Kwa mujibu wa kitengo cha kimataifa cha Shirika la Habari la Hawza, kwa kunukuu Shirika la Habari la Anadolu, Wizara ya Mambo ya Nje ya Uturuki ilitoa taarifa ya kulaani hatua ya waziri mmoja wa Israel kwa kutumia vurugu za maneno na kimwili dhidi ya wanaharakati wa “Msafara wa Kimataifa wa Sumud”, na kutaka kuachiwa huru kwa haraka na kwa usalama kwa waliokamatwa wote.
Katika taarifa ya Wizara ya Mambo ya Nje ya Uturuki imeelezwa kwamba, nchi hiyo pamoja na serikali nyingine husika zinaendelea kufanya juhudi zote zinazohitajika kwa ajili ya kuwaachia huru raia wa Uturuki na wanachama wengine wa msafara huo ambao wamekamatwa kufuatia uingiliaji wa Israel katika maji ya kimataifa.
Taarifa hiyo, huku ikilaani tabia ya waziri mmoja wa Israel dhidi ya wanaharakati waliokamatwa, ilisisitiza: “Waziri huyu ambaye anahesabiwa kuwa mmoja wa sura kuu za mauaji ya kimbari huko Ghaza, kwa mara nyingine ameweka wazi fikra za kikatili na zisizo za kibinadamu za serikali ya Benjamin Netanyahu.”
Wakati huo huo, Mustafa Çiftçi, Waziri wa Mambo ya Ndani wa Uturuki, katika ujumbe aliouchapisha kwenye mitandao ya kijamii, alilaani vikali shambulio la Israel dhidi ya msafara uliokuwa umebeba misaada ya kibinadamu kwa ajili ya Ghaza pamoja na kukamatwa kwa wanaharakati wake.
Akirejelea kufungwa mikono kwa wanaharakati hao, tabia za udhalilishaji na mashinikizo ya kisaikolojia dhidi yao, alisema; vitendo hivyo ni ukiukaji wa wazi wa haki za binadamu na sheria za kimataifa, na akasisitiza: “Hakuna mwanadamu huru anayeweza kukubali tabia kama hizi.”
Çiftçi pia, huku akirejelea kauli ya Recep Tayyip Erdogan kwamba “dunia ni kubwa zaidi kuliko nchi tano”, alisisitiza kuwa hakuna mfumo unaojengwa juu ya dhulma na kupuuza dhamiri ya kibinadamu ambao unaweza kubaki milele.
Kwa upande mwingine, Burhanettin Duran, mkuu wa Kituo cha Mawasiliano cha Rais wa Uturuki, pia aliielezea tabia ya waziri huyo wa Israel dhidi ya wanaharakati wa Msafara wa Sumud kuwa ni “ya kishenzi”, na akasema vitendo hivyo vitaandikwa katika kurasa za giza za historia.
Duran katika taarifa yake alisisitiza kwamba; kuingilia kwa maneno na kimwili dhidi ya raia wasio wanajeshi kwa mara nyingine kumeweka wazi namna Israel inavyopuuzia sheria na maadili ya kibinadamu, alitaka kurejea salama kwa waliojitolea waliokamatwa katika nchi zao, na akaongeza kuwa Uturuki itaendelea kuwaunga mkono wananchi wa Ghaza na kutetea haki zao katika majukwaa yote ya kimataifa.
Pia Omer Celik, msemaji wa Chama cha Justice and Development cha Uturuki, aliuelezea Msafara wa Sumud kuwa ni “alama ya heshima ya kibinadamu” na kulaani vurugu zilizotumika dhidi ya wanaharakati wa msafara huo.
Akitangaza uadui wa serikali ya Israel dhidi ya maadili ya kibinadamu, alisisitiza: “Kuuunga mkono Msafara wa Sumud ni kuuunga mkono ubinadamu.”
Maoni yako