Jumamosi 25 Oktoba 2025 - 23:38
Wajibu wa kuisaidia Palestina ni zaidi ya itikadi na siasa

Hawza/ Kwa juhudi za mtandao wa “SNN”, kongamano la kimataifa liitwalo "Mwito wa Palestina" limefanyika kwa njia ya mtandao (Zoom) kutoka mji wa Lucknow, India, kwa ushiriki wa kundi la wanazuoni wakuu na wasomi wa dini kutoka nchi mbalimbali duniani.

Kwa mujibu wa kitengo cha tarjama chaShirika la Habari la Hawza, kongamano hili lilifanyika kwa njia ya mtandao likiongozwa na mtandao wa “SNN” kutoka mji wa Lucknow. Katika kikao hicho, wanazuoni mashuhuri na wasomi wa dini kutoka nchi tofauti walitoa mitazamo yao kuhusu uhalifu wa utawala wa Kizayuni na mateso ya taifa la Palestina lililodhulumiwa.

Kuwasaidia wanyonge ni jukumu la Kimungu na Kibinadamu

Katika kikao hicho, Hujjatul-Islam Sayyid Mahbūb Mahdi ‘Ābedi Najafi, kutoka mji wa Chicago nchini Marekani, akirejea mwenendo wa Imam Ali (a.s), alisema: “Bwana wa wachamungu, Ali bin Abi Talib (a.s), katika wasia wake mtukufu, baada ya kusisitiza juu ya kumcha Mwenyezi Mungu, alihimiza sana kuwasaidia waliodhulumiwa. Katika wosia huo hakuweka mipaka ya kimadhehebu, kikabila wala kisiasa. Hii inaonesha kuwa kuwatetea wanyonge si jukumu la kisiasa pekee, bali ni wajibu wa Kimungu na Kibinadamu ambao Mwenyezi Mungu ameliweka juu ya mabega ya waja Wake.”

Akaongeza: “Kama tunavyosimama leo dhidi ya dhulma na jinai za utawala wa Kizayuni dhidi ya watu wasio na hatia wa Palestina, vivyo hivyo hapo awali tulisimama dhidi ya mfalme dhalimu wa Iran, ambaye ingawa kwa jina alikuwa Shia, lakini kwa vitendo alikuwa mnyanyasaji na mwenye mabavu. Kigezo cha kweli ni uadilifu na kusimama dhidi ya dhulma.”

Uislamu ni Dini kamilifu na yenye amani

Kisha, Hujjatul-Islam Sayyid Hamidul-Hasan Taqawi, mwenyekiti wa kongamano na mkuu wa Chuo Kikuu cha Nizāmiyya cha Lucknow, alisema:
“Uislamu ni dini kamili inayomzingatia binadamu, ambayo inawalingania wafuasi wake katika upendo, huruma na kuishi kwa amani na wafuasi wa dini zote. Katika mtazamo wa Uislamu, ubinadamu unatangulia mipaka ya dini na madhehebu, na dhulma katika aina yoyote ile ni jambo linalokataliwa.”

Akiashiria uhalifu unaofanywa na utawala wa Kizayuni, alisema: “Tayari kwa miaka mingi, taifa la Palestina limekuwa likiteseka chini ya wavamizi. Leo hii kuliko wakati mwingine wowote, linahitaji uungwaji mkono na mshikamano wa mataifa huru duniani. Tunatangaza wazi kwamba tuko upande wa watu wanyonge wa Palestina na tunaomba kwa dhati kwa ajili ya uhuru na wokovu wao kutoka kwenye makucha ya dhulma.”

Kufafanua maana ya Qur’ani na sura halisi ya Uislamu

Katika sehemu ya mwisho ya hotuba yake, Sayyid Hamidul-Hasan Taqawi alielezea baadhi ya dhana za Qur’ani Tukufu, akibainisha: “Kwa bahati mbaya, baadhi ya watu wamepotosha maana ya maneno kama ‘kufr’ na ‘kāfir’, na hivyo kutoa taswira ya ukatili na isiyo sahihi kuhusu Uislamu. Hali halisi ni kwamba Qur’ani imetumia maneno hayo kwa wale waliomdhuru au waliopigana na Mtume wa Uislamu (s.a.w.w).”

