Kwa mujibu wa mwandishi wa Shirika la Habari la Hawza akinukuhu Idara ya Mahusiano ya Umma ya Mshauri wa Utamaduni wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran nchini Indonesia, mkutano wa kimataifa wa kumbukumbu ya Shahidi Ayatullah Sayyid Ibrahim Raisi ulifanyika kwa ushiriki wa Dkt. Sharifani, mwakilishi wa Kiongozi Mkuu nchini Indonesia, Dkt. Boroujerdi, balozi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, Dkt. Yahya Jahangiri, mshauri wa utamaduni wa Iran nchini Indonesia, viongozi wa kidini na kitamaduni wa Indonesia pamoja na kundi la wanafikra mjini Jakarta, katika mkutano huu, nafasi ya kimkakati ya Shahidi Raisi katika kuitetea Qur'ani Tukufu na juhudi zake za kuhuisha ustaarabu wa ulimwengu wa Kiislamu zilichunguzwa kwa kina.
Mwanzoni mwa mkutano huo, Hujjatul-Islam Dkt. Sharifani, mwakilishi wa Ofisi ya Kiongozi Mkuu nchini Indonesia, pamoja na kufafanua vipengele mbalimbali vya shakhsia ya Shahidi Raisi, alieleza hatua zake za kishujaa dhidi ya wimbi la kuchomwa moto kwa Qur'ani mwaka 2023 katika baadhi ya nchi za Ulaya na kusema: “Katika mazingira ambayo maadui wa Uislamu, kwa msaada wa baadhi ya vyombo vya habari vya Magharibi, walikuwa wakijaribu kueneza chuki dhidi ya Uislamu, Shahidi Raisi katika jukwaa la juu kabisa la kimataifa ndani ya Mkutano Mkuu wa Umoja wa Mataifa, kwa kuinua Qur'ani Tukufu mkononi mwake, alithibitisha kwamba maneno ya Mwenyezi Mungu hayatatoweka kwa moto wa chuki na uadui.”
Katika mwendelezo wa hafla hiyo, Dkt. Muhammad Boroujerdi, balozi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran nchini Indonesia, akisisitiza kwamba; msimamo wa Shahidi Raisi katika Umoja wa Mataifa haikuwa hatua ya kisiasa ya muda mfupi, aliongeza: “Tukio hilo lilikuwa ni taswira ya maisha yake yote ya kuishi pamoja, kuwa karibu na kutekeleza mafundisho ya Qur'ani. Yeye baada ya kupitia hatua za imani na ufahamu wa Qur'ani, alifikia daraja ambalo liliwezesha kutetea kwa ustahiki Kitabu hiki cha mbinguni.”
Katika sehemu nyingine ya mkutano huo, msaidizi mkuu wa Waziri wa Dini wa Indonesia, huku akisisitiza dhana ya “uhuishaji wa Kiislamu”, alieleza kwamba; ulimwengu wa Kiislamu unahitaji kurejea kwenye maadili ya asili na kuimarisha umoja.
Akiashiria mafanikio ya Iran katika nyanja za kisayansi na ustaarabu, alitoa wito kwa nchi za Kiislamu kunufaika na tajiriba hizi zilizofanikiwa.
Afisa huyo wa Indonesia, huku akikosoa tofauti za kimadhehebu, alisisitiza: “Migogoro kati ya Shia na Sunni inapaswa kufikia mwisho, na mazungumzo ya umoja wa Kiislamu yanapaswa kujengeka na kuimarishwa miongoni mwa wasomi pamoja na kizazi cha vijana.”
Pia alielezea elimu ya kisasa na upatikanaji wa elimu bila mipaka, kuwa funguo za maendeleo ya Umma wa Kiislamu na kusisitiza kwamba; Waislamu hawapaswi kuogopa kujifunza maarifa kutoka katika vyanzo vingine vyenye manufaa.
Mwishoni, wazungumzaji walisisitiza umuhimu wa kuendeleza mazungumzo baina ya dini mbalimbali kwa ajili ya kufikia uelewano wa pamoja na kuishi kwa amani, na walitoa wito wa kufanyika kwa mikutano ya mara kwa mara kati ya wanafikra wa kidini kwa ajili ya kuimarisha uelewa na umoja wa Umma wa Kiislamu.
Washiriki wa hafla hiyo, sambamba na kuenzi kumbukumbu ya “Shahidi wa Jamhuri”, walisisitiza kuendelea kuifuata njia yake katika mwelekeo wa kuinua na kuimarisha malengo ya Kiislamu.
Maoni yako