Kwa mujibu wa kitengo cha tarjama cha Shirika la Habari la Hawza, Hazem Qassem, msemaji wa Hamas, siku ya Jumamosi akijibu kuhusu muendelezo wa uhalifu unaofanywa na utawala wa Kizayuni huko Ghaza alisema: Dai la adui wa Kizayuni kwamba mashambulizi na mauaji hayo ni “jibu” kwa madai ya ukiukaji wa sitisho la mapigano na Hamas, si chochote ila ni kisingizio cha uongo na kilichoshindikana cha kuhalalisha uhalifu wa kutisha na usio wa kibinadamu dhidi ya raia.
Kituo cha habari cha Al-Masirah kilimnukuu akisema: Madai haya yasiyo na msingi yanaonesha wazi dharau ya utawala wa kikoloni kwa juhudi za upatanishi za nchi zilizodhamini makubaliano, pamoja na pande zote zilizoshiriki katika kile kinachoitwa “Baraza la Amani”.
Msemaji wa Hamas aliiita jumuiya ya kimataifa, Umoja wa Mataifa na mashirika ya haki za binadamu, akisisitiza kuwa: ni lazima uhalifu huu ulaaniwe waziwazi na hatua za haraka na za vitendo zichukuliwe ili kuusitisha.
Pia alitoa wito wa kuwafikisha mahakamani viongozi wa utawala wa kikoloni kwa sababu ya kutenda uhalifu wa kivita, na kuzuia kuendelea kwa sera ya kuzalisha mauaji kwa ajili ya vita—sera inayomchochea adui kuendelea na mauaji na uharibifu zaidi.
Kauli hizi zilitolewa wakati ambapo vyanzo vya Kipalestina viliripoti kuuawa kishahidi takriban watu 15 kufuatia shambulio la utawala wa Kizayuni dhidi ya kituo cha polisi cha eneo la Sheikh Radhwan, kaskazini mwa mji wa Ghaza.
Mashahidi walio ona walisema: kituo hicho kililengwa moja kwa moja na shambulio la kikatili wakati ambao raia walikuwepo katika kiwango cha juu, na kivitendo hakukuwa na dalili yoyote ya utiifu wa utawala wa Kizayuni kwa makubaliano ya sitisho la mapigano huko Ghaza.
Katika muktadha huo huo, Haitham Abu al-Ghazlan, mmoja wa viongozi wa Harakati ya Jihad ya Kiislamu ya Palestina, alisisitiza kuwa; mauaji haya yanaonesha nia ya kweli ya utawala wa Kizayuni ya kurejea tena katika mauaji na kukiuka rasmi makubaliano ya sitisho la mapigano.
Aliongeza kuwa: kuongezeka kwa mashambulizi ya utawala huo kunaonesha wazi kwamba utawala wa kikoloni hauheshimu makubaliano yoyote na unajaribu kulazimisha hali halisi mpya katika ngazi za kijiografia na kisiasa kwa manufaa yake wenyewe.
Katika hitimisho, alisisitiza kuwa: kuendelea kwa uchokozi huu kunaweka jukumu kubwa juu ya mabega ya wapatanishi na wadhamini wa makubaliano ya sitisho la mapigano, hasa Marekani na Donald Trump, kwani wao ndio wanaopaswa kuulazimisha utawala wa Kizayuni kutekeleza kikamilifu makubaliano hayo.
Chanzo: Ava Press
Maoni yako