Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Hawza, mkutano huo unatarajiwa kufanyika kuanzia tarehe 13 hadi 15 mwezi Aban mwaka 1404 Hijria Shamsia (sawa na tarehe 4 hadi 6 Novemba 2025) ukiwahusisha mamia ya marabi wa Kiyahudi kutoka barani Ulaya, katika mji mkuu wa Jamhuri ya Azerbaijan. Kwa mujibu wa taarifa, mada kuu zitakazojadiliwa ni pamoja na “Mikataba ya Ibrahim” na mikakati ya kukabiliana na harakati za kupinga Uzayuni.
Doğu Perinçek, katika barua yake hiyo, akilaani kufanyika kwa tukio kama hilo katika nchi ya Kiislamu ya Azerbaijan, aliandika: “Kufanyika kwa mkutano wa aina hii hakuna mfano wake katika nchi yoyote nyingine ya Kiislamu au ya Kituruki. Hatua hii inaweza kuongeza vitisho dhidi ya nchi za eneo hili na majirani katika Asia ya Magharibi, na kudhoofisha umoja wa mhimili wa ubinadamu, ulimwengu wa Kituruki na Uislamu.”
Aliendelea kumhutubia Ilham Aliyev kwa kusema: “Jamhuri ya Azerbaijan, chini ya uongozi wako wenye uzoefu, haiwezi kuwekwa katika safu ya Marekani na Israel. Kufanyika kwa mkutano huu kutakuwa ni doa katika historia.”
Kiongozi huyo wa Chama cha Watwan cha Uturuki, mwishoni mwa barua yake, alimwomba Rais wa Azerbaijan aichukue hatua ya kufuta mkutano huo kwa kuzingatia uhuru, usalama na mustakabali wa nchi za eneo hilo, na kuizuia Jamhuri ya Azerbaijan isiingie katika mkondo wa siasa za Magharibi.
Kuchapishwa kwa barua hiyo katika vyombo vya habari vya Uturuki na nchi nyingine za Kiislamu kumezua mwitikio mpana, na kumekuwa miongoni mwa mada kuu zinazojadiliwa katika duru za kisiasa na vyombo vya habari vya Uturuki.
Maoni yako