Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Hawza, Ayatollah Jawadi Amoli katika Tafsiri ya Qur’ani, juzuu ya 17, ukurasa wa 241, katika mjadala wa “Jamii katika Qur’ani” amebainisha kuwa: Katika aya nyingi za Qur’ani, Mwenyezi Mungu anakosoa vikali tabia ya jamii ya wanafiki na anawazuia waumini wasiwafanye marafiki:
﴿ومِنَ النّاسِ مَن یَقولُ آمَنّا بِاللهِ وبِالیَومِ الآخِرِ وما هُم بِمُؤمِنین﴾.
“Miongoni mwa watu wako ambao husema: Tumemuamini Mwenyezi Mungu na Siku ya Mwisho, ilhali wao si waumini.”
Marji' huyu aliendelea kufafanua baadhi ya sifa za wanafiki na akasema: Wanafiki humuadaa Mwenyezi Mungu na waumini:
﴿یُخَادِعُونَ اللهَ والَّذینَ آمَنُوا وما یَخدَعونَ إلاّ أنفُسَهُم وما یَشعُرون﴾
“Wanamhadaa Mwenyezi Mungu na wale walioamini, lakini hawamdanganyi yeyote isipokuwa nafsi zao, wala hawatambui.”
Wanafiki huwafanya marafiki makafiri badala ya Waislamu:
﴿ألَّذینَ یَتَّخِذونَ الْکافِرِینَ أولِیاءَ مِن دونِ المُؤمِنین﴾
“Wale wanaowafanya makafiri kuwa marafiki badala ya waumini.”
Mtukufu huyo aliweka bayana kuwa: Kwa sababu hii Mwenyezi Mungu atawakusanya wanafiki pamoja na makafiri katika moto wa Jahannam:
﴿إنَّ اللهَ جامِعُ المُنَافِقِینَ وَالْکافِرِینَ فی جَهَنَّمَ جَمیعا﴾
“Hakika Mwenyezi Mungu atawakusanya wanafiki na makafiri pamoja katika moto wa Jahannam.”
Kwa mujibu wa maelezo yake, mkusanyiko huu wa kwenye Jahannam si wa kudumu wala hauoneshi kuwa wako katika kiwango sawa, kwa sababu daraja za moto kwa wanafiki ni za chini zaidi kuliko za makafiri:
﴿إنَّ المُنَافِقِینَ فِی الدَّرکِ الاسفَلِ مِنَ النّار﴾.
“Hakika wanafiki watakuwa katika tabaka la chini kabisa Motoni.”
Amesisitiza kuwa usaliti mbaya zaidi katika vita vya Mtume (rehema na amani zimshukie yeye na AhluBayt wake) huko Madina ulihusiana na wao:
﴿وإذَا جاءَهُم أمر مِنَ الأمنِ أوِ الخَوفِ أذاعوا بِه﴾
“Na linapo wafikia jambo lolote lilio khusu amani au la kitisho wao hulitangaza.”
Ayatollah Jawadi Amoli amesema: Kwa sababu hii, Mwenyezi Mungu alimwamuru Mtume wake kupigana “jihad maalum” dhidi yao:
﴿یا أیُّهَا النَّبِی جَاهِدِ الکُفّارَ والمُنَافِقِینَ واغلُظ عَلَیهِم﴾
“Ewe Nabii! Pambana na makafiri na wanafiki, na uwe mkali dhidi yao.”
Maoni yako