Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Hawza, matini ya ujumbe wa Ayatullah A‘rafi, Mkuu wa Hawza za Kielimu, kwa mnasaba wa kumbukumbu ya kutolewa kwa ujumbe wa “Hawza Inayoongoza na Bora” ni kama ifuatavyo:
بسم الله الرحمن الرحیم
مِنَ الْمُؤْمِنِینَ رِجَالٌ صَدَقُوا مَا عَاهَدُوا اللَّهَ عَلَیْهِ فَمِنْهُمْ مَنْ قَضَی نَحْبَهُ وَمِنْهُمْ مَنْ یَنْتَظِرُ وَمَا بَدَّلُوا تَبْدِیلًا
Kumbukumbu ya kutolewa kwa ujumbe wa kihistoria wa Imam na Kiongozi Shahidi Ayatullah al-Udhma Khamenei (q.s) kwa kongamano kubwa la kimataifa la miaka mia moja tangu kuanzishwa upya kwa Hawza kongwe na yenye zaidi ya miaka elfu moja ya Qum, wenye anuani ya “Hawza Inayoongoza na Bora”, imewadia, na kwa mara nyingine sauti yenye kutia roho ya ujumbe huo inasikika katika fikra na dhamiri za wanahawza. Lakini kwa huzuni na hali isiyoaminika, kumbukumbu ya tukio hili kubwa la kihawza, kielimu na kimapinduzi imefika katika hali ambayo kiongozi huyo mtukufu hayupo tena miongoni mwetu na amefikia neema kubwa ya shahada. Msiba huu mkubwa umetuingiza sisi sote wana Hawza, Iran nzima na ulimwengu mzima katika huzuni yenye kuunguza moyo na maumivu ya kuachwa na kiongozi huyo mwenye hekima.
Lakini majonzi haya yenye kuunguza moyo na shahada hiyo ya kidhulma, yalizalisha mwamko wa kushangaza na mapinduzi makubwa yaliyoenea Iran, katika ukanda na dunia nzima, na kufuatia hilo mawimbi makubwa yenye kutikisa dunia yalitokea na kuvunja hesabu za kimataifa pamoja na mipango ya kibeberu. Ujumbe wa kihistoria na wa kistaarabu wa “Hawza Inayoongoza na Bora” ni kiini cha fikra za shahidi huyo na kiongozi bora, uliotokana na mlingano wa fikra wa Mapinduzi ya Kiislamu na Imam Khomeini (ra), ni hati ya Hawza za Kielimu, ramani ya mustakabali wa wanahawza na wanazuoni wenye uelewa, mwongozo wa wanafunzi na vijana, na dira ya mabadiliko na mageuzi yajayo ya Hawza.
Ujumbe huu ni mwendelezo wa hati ya uanazuoni ya Imam mtukufu na fikra za Maimamu wawili wa Mapinduzi, pamoja na hotuba na maelekezo mengi ya Imam Shahidi, na sambamba na jumbe na nasaha za Marajii wakubwa wa taqlid (damat barakatuhum) pamoja na taasisi na wakubwa wa Hawza ya Kielimu, uliandika ukurasa mpya katika historia ndefu ya Hawza za Kielimu na Hawza ya Qum yenye kuleta mapinduzi, kujenga mfumo na kustawisha ustaarabu.
Ujumbe huu uliakisi matarajio ya mwanzilishi wa Hawza ya Qum, marehemu Ayatullah al-Udhma Hairi Mehrjerdi Yazdi (r.a), pamoja na watangulizi wakubwa wa Hawza hii, wema waliotangulia na njia yenye nuru ya mashahidi watukufu wa Uislamu, Iran, Mapinduzi ya Kiislamu, Muqawama na uanazuoni. Pia ulionesha njia ya harakati, ukachora vilele, na kufanya jukumu la wanahawza, taasisi na wakubwa wa Hawza, hususan kizazi kipya na madhubuti cha wanafunzi, walimu, watafiti, wabebaji wa tablighi na wasimamizi wa Hawza kuwa kubwa na zito zaidi.
