Alhamisi 16 Oktoba 2025 - 23:49
Misingi mitano ya maudhui katika ujumbe wa Kiongozi Mkuu wa Mapinduzi wa Iran kwa hawza / Wajibu wa kimataifa wa Hawza na maulama

Hawza/ Ayatullah Alireza A‘rafi amesisitiza kwamba “walengwa wa kwanza wa ujumbe wa Kiongozi Mkuu wa Mapinduzi katika kumbukumbu ya miaka mia moja ya kuasisiwa upya kwa Hawza ya kielimu ya Qum ni viongozi na walimu wa Hawza wenyewe.” Amesema: “Sisi viongozi na walimu ndio walengwa wa mwanzo wa ujumbe huu, na kwa hakika taasisi na makundi mbalimbali ndani ya Hawza katika ngazi zote zinabeba jukumu kubwa.”

Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Hawza, Ayatullah A‘rafi katika kikao cha walimu wa Taasisi ya Elimu ya Juu ya Fiqhi kilichofanyika katika kituo cha Amin Qum Iran, amesisitiza tena kwamba: “Sisi viongozi na walimu ndio walengwa wa kwanza wa ujumbe wa Kiongozi Mkuu wa Mapinduzi katika kumbukumbu ya miaka mia moja ya kuasisiwa upya Hawza ya Qum, na taasisi zote za kielimu zinawajibika kuutekeleza.”

Wajibu wa kimataifa wa Hawza na ulazima wa kuitikia mahitaji ya dunia ya kisasa

Mjumbe wa Baraza la Wataalamu wa uongozi (Majlisi Khobregan) amesema kuwa tangia ujana wake amekuwa na hamu ya kuona ujumbe wa Uislamu, Mapinduzi ya Kiislamu na mafundisho ya Ahlul Bayt (a.s) ukienea ulimwenguni. Alibainisha kuwa lengo kuu linalofuatwa katika taasisi ya Al-Mustafa International University ni kudhihirisha fikra na mafundisho ya Uislamu na Ahlul Bayt (a.s) katika mfumo wa mwanga wa Hawza na Mapinduzi ya Kiislamu kote ulimwenguni.
Akasema: “Pamoja na juhudi zote tulizofanya, bado tuko mwanzoni mwa safari.”

Ameongeza kwa kueleza kwamba katika safari zake za kimataifa katika miaka ya karibuni, ameona wazi kuwa dunia ya leo inahitaji ujumbe wa Uislamu na Mapinduzi ya Kiislamu. Akasema: “Kazi zote tunazofanya bado ni ndogo. Uhitaji huu si wa kinadharia tu, bali ni wa kweli na wenye hamu ya dhati. Hili ndilo jukumu muhimu zaidi lililoko mabegani mwa Hawza ya Qum, hususan jaamiatul Al-Mustafa.”

A‘rafi alisisitiza kuwa: “Hawza ya sasa imepiga hatua, lakini bado haijafikia kiwango inachotakiwa kuwa nacho. Nikipewa nafasi, naweza kuzungumza kwa saa kumi bila maandiko kuhusu mipango na miradi tuliyo nayo, lakini kwa yote hayo, bado tupo nyuma.”

Uchambuzi wa kihistoria wa Hawza na mtazamo wa ustaarabu wa Kiislamu

Ayatullah A‘rafi alisoma kipande cha Nahjul Balagha kinachomuelezea Mtume Mtukufu (s.a.w.w), akasema: “Mtume (s.a.w.w) alifungua milango ambayo isingefunguliwa ila kwa nuru yake. Aliibomoa fahari ya upotovu na kwa azma yake thabiti akaifanya njia ya haki iwe nyoofu.”

Kisha akarejea katika ujumbe wa hivi karibuni wa Kiongozi Mkuu wa Mapinduzi, akabainisha baadhi ya mihimili yake ya kimaudhui: Mojawapo ya mambo muhimu katika ujumbe huo ni mtazamo wa kihistoria na haja ya kuhuisha mtazamo wa kihistoria ndani ya Hawza.
Amesema: “Kwa ajili hiyo nimekiagiza kituo cha uandishi wa Hawza kuandaa maandiko ya kihistoria kwa muhtasari ili mashindano ya kielimu yaandaliwe kulingana nayo.”

Ameeleza kuwa maandiko hayo yatagawanywa katika sehemu tano:

1. Historia ya vijana na ulimwengu wa Magharibi wa kisasa;

2. Historia ya ulimwengu wa Kiislamu katika karne moja au mbili zilizopita;

3. Historia ya Iran kwa msisitizo maalum juu ya miaka 150 iliyopita;

4. Historia ya Hawza na wanazuoni wa Kishia, hasa Qum katika miaka 100 iliyopita;

5. Historia ya Mapinduzi ya Kiislamu.

Ayatullah A‘rafi amesema: “Uanazuoni wa Kishia umepitia nyakati za kupanda na kushuka nyingi, lakini kwa jumla umekuwa katika mwenendo wa maendeleo. Kutoka zama za taqiyya hadi harakati za baada ya Karbala, tumeshuhudia mwendelezo wa kupanda kwa Uislamu halisi.”

