Kwa mujibu wa Kitengo cha tarjama cha Shirika la Habari la Hawza, Sheikh Ahmad Qabalan, Mufti Mkuu wa Jaafari wa Lebanon, alitoa ujumbe wa kitaifa uliowaelekeza wananchi wa Lebanon na makundi ya kisiasa, akisema:
“Enyi wananchi wapendwa wa Lebanon na enyi nguvu za kisiasa za kitaifa, ninatamka kwa ajili yenu na kwa ajili ya historia, kwamba leo tumesimama mbele ya wakati ambao ni vigumu hata kuelezea ukubwa wa janga la ‘Makubaliano ya Mfumo’ (Makubaliano ya Washington) yaliyotiwa saini na utawala wa sasa wa Lebanon. Hata mkuu wa kijiji anayejidai kuwa mtetezi wa mamlaka ya taifa asingekubali kutia saini makubaliano ya aina hii, lakini Rais Joseph Aoun pamoja na serikali yake walifanya hivyo na kuiingiza nchi katikati ya mgogoro mkubwa wa kitaifa na janga la kiusalama na kisiasa ambalo halijawahi kushuhudiwa hata katika kipindi cha Makubaliano ya tarehe 17 Mei mwaka 1983.”
Aliongeza: “Rais Aoun na timu yake, ambao ni washirika katika mpango huu wa ‘kujifanyia maamuzi peke yao’ kama alivyouita Walid Jumblatt, wanafahamu vizuri maelezo ya majanga yaliyomo ndani ya makubaliano hayo pamoja na masharti yake yaliyofichwa na viambatisho vyake vya kiusalama; viambatisho vinavyolenga kiini cha maslahi ya Lebanon na dhana ya kuendelea kuwepo kwake kama dola yenye mamlaka kamili. Sasa ni wakati wenu, enyi Walebanon, kufanya uamuzi, suala hili halihusu kusini mwa Lebanon pekee, ambayo kwa miongo mingi imelipa gharama kubwa zaidi katika kuitetea nchi hii. Kilichotokea ni makubaliano ya kishetani yaliyolenga kuitumbukiza Lebanon katika mzunguko mpya wa fitna za ndani ambazo zikichochewa, zitachoma kila kitu na kila mtu katika nchi hii pendwa.”
Sheikh Qabalan aliendelea kusema: “Leo vyombo vya habari vya Tel Aviv vinashangilia jambo hili na vinaamini kuwa makubaliano haya yamehamisha vita kutoka nje na kuviingiza ndani ya Lebanon, ili Lebanon ibakie ikizama katika migogoro yake ya umwagaji damu kwa manufaa ya usalama wa Israel. Kwa msingi huu, makubaliano haya yanaipa Tel Aviv uwezo wa kuichoma Lebanon kwa mikono ya Walebanon wenyewe, Rais Joseph Aoun na timu yake wanabeba jukumu kamili la janga hili la kitaifa, hatari zaidi ni kwamba Rais Aoun anaamini anaweza kufanikisha kile ambacho Tel Aviv na Washington zilishindwa kukifanya kwa kuligombanisha jeshi dhidi ya Muqawama na kuiingiza nchi katika moto wa vita. Ni kana kwamba hakusoma historia, hakuona ukubwa wa mapambano ya kizalendo ya kihistoria, wala hakujifunza kutokana na fitna ya vita vya wenyewe kwa wenyewe na madhara yake.”
Akiashiria kauli za Nabih Berri na Walid Jumblatt, alisema kwamba; makubaliano hayo ni hati inayoitumikia harakati ya Kizayuni na lengo lake ni kutekeleza mpango wa “Israel Kubwa” katika eneo la Mashariki ya Kati.
Mufti wa Jaafari wa Lebanon aliongeza: “Baada ya Washington na Tel Aviv kushindwa katika vita vya eneo hili, sasa wamerejea kupitia utawala wa kisiasa ili kupenya ndani ya Lebanon na kutulazimisha kukubali kile ninachokiita ‘Makubaliano ya Tetemeko la Ardhi’, ambayo yanampa Israel gaidi mamlaka ya kutawala usalama na mamlaka ya Lebanon, jeshi lake na uongozi wake wa kisiasa. Kwa kipimo chochote kile, hili ni janga kubwa na haliwezi kukubalika kamwe.”
Sheikh Qabalan aliendelea kusisitiza: “Zimeni moto wa fitna unaochochewa na utawala wa sasa kabla haujaiteketeza Lebanon yote. Lebanon haipaswi kuungua mbele ya macho yetu kwa ajili ya timu iliyowekwa kutekeleza fitna hii, Rais Aoun kwa sasa anafanya mazoezi ya utawala wa mtu mmoja na udikteta wa kisiasa na kiusalama kwa namna inayotishia maslahi makuu ya Lebanon. Tunachokitaka ni Lebanon inayojengwa juu ya ushirikiano wa kitaifa na iliyo mbali na fitna zote za Marekani na Uzayuni.”
Alisema pia: “Ninawaambia ninyi, enyi wananchi wapendwa wa Lebanon: yale yanayowakumba watu wa Kusini, Dhahiya na Bonde la Bekaa ni vita vya kimataifa vinavyotumia silaha ambazo hazijawahi kushuhudiwa, huku kukiwa na serikali ya utendaji inayotafuta kulipiza kisasi ambayo imeiweka hatima ya Lebanon mezani kwa Netanyahu na Trump. Serikali hiyo haijali Kusini wala watu wake na haina dhamiri yoyote ya kitaifa, hali hii haiwezi kutenganishwa na uhalisia wa mchezo wa kimataifa unaolenga kuiangamiza Lebanon, kile ambacho Muqawama imekitoa katika kuitetea Lebanon ni simulizi la kishujaa lisilo na mfano katika nyanja zote, hata hivyo, utawala wa sasa unataka kuinyang'anya silaha ya kitaifa ya Muqawama, ilhali silaha hiyo ndiyo imekuwa ikiitetea Lebanon, wananchi wake, msingi wa kuwepo kwa taifa hili na makundi yake yote yenye heshima, na itaendelea kufanya hivyo.”
Mufti wa Jaafari aliongeza: “Utawala wa sasa unajua wazi kwamba kuuondolea Muqawama silaha yake, ambayo ndiyo dhamana ya usalama wa Lebanon na mamlaka yake ya kitaifa, ni jambo lisilowezekana, hata kama Mashariki ya Kati yote ingeteketea kwa moto. Hata hivyo, bado unataka kujitumbukiza katika fitna hii ya hatari kwa manufaa ya Tel Aviv na Washington, hili ni suala la kitaifa kwa kiwango cha juu kabisa na pia ni suala la kikanda kwa kiwango cha juu kabisa, kosa lolote katika kufanya mahesabu litatuingiza katikati ya vita vya kikanda vya maangamizi, na zama za Marekani na Uzayuni kutawala Lebanon kwa mabavu zimekwisha.”
Maoni yako