Na sasa mwito wa ujumbe huu na mawimbi ya maelekezo ya mujahid huyo mkubwa na kiongozi mwenye mwamko, yanaendelea kusikika masikioni mwetu. Katika mapambano haya makubwa na makabiliano ya kimstaarabu kati ya Iran na Mapinduzi ya Kiislamu dhidi ya ubeberu wa kishetani na jeshi la kiibilisi, hofu, udhaifu, kulegea, kughafilika na kubaki nyuma ya mabadiliko havikubaliki kwa Hawza inayoongoza na bora. Wanahawza wanapaswa, kwa mwanga wa ujumbe huu na kwa kufuata Wilayat al-Faqih pamoja na Kiongozi Mkuu Ayatullah Sayyid Mujtaba Husayni Khamenei (dam dhilluhu) na Maraji wakubwa (damat barakatuhum), kuchukua hatua kubwa mbele na kutumia mazingira mapya pamoja na fursa mpya kwa ajili ya kujenga ulimwengu unaotegemea dini kamili, maadili na mwelekeo wa kiroho, na kwa mtazamo hai kuelekea kuweka msingi na kustawisha ustaarabu mpya wa Kiislamu.
Wanapaswa pia, kwa kuhamasishwa na mwamko wa wananchi na nafasi ya Hawza na utamaduni katika vita ya tatu, kuwaza mustakabali bora zaidi, kubeba hatari, kupasua dari la anga na kuanzisha mpango mpya.
Kuhusu hati ya uanazuoni na ujumbe wa “Hawza Inayoongoza na Bora”, maudhui mengi ya ufafanuzi na uchambuzi yamezalishwa, na wanazuoni wakubwa wa Hawza na wengine wamezungumza juu yake. Mimi pia kwa mchango wangu mdogo, katika hotuba mbalimbali nimeeleza pande na vipengele tofauti vya ujumbe huu. Na sasa katika kumbukumbu ya kutolewa kwa ujumbe huu na katika mazingira nyeti mno ya historia ya nchi, Mapinduzi ya Kiislamu na Hawza ya Kielimu, ningependa kwa unyenyekevu na kuomba radhi kuwakumbusha walimu waheshimiwa, wasomi wa Hawza na vyuo vikuu, wanafunzi, na watafiti vijana wapendwa mambo machache:
Kwanza: Kiini cha msingi na mhimili mkuu wa mlingano wa fikra wa Maimamu wawili wa Mapinduzi pamoja na wakubwa na viongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu, hususan ujumbe wa juu na mtukufu wa “Hawza Inayoongoza na Bora”, zaidi kuliko mhimili mwingine wowote, ni kutoa tafsiri mpya na yenye mwangaza wa “Hawza ya Kielimu katika ulimwengu wa kisasa”.
Hawza ina historia ndefu, na ndani ya hazina yake yenye thamani kuna urithi na hazina adhimu katika kuzalisha elimu na kuendeleza taaluma mbalimbali, hususan hikma na fiqhi, pamoja na kuwaongoza watu wa Iran na Umma wa Kiislamu katika nyanja za kiroho, kimaadili, kitamaduni, kijamii na kisiasa, na pia katika jihadi, kujitolea na kuwahudumia watu.
Lakini katika zama hizi mpya tunakabiliwa na mabadiliko ya kasi, mageuzi makubwa na mabadiliko katika maarifa na maisha ya kijamii na walimwengu. Maswali na mahitaji yasiyo na mwisho yako mbele yetu. Aidha, tawala za elimu na teknolojia mpya pamoja na nguvu na udhaifu wake mkubwa zimeizunguka dunia yetu. Muhimu zaidi ni kwamba ustaarabu wa kimada umeleta vitisho vingi kwa ubinadamu, ulimwengu wa Kiislamu, utamaduni wa dini na maadili.
Zaidi ya hayo, zama za mwamko wa Kiislamu, kusimama kwa wanyonge duniani na kipindi cha Mapinduzi ya Kiislamu vimefungua kurasa mpya mbele ya Hawza na taasisi ya dini na kuyafanya majukumu yake kuwa mazito zaidi. Hawza katika kiwango kipya na katika tafsiri ya Hawza inayoongoza, bora na ya kimapinduzi, lazima itimize wajibu wake katika uwanja huu uliowekwa mbele yake.
