Kwa mujibu wa Kitengo cha Kimataifa cha Shirika la Habari la Hawza, kikinukuu Shirika la Habari la Anadolu, Recep Tayyip Erdoğan, Rais wa Uturuki, akirejelea kuendelea kwa migogoro na vita katika eneo hilo, alitangaza kuwa kutoka Ghaza hadi Lebanon, sauti za maumivu za watu waliodhulumiwa bado zinaendelea kusikika.
Erdoğan alisema kuwa; Israel tangu kuanzishwa kwake imekuwa ikitishia amani, uthabiti, ustawi na usalama wa eneo hilo.
Aliongeza kusema: “Ukaliaji wa Palestina na mauaji ya kimbari dhidi ya Wapalestina yanaendelea kwa mfumo uliopangwa, huko Ghaza mbele ya macho ya ulimwengu watu 73,000 wasio na hatia wameuawa. Mauaji haya ya kimbari yanaendelea, iwe kwa njia ya mauaji ya moja kwa moja au kwa njia ya mzingiro na kutengwa kwa namna isiyo ya kibinadamu. Israel, ambayo imetekeleza moja ya mauaji ya kimbari yenye umwagaji damu mkubwa zaidi katika historia ya kisasa, wakati huo huo imeishambulia Iran na baadaye imeanza pia uvamizi kwa Lebanon.”
Akizungumzia kuendelea kwa uwepo wa kijeshi wa Israel nchini Lebanon, Erdoğan alisema kuwa; licha ya malalamiko ya nchi za eneo hilo, ikiwemo Uturuki, Israel imekataa kujiondoa kutoka Lebanon na inaendeleza operesheni zake za kijeshi, kwa mujibu wa Erdoğan, tangu tarehe 2 Machi hadi sasa, idadi ya waliouawa nchini Lebanon imefikia watu 3,700, huku waliojeruhiwa wakifikia watu 11,400.
Rais wa Uturuki pia alisisitiza kuwa; Israel wakati huohuo inajaribu kuyumbisha baadhi ya nchi za Afrika na eneo la Bahari ya Mediterania. Aliitaja serikali ya Israel kuwa ni “kitovu cha migogoro na kiwanda cha fitna”, na kusema kwamba; utawala huo unajishughulisha na kuzalisha ukosefu wa usalama na mivutano katika eneo kubwa la kanda hiyo.
Erdoğan, akikosoa mwitikio usioridhisha wa jumuiya ya kimataifa kuhusu sera za Israel, alisema: “Israel, chini ya serikali yake ya sasa imekuwa jasiri kupita kiasi kiasi, imegeuka kuwa tishio si kwa eneo hili pekee bali kwa wanadamu wote, mashambulizi ya Benjamin Netanyahu na mtandao wa wahalifu unaoshirikiana naye dhidi ya Syria na Lebanon sasa, mbali na kuzitishia nchi hizi mbili ndugu, pia yanaitishia Uturuki.”
Akisisitiza kwamba Syria na Lebanon ni nchi mbili huru, aliongeza kusema: “Syria na Lebanon ni sehemu ya jiografia ya mapenzi na udugu wa Uturuki, Damascus na Beirut ni miji dada ya Istanbul, usalama wa Uturuki hauanzi tu katika mipaka ya Hatay; unaanzia Aleppo na Damascus, usalama wa Uturuki pia unaanzia Beirut, hatutanyamaza mbele ya hatua yoyote ya kulazimishwa katika nchi zetu ndugu, na hatutapuuza shambulio lolote dhidi yao.”
Erdoğan pia alionya kwamba Ankara inafahamu vyema malengo na mipango ya wapinzani wake, na akaongeza: “Tunafahamu vizuri kabisa lengo la mwisho la dhana inayoitwa ‘Ardhi ya Ahadi’, kwa msaada wa Mwenyezi Mungu, hatutaruhusu kamwe ndoto hiyo kutimia.”
Rais wa Uturuki, akizungumzia maendeleo ya Mashariki ya Mediterania na kisiwa cha Cyprus, alisema kuwa; Ankara inafuatilia kwa karibu juhudi za kuzua mivutano katika eneo hilo, Alisema: “Baadhi ya miundo midogo ambayo tamaa zake ni kubwa mno kuliko uwezo wake halisi, imepanda katika mashua ya fitna ya Israel na kuchukua jukumu la wakandarasi wa Uzayuni, hakuna anayepaswa kutafuta vituko vya hatari wala kufuata sera za mtandao wa wahalifu wa Kizayuni ikiwa haki na maslahi ya Uturuki na Waturuki wa Cyprus katika Mashariki ya Mediterania yatakuwa shabaha ya mashambulizi, jibu letu litakuwa wazi kabisa na lenye msimamo mkali.”
Erdoğan pia alisema kuwa; Israel, kwa kutumia kimakosa ukimya wa jumuiya ya kimataifa, imezuia eneo hili kufikia amani, uthabiti na usalama.
Alisisitiza kwamba; kuidhibiti Israel na kuilazimisha kuheshimu sheria za kimataifa si suala la nchi chache tu tena, bali limekuwa jukumu la pamoja kwa wanadamu wote.
Rais wa Uturuki, akilinganisha hali ya sasa na miaka iliyotangulia kabla ya kuanza kwa Vita vya Pili vya Dunia, alisema: “Miaka themanini na mitano iliyopita, ukimya mbele ya Hitler ulisababisha vifo vya takriban watu milioni 80, leo pia kosa hilohilo linaendelea kurudiwa, mauaji ya kimbari yanayofanywa na Netanyahu na baraza lake la mawaziri yanakabiliwa na ukimya na kutokujali kwa kiwango kilekile kama ilivyokuwa kwa uhalifu wa Hitler.”
Alionya kwamba; ikiwa Israel haitadhibitiwa, athari za hatua zake hazitabaki katika eneo hili pekee bali zitaathiri dunia nzima.
Mwishoni, Erdoğan alisisitiza kwamba; Uturuki, licha ya vikwazo na hujuma zote za Israel, itaendelea na juhudi zake za kuleta amani na uthabiti katika eneo hili, na itatumia uwezo wake wote wa kidiplomasia ili kukomesha vita na umwagaji damu.
Pia aliwaambia wananchi wa Ghaza na Lebanon kuwa: “Tunawatumia ndugu zetu wa Ghaza na Lebanon ujumbe wetu wa mshikamano, na tunasisitiza tena kwamba Uturuki, kama ilivyokuwa pamoja nao hadi sasa, itaendelea kusimama pamoja nao pia katika siku zijazo.”
Maoni yako