Akaendelea kusema: “Kuanzia enzi za Sheikh Mufid (r.a) na Sheikh Tusi (r.a) huko Baghdad, hadi zama za Khwaja Nasir na Allamah Hilli (r.a) wakati wa uvamizi wa Mongolia, harakati za kielimu na kitamaduni za Ahlul Bayt (a.s) zilifanya mageuzi makubwa kiasi cha kubadilisha hata dola ya kikandamizaji ya Wamongolia kuwa chombo cha kitamaduni.”

Mapinduzi ya Kiislamu – Kipindi cha kimkakati cha miaka elfu katika historia ya Kishia

Mkurugenzi wa vyuo vya kidini amesema kuwa Mapinduzi ya Kiislamu ni hatua ya kipekee katika historia ya Hawza.
Akasema: “Kile kilichotokea katika Mapinduzi ya Kiislamu chini ya uongozi wa Imam Khomeini (r.a) na Qum, ni tofauti kabisa na vipindi vyote vilivyotangulia. Zamani kulikuwa na harakati na vuguvugu zilivyosababisha mabadiliko ya kijamii na kisiasa, lakini Mapinduzi ya Kiislamu yalivunja hesabu za miaka elfu na kukusanya hazina zote za kihistoria za Kishia katika nukta moja.”

Ameongeza: “Kazi kuu ya jamiatul-Mustafa ni kufungua milango duniani kwa ajili ya kuifikisha elimu ya Ahlul Bayt (a.s). Mtazamo huu wa kihistoria unapaswa kuwa msingi wa awamu mpya ya mageuzi ndani ya Hawza.”

Uislamu unaounda ustaarabu; ukosoaji wa ustaarabu wa Magharibi na msisitizo wa kujitegemea kielimu

Ayatullah A‘rafi ameendelea kwa kusema kuwa “utambulisho wa kistaarabu” ni mojawapo ya mihimili muhimu zaidi katika ujumbe wa Kiongozi Mkuu wa Mapinduzi.
Amesema: “Mtazamo wa kistaarabu ni kinyume cha mitazamo ya juu juu kuhusu dini. Uislamu si mkusanyiko wa kauli zilizotawanyika, wala haupingani na maendeleo ya kisayansi ya mwanadamu. Uislamu ni mfumo wa kifikra ulio kamili kama mti wenye mizizi, unaoweza kubadilika kulingana na wakati huku ukihifadhi asili yake.”

Mjumbe wa Baraza Kuu Hawza amebainisha kuwa; ustaarabu wa kisasa wa Magharibi ulianza kwa falsafa ya kimaada, na umetengeneza mfumo wa kifikra na kimaadili kwa mwanadamu wa leo, ambao lazima ukosolewe na kufanyiwa mapitio kwa mtazamo wa kiakili, wa kina na wa kishujaa.
Akasema: “Ni jukumu la vyuo vya kidini kuandaa na kuwasilisha ulimwenguni mfumo mpya wa kistaarabu unaotegemea mafundisho ya Ahlul Bayt (a.s).”

Umuhimu wa kulea wanazuoni wenye upeo mpana na wa kimataifa

Mkurugenzi wa vyuo vya kidini nchini aliendelea kusema kuwa Taasisi ya Elimu ya Juu ya Fiqhi tangia kuasisiwa kwake imekuwa ni alama ya kushikamana na asilia za Hawza sambamba na mtazamo wa kisasa na wa kimataifa.
Akasema: “Kulea wanazuoni wabobezi, wenye mizizi imara na upeo mpana wa kielimu katika taasisi hii ni matunda yenye thamani kubwa ambayo yanapaswa kuendelezwa.”

Mjumbe huyo wa Baraza Kuu la Hawza aliongeza kuwa: “Leo katika nchi zote duniani tunahitaji wanazuoni walio na msingi thabiti – wajuzi wa fiqhi, teknolojia na tafsiri – ambao pia wana uwezo wa kufanya mazungumzo na kushirikiana kielimu na fikra mbalimbali. Wanafunzi wahitimu kati ya 50,000 hadi 70,000 wa Jamia Al-Mustafa walioko kote ulimwenguni ni ushahidi wa ushawishi na athari ya Hawza katika pembe zote za dunia.”

Mwisho, Ayatullah A‘rafi alisisitiza kwa kusema:
“Kwa sasa tunahitaji mwamko mpya katika malezi ya wanazuoni wenye upeo mpana – wanazuoni watakaobeba jukumu la uongozi wa kifikra, tafsiri na ijtihadi katika ngazi ya kimataifa. Hili ndilo jukumu kuu lililo juu ya mabega yenu walimu na wanafunzi wa taasisi hii.”

Lebo

Maoni yako

You are replying to: .
captcha