Kwa upande mmoja, lazima ihifadhi utambulisho na uasilia wake wa kihistoria, ishikamane na misingi sahihi ya kielimu na ijtihadi, pamoja na njia za kiroho na kimaadili na mila zake asili, bila kuacha hata chembe moja ya mwenendo wake mashuhuri na msingi wake maarufu. Na kwa upande mwingine, ifungue dirisha la uelewa wake kuelekea ufahamu hai wa mabadiliko, kutoa majibu sahihi kwa mahitaji, kushirikiana kwa hekima na ujasiri na matukio mapya, kufungua upeo kuelekea maisha ya Kiislamu na Kiimani na kuweka msingi wa mtazamo mpya wa kimstaarabu, huku ikitumia roho ya kijihadi, kimapinduzi na ya kuvunja vikwazo.
Huu ndio mtazamo na mlingano wa fikra ambao Imam mkubwa Khomeini (r.a), Kiongozi Shahidi mtukufu (r.a), na wanafikra wakubwa wa Hawza za Kielimu waliuweka msingi wake, na ukapelekea harakati, mapinduzi, mfumo wa Kiislamu, Muqawama wa Kiislamu na mageuzi makubwa katika ulimwengu wa kisasa. Kudumisha mtazamo huu na kujitahidi kuistawisha Hawza katika upeo huu ndiyo roho ya ujumbe huu na mwito wake wa kimbinguni, na lazima ufuatiliwe kwa jihadi ya kielimu na kivitendo. Sote katika ngazi zote tuna wajibu katika uwanja huu.
Pili: Msingi wa Hawza inayoongoza na bora umejengwa juu ya kutumia akili, kuzalisha fikra na kuumba elimu katika nyanja ya fiqhi na maarifa ya Kiislamu kwa msingi wa Qur’ani Tukufu na Sunna ya Mtume Mkuu (s.a.w.w) pamoja na Ahlul-Bayt wake watoharifu (a.s). Lakini uwekezaji huu wa kielimu, pamoja na kuwa na uasilia na uimara katika vyanzo, misingi na mbinu zake, unahitaji pia utambuzi wa mada, kupima mahitaji, undani wa kielimu, umakini wa kifkra na uelewa mpana wa mabadiliko, maswali na changamoto za zama hizi mpya, pamoja na kuzingatia kwa kina mahitaji ya mfumo wa Kiislamu, Mapinduzi ya Kiislamu, hali ya Umma wa Kiislamu na jamii ya kimataifa.
Msisitizo wa ujumbe huu juu ya umuhimu wa kujenga mifumo ya kidini katika nyanja mbalimbali, kuimarisha mijadala mipya na ya kisasa, kuzingatia elimu zote za Kiislamu na kihawza, kujiepusha na kupoteza fursa, na kupanga vizuri mifumo ya kihawza unatokana na mhimili huu. Jambo hili linahitaji mageuzi katika mitazamo katika ngazi zote za kihawza.
Kwa rehema za Mwenyezi Mungu, chini ya uangalizi wa Mara'jii na wakubwa wa Hawza, Baraza Kuu na taasisi za juu pamoja na taasisi za kihawza katika sehemu za ndani na za kimataifa, kwa upande wa ndugu na dada, na katika nyanja za kielimu, kitamaduni na tablighi kote nchini, chimbuko la mwelekeo huu limeanza kuonekana. Hususan katika miaka ya karibuni, kwa mwanga wa matakwa ya Maimamu wawili wa Mapinduzi na matakwa ya zaidi ya miongo mitatu ya uongozi wa Kiongozi Shahidi (r.a), miradi na hatua nyingi zimeandaliwa na kutekelezwa. Inshaallah Makao ya Ujumbe wa “Hawza Inayoongoza na Bora” yatatoa ripoti zake.
