Jumamosi 21 Februari 2026 - 13:18
Haki ya kijamii inategemea haki ya kiuchumi

Hawza/ Hujjatul-Islam Sayyid Sajid Ali Naqvi amesisitiza katika ujumbe wake kwamba; kwa kuendelea kutawala mifumo dhalimu ya kiuchumi na kisiasa, haiwezekani kufanikisha haki ya kijamii. Ameongeza kuwa, Umoja wa Mataifa unapaswa kuwasilisha mifumo ya vitendo kwa ajili ya kuimarisha haki ya kiuchumi.

Kwa mujibu wa ripoti ya Kitengo cha tarjama cha Shirika la Habari la Hawza, Hujjatul-Islam Sayyid Sajid Ali Naqvi, Rais wa Baraza la Wanazuoni wa Kishia nchini Pakistan, katika ujumbe wake wa tarehe 20 Februari (Siku ya Kimataifa ya Haki ya Kijamii), alisisitiza uhusiano wa kina uliopo kati ya haki ya kijamii na haki ya kiuchumi, kwa kusema:

Haiwezekani kufanikisha haki ya kijamii bila kuwepo haki ya kiuchumi. Mfumo wa kiuchumi na kisiasa unaotawala dunia umechukua sura ya wazi ya udhalimu, na hali hii imesababisha malengo ambayo Umoja wa Mataifa husisitiza katika Siku ya Kimataifa ya Haki ya Kijamii kuendelea kuwa magumu kufikiwa.

Ukosoaji wa miundo ya kimataifa isiyo ya haki

Aliendelea kusema kuwa; mfano wa wazi wa mfumo huu usio wa haki unaonekana katika sera za kiutawala na lugha za kibabe za baadhi ya mataifa yenye nguvu. Alitaja matukio machungu huko ukanda wa Ghaza, Ukingo wa Magharibi, Khan Younis, pamoja na maendeleo ya hali katika Syria na Lebanon kuwa ni mifano ya wazi ya matokeo ya mfumo huo; mfumo unaozuia kupatikana kwa amani ya kudumu na haki ya kweli duniani.

Kukumbusha wajibu wa kimataifa

Rais huyo wa Baraza la Wanazuoni wa Kishia Pakistan alikumbusha mpango wa mwaka 2009 wa Umoja wa Mataifa uliopewa jina la “Mpango wa Kutoa Kiwango cha Chini cha Ulinzi wa Kijamii,” ambao ulikuwa na lengo la kuhakikisha kiwango cha chini cha ulinzi wa kijamii kwa watu wote duniani, ukisisitiza misingi kama haki, usawa, kuheshimu utofauti, upatikanaji wa huduma za kijamii, na utekelezaji wa haki za binadamu katika nyanja zote za maisha.

Alihoji kuwa; katika kipindi cha muongo mmoja tu uliopita, ni aina gani ya dhuluma na shinikizo zilizo lazimishwa na mataifa, mifumo ya kisiasa na kiuchumi ya kibabe, huku jamii ya kimataifa ikiwa imeshindwa kuzuia hali hiyo?

Akielezea migogoro kama ile ya Iraq, Afghanistan, Rohingya, Sudan, na hasa matukio ya hivi karibuni katika Ukanda wa Ghaza, Ukingo wa Magharibi, Bayt al-Maqdis inayokaliwa kwa mabavu, Lebanon na Syria, alisisitiza: Katika mazingira kama haya, inawezekanaje kuzungumzia utekelezaji wa haki ya kijamii, ilhali haki za msingi kabisa za binadamu — zikiwemo usalama wa maisha, afya, elimu, ajira yenye heshima, kulinda utamaduni na mila, uhuru wa kidini na kijamii, na uhuru wa kujieleza — bado viko hatarini?

Umuhimu wa kurekebisha mifumo ya kiuchumi ya kimataifa

Mwisho, alisisitiza kuwa; ikiwa Umoja wa Mataifa unataka kurejesha mamlaka na nafasi yake yenye athari katika uwanja wa kimataifa, lazima kwanza uwasilishe na kuimarisha mifumo ya haki ya kiuchumi kwa ajili ya kufanikisha haki ya kijamii, na kusimama dhidi ya malengo ya kiutawala ya mataifa makubwa.

Alisema kuwa; ni kwa kuweka vizuizi madhubuti dhidi ya tamaa za kisiasa na kiuchumi, na kwa kuunga mkono nguvu zinazojali hifadhi ya uhai na hadhi ya binadamu, ndipo tunaweza kuwa na matumaini ya kufanikisha ndoto ya haki na usawa wa kijamii kwenye ngazi ya kimataifa.

Lebo

Maoni yako

You are replying to: .
captcha