Ijumaa 5 Juni 2026 - 10:47
Sheikh Ahmad Qabalan: Tunajivunia uhusiano wetu wa milele na Iran

Hawza/ Mufti Mkuu wa Jaafaria na mwanazuoni wa Kishia wa Lebanon amesema kuwa: Sitisho lolote la vita au njia yoyote itakayotufikisha kwenye matokeo haya, pamoja na mambo yanayohitajika kwa ajili ya kuimarisha mizani mpya ya nguvu, linatokana na mambo mawili makuu.

Kwa mujibu wa ripoti ya Kitengo cha tarjuma cha Shirika la Habari la Hawza, Hujjatul-Islam Sheikh Ahmad Qabalan, Mufti Mkuu wa Kijaafari na mwanazuoni wa Kishia wa Lebanon, katika taarifa amesema: “Sitisho lolote la vita au njia yoyote itakayotufikisha kwenye matokeo haya, pamoja na kile kinachohitajika kwa ajili ya kuimarisha mizani mpya ya nguvu, kinatokana na mambo mawili makuu: kusimama kwa kishujaa na kihistoria kwa Muqawama pamoja na tishio kubwa la Iran la kuingia vitani dhidi ya Israeli ya kigaidi.”

Alibainisha kwamba Nabih Berri (Spika wa Bunge la Lebanon), kupitia mlinganyo huu, alijenga ngome ya Muqawama ambayo iliilinda serikali ya Lebanon pamoja na misingi yake ya kihistoria dhidi ya kamari ya bei rahisi ya mkondo wa kisiasa unaotawala.

Sheikh Qabalan aliongeza: “Mandhari hii pamoja na vipengele vyake vyote inatuweka katikati ya medani za mapambano ya kihistoria ambayo Muqawama imepitia katika kipindi cha miezi mitatu iliyopita katika mstari wa mbele (katika eneo lenye upana wa kilomita 4 hadi 8 kutoka mipaka ya kusini); maeneo ambayo ndani yake makumi ya mizinga, magari ya kivita na vifaa vingine vya kijeshi vya gaidi Israeli viliharibiwa, kusagwa na kuchomwa moto. Aidha, siku zijazo zitafichua ukubwa halisi wa maelfu ya waliouawa na kujeruhiwa miongoni mwa maafisa na askari wa jeshi la Kizayuni.”

Tunajivunia uhusiano wetu wa milele na Iran

Mufti wa Jaafaria alisisitiza: “Muqawama unauthibitishia ulimwengu mzima kwamba ni nguvu ya kijeshi ya kishujaa ya kitaifa, nguvu ya kipekee ya kikanda na sehemu kuu ya nguvu za eneo hili pamoja na muundo wake mpya, tunajivunia uhusiano wetu wa milele na Iran, kwa sababu Iran ni nchi ambayo iliwahi kuinusuru Lebanon na Muqawama wake wakati watu wa karibu na wa mbali walipoisaliti; hususan wale waliokuwa wakisisitiza kutenganisha mkondo wa Lebanon na mazungumzo ya Iran ili kuigeuza kuwa zawadi ya bure kwa mchinjaji wa Tel Aviv, yaani Netanyahu.”

Akikosoa vikali mkondo wa kisiasa unaoitawala Lebanon, alisema: “Haijawahi kuwepo siku yenye fedheha na kukatisha tamaa zaidi kwa utawala huu ambao uliiacha nchi, wananchi wake na maeneo yake nyeti ya mipakani kuliko leo. Mpango wa sitisho la vita kwa mfumo huu, wakati wowote utakapotimia, utakuwa ushindi mkubwa zaidi kwa Muqawama na Lebanon ya kitaifa, na kushindwa kukubwa zaidi kwa Israeli pamoja na utawala wowote uliosaliti nchi na watu wake na kujigeuza kuwa chombo kinachoitumikia Washington na kambi yake ya kikanda, yaani Tel Aviv; huu ndio ukweli wa jambo hili.”

Tunakaribisha nafasi ya jeshi la Lebanon katika kuilinda mipaka ya mamlaka kwa msingi wa kukabiliana na Israeli

Sheikh Qabalan alifafanua: “Enzi ya orodha za Marekani na Kizayuni imekwisha milele, na wakati wa ‘kuifanya Lebanon kuwa ya Kizayuni’ umemalizika baada ya kushindwa kwa vita hivi vya kimataifa dhidi ya Lebanon yenye Muqawama na itikadi ya kitaifa. Lengo letu ni Lebanon yenye mamlaka kamili, heshima na mshikamano wa kuishi pamoja kwa amani, mbali na miradi ya kuifanya kuwa ya Kimarekani na njia ovu za Uzayuni.”

Aliendelea kusema: “Aliyepigana, aliyesimama imara na kuharibu ghala la silaha la Israeli ni Muqawama wenyewe, ambao utabaki kuwa mlinzi wa milele wa mipaka ya mamlaka ya Lebanon, tunakaribisha nafasi ya jeshi la Lebanon katika kuilinda mipaka ya mamlaka kwa msingi wa kukabiliana na Israeli.”

Aliongeza: “Tutapambana na nafasi yoyote kutoka kwa upande wowote ambao utakuwa kwa manufaa ya Israeli, enzi ya ‘taqiyya ya kitaifa’ imekwisha, na yeyote aliyekuwa akitarajia kuuawa kwetu au kutuondoa amekata tamaa, hatutakubali tena maridhiano yoyote kwa gharama ya Muqawama, wananchi na kujitolea kwao kwa taifa.”

Harakati ya Amal na Hizbullah ni roho moja katika miili miwili na Muqawama mmoja

Akigusia kwamba Kasri la serikali linapaswa kutumikia maslahi ya Lebanon na si Washington au Tel Aviv, alisema: “Siku za kisiasa za Netanyahu zimepita, utawala wa sasa umeacha kuilinda Lebanon, ukalizuia jeshi kutekeleza jukumu lolote la ulinzi na ukafanya kosa kubwa.”

Sheikh Qabalan akiwaelekea watu wa kusini mwa Lebanon, Dhahiya na Biqaa alisema: “Hakuna kitu kikubwa zaidi kuliko kujitolea kwa Muqawama, na hakuna jambo tukufu zaidi kuliko ushujaa wenu, mtarudi kwenye ardhi tukufu zaidi, na hatutaruhusu utawala wowote kufanya biashara juu ya mamlaka ya Lebanon na uwezo wa Muqawama.”

Mwisho alisisitiza kwa kusema: “Harakati ya Amal na Hizbullah ni roho moja ndani ya miili miwili na Muqawama mmoja, mabadiliko ya msingi ya mfumo wa kimataifa na mwanzo wa dunia yenye nguvu nyingi yamechorwa kwa mikono ya Tehran na Muqawama wa Lebanon, na kesho itakuwa siku nyingine yenye msingi wa ushirikiano wa kitaifa na mamlaka ya Lebanon.”

Lebo

Maoni yako

You are replying to: .
captcha