Kwa hivyo, sote tunapaswa kukubali mapungufu yetu, kuomba radhi kwa uzembe na upungufu wetu, na katika kumbukumbu ya ujumbe huu sisi sote, taasisi zote, wasimamizi, shakhsia na mikondo ya kihawza tujifanyie tathmini upya na kuongeza juhudi. Sehemu ya hayo inaweza kurekebishwa na kukamilishwa katika mpango wa pili wa miaka mitano. Jukumu hili muhimu si la taasisi rasmi pekee, bali pia ni la mwili wa Hawza, tabaka za kati, wanafunzi na vijana bora, jumuiya huru na taasisi mbalimbali za kihawza, ambao wanaweza kuwa mbele na viaongozi.
Tatu: Yote yaliyotajwa hayapaswi kutufanya sisi wanahawza na wanazuoni tusahau jukumu muhimu la kuwa karibu na wananchi, kuwapa nafasi vijana, kuwa mstari wa mbele, kushikamana na maadili na namna ya kutekeleza majukumu haya, pamoja na kushirikiana na wasomi wa vyuo vikuu, taasisi za vyuo, wanafunzi na walimu wenye mwamko na wanaotafuta haki, na pia mahusiano ya kimataifa. Mihimili hii muhimu imejitokeza katika sehemu mbalimbali za ujumbe huu na inapaswa kupewa umuhimu, kupangiwa mipango na kufanyiwa juhudi zaidi.
Nne: Na sasa sisi tupo pamoja na barabara, medani na mwamko mkubwa wa taifa la Iran, mhimili wa Muqawama, Umma wa Kiislamu na mapinduzi ya kimungu katika vita ya tatu na hatua mpya ya historia ya Iran, eneo na dunia. Kwa fadhila za Mwenyezi Mungu, wanafunzi vijana, wabebaji wa tablighi wenye heshima, wanazuoni wenye mwamko, taasisi za juu za Hawza, misafara mikubwa ya kihawza, makao ya ufikishaji ulio bayana “بلاغ مبین” ya Hawza za Kielimu pamoja na taasisi zake zimecheza nafasi ya kusifiwa.
Nafasi hii lazima iendelee hadi ushindi dhidi ya adui na kuishinda adui mdanganyifu na mkatili, na pia iendelee hata baada ya vita. Viongozi wa mihimili mitatu ya dola, wananchi waheshimiwa, vijana wapendwa, Hawza za Kielimu, taasisi za kihawza, vyuo vikuu, taasisi za kitamaduni na Basij wana majukumu mazito mbele yao na wanapaswa kujiandaa kwa ajili yake.
Wanahawza kwa ujumla, na vijana wapendwa wa Hawza na jamii hususan, wanapaswa kujiandaa kwa mustakabali nyeti na nafasi maalumu za kutekeleza wajibu. Kwa fadhila za Mwenyezi Mungu, mustakabali wa Iran na dunia utakuwa wa Uislamu na Mapinduzi ya Kiislamu.
Tano: Tablighi, ufafanuzi, jihadi ya kuelimisha, kupanga na kuinua mfumo wa tablighi, uenezaji na usambazaji wa fikra za kidini, ni wasia wa daima wa Imam Shahidi (r.a), ujumbe wa “Hawza Inayoongoza na Bora”, na pia hotuba yao ya kihistoria mbele ya wabebaji wa tablighi tarehe 21 Tir mwaka 1403. Licha ya mageuzi makubwa yaliyotokea katika miaka hii, wafuasi wa Hawza na taasisi zake wanapaswa kuendelea kufuatilia jambo hili na kutoa ripoti. Hata hivyo bado tupo mwanzoni mwa njia ya mageuzi haya, na kunahitajika juhudi kubwa zaidi pamoja na ushirikiano mpana zaidi wa wote.
Namuomba Mwenyezi Mungu Mtukufu afya na mafanikio kwa wanahawza wote na wanazuoni waheshimiwa, pamoja na ushindi wa mwisho wa Waislamu, wanyonge wa dunia, vikosi vya ulinzi na mhimili wa Muqawama dhidi ya maadui na mabeberu wa dunia.
Alireza A‘rafi
Mkuu wa Hawza za Kielimu
Maoni yako