qaid Ali Khamenei.' Akasema: 'Inshaallah, kheri itakuwa.'"
Ibrahim anaendelea na simulizi yake kwa kuelezea jinsi mambo yalivyobadilika haraka na kuwezesha mkutano huo. Anasema: "Baada ya muda mfupi, nilikuwa Tehran katika kikao rasmi na Waziri wa Usalama. Kabla hata ya kupita saa moja, waziri alipokea karatasi kutoka kwa mtu fulani, kana kwamba ghafla aliarifiwa kuwa kikao kimekwisha, akaniambia: 'Sayyid, kikao kimeisha, tunaomba radhi.' Kisha wakanisindikiza hadi kwenye gari, walipofika kwenye mlango wa gari waliniambia: 'Laiti na sisi tungeweza kuja pamoja nawe.' Hapo ndipo nilihisi kwamba nilikuwa nikielekea mahali muhimu sana."
Luteni Jenerali Ibrahim anaongeza: "Baadaye walinifikisha mahali pa mkutano, baadhi ya viongozi walikuwa pamoja nami, akiwemo Ali Shamkhani (Mshauri wa Imam) na Gholam-Ali Haddad Adel (Spika wa zamani wa Bunge la Iran). Baada ya takribani dakika tano, Hadhrat Imam Khamenei aliingia, akatusalimia na akazungumza nasi kuhusu hali ya Lebanon, kisha akavua shali yake na kuniwekea shingoni, akisema: 'Palestina ni amana iliyo shingoni mwenu, mfikishieni Sayyid salamu zangu, karibuni.'"
Luteni Jenerali Ibrahim anahitimisha simulizi yake kwa kueleza kwamba; aliswali Swala ya Adhuhuri nyuma ya Imam Khamenei, kisha akaagana naye.
Anaamini kwamba huo ndio ulikuwa mkutano wake wa kwanza na wa pekee na Imam Khamenei, lakini uliacha athari kubwa sana ndani yake, hasa kutokana na nasaha na ujumbe alioupokea, juu ya yote, ulikuwa ni msisitizo kwamba Palestina ni amana na jukumu lililo juu ya mabega ya Umma.
Kilichompata Luteni Jenerali Ibrahim ni ushahidi mwingine wa nafasi ya Palestina katika fikra na dhamiri ya Kiongozi huyo. Palestina daima ilikuwa dira isiyobadilika katika hotuba zote za "Imam wa Waliodhulumiwa", na lilikuwa suala la msingi ambalo alisisitiza kila alipokutana na watu au kutoa msimamo, ili kuthibitisha umuhimu wake wa kipekee.
Imam Shahidi aliichukulia Palestina kuwa ni suala la Umma mzima na jukumu la kidini lililo juu ya mabega ya Waislamu wote—watu binafsi na serikali zao—wala si faili la muda mfupi au chaguo la kisiasa.
Aidha, alikuwa akisisitiza kwamba; kuiunga mkono Palestina na kuisaidia harakati yake ya muqawama ni mwendelezo wa kanuni ya kukataa dhulma na kukabiliana na ukaliaji wa mabavu, ndani ya mfumo wa mradi wa uamsho unaolenga kuikomboa ardhi na mwanadamu.
Maoni yako