Kwa mujibu wa ripoti ya Shirika la Habari la Hawza, katika kumbukumbu ya siku za Fatimiyya, hapa kuna nukuu ya maneno ya marehemu Ayatollah Misbah Yazdi kuhusiana na Khutba ya Fadakiyya ya Bibi Zahra (a.s):
Lengo na dhamira ya Bibi Fatima Zahra (a.s) katika maneno yake, kwa bahati mbaya, havikueleweka ipasavyo hata mbee ya baadhi ya marafiki wa karibu na wafuasi wake.
Madhumuni yake katika kuitoa khutba hiyo yalikuwa ni yale yale aliyokuwa nayo Mtume Mtukufu (s.a.w.w) alipokuwa akifikisha ujumbe wa Mwenyezi Mungu: kuwalingania watu kwenye uongofu, kuwaokoa na upotovu na kuwaelekeza kwenye wokovu wa kweli.
Kama ambavyo Mtume (s.a.w.w) alihisi uchungu wa ndani kwa kuona watu wakipotea na kushindwa kuifikia furaha ya kweli — akiteseka kwa sababu walikuwa wanakanyaga njia ya batili, njia inayowaongoza kwenye adhabu ya milele — ndivyo hivyo Bibi Zahra (a.s) alivyoshiriki hisia hizo na dhamira hiyo hiyo.
Ndiyo maana aliianza hotuba yake kwa kukumbushia sifa za Mtume (s.a.w.w) na kusema kwa maneno yenye nguvu:
"Mimi ni binti wa Mtume yule yule."
Kwa kauli hii, alitaka kuweka wazi kuwa yale anayoyasema si kwa misingi ya hasira au maslahi binafsi, bali ni kwa sababu ya huruma, upendo na wasiwasi wa kweli kwa watu.
Madhumuni yake yalikuwa ni kuwaokoa watu wasipotee, kuwasaidia wapate mwanga wa haki na hatimaye wafikie furaha ya dunia na akhera.
Kwa hiyo, mwanzoni mwa hotuba yake, Bibi Fatima Zahra (a.s) alisoma aya tukufu ya Qur’ani inayomzungumzia Mtume (s.a.w.w):
«لَقَدْ جَاءَكُمْ رَسُولٌ مِّنْ أَنفُسِكُمْ عَزِيزٌ عَلَيْهِ مَا عَنِتُّمْ حَرِيصٌ عَلَيْكُمْ بِالْمُؤْمِنِينَ رَؤُوفٌ رَّحِيمٌ»
“Hakika amekwisha kujieni Mtume kutokana na nyinyi wenyewe; yanamhuzunisha yanayo kutaabisheni; anakuhangaikieni sana. Kwa Waumini ni mpole na mwenye huruma.
” (At-Tawba: 128)
Kwa kuisoma aya hii, Bibi Zahra (a.s) alibainisha wazi chanzo cha maneno yake — kwamba roho ileile ya huruma na upendo ya Mtume ipo ndani yake. Hotuba yake haikuwa malalamiko ya kisiasa au madai ya mali, bali ulikuwa wito wa kimantiki na kiroho wa kuwarejesha watu kwenye njia ya haki na kuwaokoa na upotovu. Lengo lake kuu lilikuwa kuuongoza umma, uamsho wa kiakili na kimaadili, na kuwaongoza watu kwenye wokovu wa kweli duniani na akhera.
            
                
Maoni yako