Kwa mujibu wa ripoti ya Kitengo cha tarjama cha Shirika la Habari la Hawza, Ataba Tukufu ya Husseini katika Mwezi Mtukufu wa Ramadhani inaendelea kutoa huduma zake za kibinadamu kwa mazuwari, na kila siku husambaza zaidi ya milo 4,000 ya futari bila malipo kupitia Idara ya Nyumba ya Wageni ya Imam Hussein (amani iwe juu yake).
Adnan Al-Naqib, mkuu wa idara hiyo, alisema: Idara ya Nyumba ya Wageni ya Haram Tukufu ya Imam Hussein (amani iwe juu yake), iliyo chini ya Ataba Tukufu ya Husseini, sambamba na siku za Mwezi Mtukufu wa Ramadhani, husambaza kila siku zaidi ya milo elfu nne ya futari bila malipo miongoni mwa mazuwari.
Alifafanua: Hatua hii inatekelezwa katika muktadha wa juhudi za Ataba Tukufu ya Husseini katika kuwahudumia mazuwari wa Husayn ibn Ali, hususan katika siku za mwezi huu wenye baraka, ambapo Haram ya Bwana wa Mashahidi (amani iwe juu yake) hushuhudia uwepo mkubwa wa mazuwari kutoka ndani na nje ya Iraq.
Al-Naqib aliongeza: Wafanyakazi wa Nyumba ya Wageni ya Husseini wanafanya juhudi kubwa katika kuandaa na kusambaza milo ya futari kila siku, kwa kuzingatia viwango vya juu kabisa vya ubora na nidhamu, ili iwe kwa hadhi ya utakatifu wa mahali hapa na huduma kwa mazuwari.
Inafaa kutajwa kwamba, Ataba Tukufu ya Husseini katika kipindi chote cha Mwezi wa Ramadhani inaendelea kutoa huduma zake kwa mazuwari, na daima inasisitiza roho ya ukarimu na rehema ili kuhuisha kila siku ujumbe wake wa kibinadamu.
Maoni yako