Kwa mujibu wa Idara ya Kimataifa ya Shirika la Habari la Hawza, mmoja wa wazungumzaji wa kikao maalumu cha “Mustakbali wa Mapambano” kilicholenga “nafasi ya Umma wa Kiislamu katika kuvunja tawala ya Marekani” na kurushwa siku ya Jumapili kupitia Televisheni ya Al-Kawthar, alikuwa Sheikh Abdeljalil al-Salem, aliyekuwa mkuu wa Chuo Kikuu cha Zaytouna na Waziri wa Mambo ya Dini wa Tunisia.
Mwanzoni mwa hotuba yake, alionesha furaha yake kwa kushiriki katika kikao hicho, na akaelezea mada yake iliyoitwa “Iran na mhimili wa Muqawama katika mizania ya mzozo wa kikanda”, akisema: Nafasi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na mhimili wa Muqawama unaojumuisha Lebanon, Iraq na Yemen, katika miaka ya hivi karibuni imekuwa na mabadiliko muhimu ya kihistoria, kisiasa na kijeshi katika eneo hili.
Sheikh Abdeljalil al-Salem aliongeza kuwa: Mabadiliko haya kwa vitendo yamesababisha kudhoofika na kupungua kwa ushawishi na dola ya Marekani katika kiwango cha kikanda, na yako katika mchakato wa kuunda mizania mpya katika mfumo wa kimataifa.
Mwanazuoni huyo wa Tunisia, huku akirejea mabadiliko ya mizania ya nguvu ya kikanda, alisisitiza kuwa: Katika siku zijazo tutashuhudia kuibuka kwa Iran kama nguvu yenye athari katika eneo la Mashariki ya Kati na Ghuba ya Uarabuni; nguvu ambayo inaweza kuwa na nafasi muhimu katika kuamua mizania na sera za kikanda.
Aidha, huku akirejea athari za kimataifa za mabadiliko haya, alisema: Mwelekeo huu unaweza kuweka msingi wa kuibuka kwa mfumo mpya wa dunia unaojengwa juu ya uadilifu, heshima ya utu wa binadamu na uhuru wa mataifa, na ambao unapingana na mfumo wa zamani uliowekwa na nguvu za Magharibi.
Aliendelea kusema: Katika muktadha huu, ushirikiano kati ya Iran, China na Urusi unaweza kuwa miongoni mwa mihimili mikuu ya mfumo huu mpya wa dunia, na unaweza kusababisha mabadiliko katika muundo wa nguvu wa mfumo wa kimataifa.
Mkuu huyo wa zamani wa Chuo Kikuu cha Zaytouna alisisitiza kwamba: Mabadiliko ya hivi karibuni si tu yanaonesha mageuzi ya kisiasa na kijeshi, bali pia yanaweza kuwa msingi wa kuibuka kwa ustaarabu mpya wa kibinadamu unaojengwa juu ya thamani kama uadilifu, ubinadamu na mazungumzo ya ustaarabu; ustaarabu unaosimama dhidi ya ustaarabu wa mabavu ambao umeonesha sura yake halisi katika matukio ya eneo hili.
Mwisho, aliwashukuru waandaaji wa kikao hicho na kusema: Mabadiliko haya yameelekeza fikra za umma duniani kuelekea kutathmini upya simulizi zilizotawala na kuelewa ukweli mpya.
Maoni yako