Kwa mujibu wa kitengo cha kimataifa cha Shirika la Habari la Hawza, Ofisi ya Mwendesha Mashtaka Mkuu wa Istanbul imetangaza kwamba kufuatia shambulio la jeshi la Israel dhidi ya msafara wa kimataifa wa “Sumud” katika maji ya kimataifa, imeanza moja kwa moja uchunguzi wa kisheria.
Katika taarifa iliyotolewa na Ofisi ya Mwendesha Mashtaka wa Istanbul imeelezwa kuwa:
“Baada ya shambulio lililofanywa na vikosi vya majini vya Israel katika maji ya kimataifa dhidi ya msafara wa kimataifa wa Sumud—uliokuwa ukielekea kupeleka misaada ya kibinadamu kwenda Ghaza—na kusababisha kutiwa mbaroni kwa raia wa nchi yetu, kwa mujibu wa kanuni za Mkataba wa Sheria za Bahari wa Umoja wa Mataifa, kifungu cha 15 cha Sheria ya Mwenendo wa Mashauri ya Jinai namba 5271 na vifungu vya 12 na 13 vya Sheria ya Adhabu ya Uturuki namba 5237, Ofisi ya Mwendesha Mashtaka Mkuu imeanza moja kwa moja na ndani ya mfumo wa jalada lililopo, uchunguzi kuhusu makosa ya ‘kunyimwa uhuru’, ‘utekaji na kuzuiliwa vyombo vya usafiri’, ‘wizi uliokithiri’, ‘uharibifu wa mali’ na ‘unyanyasaji’.”
Hapo awali, maafisa wa msafara wa kimataifa wa “Sumud” nchini Uturuki walikuwa wametangaza kwamba jeshi la Israel katika umbali wa zaidi ya maili 600 kutoka Ghaza na katika maji ya kimataifa karibu na maji ya mipaka ya Ugiriki, lililenga msafara huo na kuwakamata raia 20 wa Uturuki waliokuwamo ndani yake.
Maoni yako