Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Hawza, – Idara ya Habari za Kimataifa – Qadir Akaras, Rais wa Umoja wa Maimamu wa Ahlulbayt (Ehlader) nchini Uturuki, ambaye alikuwa mgeni katika moja ya vipindi vya kituo cha Shabake Khabar cha televisheni ya Iran, katika tathmini yake juu ya matokeo ya kikao hicho kilichofanyika hivi karibuni katika mji wa Sharm al-Sheikh nchini Misri, alisema:
“Ijapokuwa kikao hiki kiliitishwa kwa jina la amani, lakini kama ilivyokuwa katika mikutano ya Camp David na Oslo, hatimaye kitakuwa na matokeo yenye kuumiza kwa mustakabali wa jambo la Palestina.”
Akaongeza: “Jabha ya muqawama, kama ilivyoshikamana kwa muda wa zaidi ya miaka 75 iliyopita, itaendelea kwa uthabiti katika njia yake. Mikutano kama hii kamwe haiwezi kuivunja irada ya muqawama. Wala Marekani, wala Israel, wala tawala za Kiarabu washirika wao, hawawezi kuizima azma na dhamira ya Wapalestina.”
Akaras alieleza kuwa kikao cha Sharm al-Sheikh kilifanyika katika mfumo wa mpango wa Rais wa Marekani Donald Trump unaolenga kutangaza usalama wa muda (au kusitisha mapigano), na kusema: “Jabha ya muqawama ilikataa masharti mengi yaliyokuwa yakilazimishwa na Trump. Wapalestina hawatakubali kamwe kuona damu ya mashahidi wao ikigeuzwa bidhaa ya biashara au mazungumzo. Tawala za Kiarabu ambazo zimekaa kimya kwa miaka miwili mbele ya mauaji ya kimbari ya Ghaza, hazina haki yoyote ya kuzungumza katika meza hii.”
Rais wa Ehlader aliendelea kusema kuwa hakutarajiwa kikao hicho kipate matokeo yoyote ya maana, akibainisha: “Mataifa ya muqawama yataendelea na njia yao. Matokeo pekee ya kikao hiki ni kudhihirika zaidi kwa azma na uimara wa jabha ya muqawama.”
Akaras alisisitiza pia: “Trump anajitahidi kujionesha kuwa mtu mpenda amani, lakini hili ni jaribio la kuosha sura yake iliyochukiwa. Kwa kuvaa vazi la amani, anataka kupunguza chuki ya umma dhidi yake, lakini hakuna atakayejidanganya na maigizo haya.”
Kuhusu mustakabali wa Ghaza, Akaras alisema: “Jambo muhimu ni upande gani umefikia malengo yake. Israel haijafanikiwa kufanikisha hata moja kati ya malengo yake iliyoitangaza. Ushindi wa kweli si wa kijeshi tu, bali ni ule wa kuzishinda nyoyo na dhamira za mataifa.”
Aidha, Akaras alitaja kutohudhuria kwa Benjamin Netanyahu katika kikao hicho kuwa ni ishara ya: “Chuki kubwa iliyo ndani ya jamii ya Israel na hofu binafsi ya Netanyahu juu ya usalama wake.”
Kuhusu kutohudhuria kwa Iran katika kikao hicho, alisema: “Jambo hili si udhaifu wa kidiplomasia hata kidogo. Iran ni nchi yenye sera huru za kigeni na hufanya maamuzi yake bila kushinikizwa au kuathiriwa na mataifa ya nje.”
Rais wa Ehlader pia alizungumzia nafasi ya Uturuki katika kikao hicho akisema: Uturuki, kwa kuwa ni mwanachama wa NATO, ililazimika kushiriki katika kikao hicho. Hata hivyo, Ankara ilibainisha waziwazi msimamo wake. Wakati huohuo, wananchi wa Uturuki walisimama imara upande wa muqawama wa Ghaza na kuonesha uungaji mkono wao kwa ari kubwa.”
Katika hitimisho la mahojiano hayo, Qadir Akaras alizungumzia pia safari yake ya hivi karibuni kwenda Iran baada ya vita na kusema: Katika mji wa Tehran hakuna dalili zozote za uharibifu wa vita. Watu wameendelea na maisha yao ya kawaida. Umoja na mshikamano wa wananchi wa Iran ni dalili ya uungaji mkono wao wa dhati kwa mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.”
Maoni yako