Akaendelea kusema: “Historia inashuhudia kuwa kipindi chote Mtume Mtukufu (s.a.w.w) alipokuwa Makka, hakuna vita hata moja vilivyoanzishwa na Waislamu; na vita vyote vya Madina vilikuwa vya kujilinda. Uislamu ni dini ya amani, upendo na haki — si dini ya vita na vurugu.”

Hakuna dhalimu aliyedumu katika historia

Dānish Nabil Qāsimī, mmoja wa wanazuoni wa Kisunni na Qari wa kimataifa wa Qur’ani Tukufu, akilihutubia jeshi la Kizayuni, alisema: “Mnyanyasaji anapaswa kujua kwamba muda wa dhulma ni mfupi; hakuna dhalimu aliyedumu katika historia, na hatimaye wote wamepata malipo ya matendo yao. Hii ni ahadi ya Mwenyezi Mungu kwamba dhulma haiwezi kudumu milele.”

Akaongeza kusema: “Katika mazingira haya nyeti, umoja kati ya Shia na Sunni si tu jukumu la kidini, bali ni haja muhimu kwa ajili ya kulinda heshima na hadhi ya Umma wa Kiislamu. Leo maadui wa Uislamu wananufaika na mgawanyiko wetu, ilhali Qur’ani inatuita kwenye udugu, upendo na ushirikiano katika kukabiliana na dhulma.”

Kuitetea Palestina ni kuitetea dhamiri na ubinadamu

Baadaye, Hujjatul-Islam Sayyid Haidar Hasan Āl-Najm al-Millat, kutoka mji wa Lucknow, alisema: “Uhalifu unaofanyika huko Gaza umeumiza dhamiri ya ubinadamu. Maelfu ya wanawake, wanaume na watoto wasio na hatia wameuawa kutokana na mashambulizi ya kinyama ya adui. Hata njia za kutoa misaada zimezuiwa, ili watu wa Palestina wafe kwa njaa na kiu. Matendo haya si tu kinyume cha ubinadamu, bali ni doa jeusi katika historia ya sasa.”

Akaongeza: “Tunalaani kwa nguvu zote dhulma hii ya kikatili, na tunatoa mwito kwa mataifa yote huru duniani kutonyamaza mbele ya uovu huu. Leo, kuutetea Palestina ni kuutetea dhamiri na ubinadamu.”

Kufichua njama za kisiasa chini ya jina la ‘kusitisha mapigano

Hatimaye, Hujjatul-Islam Sayyid Aslam Rizvī, mhubiri kutoka India, akirejea katika mkutano uliofanyika mjini Sharm al-Sheikh, Misri, chini ya uenyekiti wa Rais Abdel Fattah al-Sisi, alisema:
“Tukio hilo lilikuwa njama kubwa dhidi ya watu wanyonge wa Palestina. Kwa jina la ‘kusitisha mapigano’, moja ya ulaghai mkubwa zaidi wa kisiasa katika historia umefanyika.”

Lengo la hatua hii lilikuwa kuzima wimbi la upinzani wa kimataifa dhidi ya Israel

Kiongozi huyo alisema: “Madhumuni ya hatua hiyo yalikuwa kuzima wimbi la maandamano na upinzani wa kimataifa dhidi ya Israel. Watu duniani walidhani kuwa amani imepatikana na hivyo hakuna tena haja ya kuendelea na maandamano; lakini kwa hakika, uhalifu uleule uliendelea kwa ukali na ukatili zaidi.”

Akaongeza kwa kusema: “Amani ya kusitisha mapigano ambayo imejengwa juu ya udanganyifu na usaliti, si amani ya kweli, bali ni mazingira yanayowezesha kuendelea kwa dhulma. Historia ya binadamu itaiandika ‘amkataba huu wa kusitisha mapigano’ kuwa moja ya ulaghai mkubwa zaidi wa kisiasa na kimaadili.”

Mwishoni mwa kikao hicho, walitoa shukrani maalum kwa Ali Abbas Wafā, mhariri mkuu wa mtandao wa SNN, ambaye mbali na kuratibu na kuongoza kongamano hili, alibeba pia jukumu la kusimamia utekelezaji wa programu nzima. Kwa uongozi wake makini na hotuba zenye malengo ya wazi, aliweza kuunda mazingira ya umoja na mazungumzo yenye kujenga kati ya wanazuoni wa Kishia na Kisunni.

Lebo

Maoni yako

You are replying to: .
captcha