Kwa Mujibu wa Shirika la Habari la Hawza, Matini kamili ya ujumbe wa Ayatullah Subhani
Bismillahir Rahmanir Rahim
“Enyi watu! Mcheni Mola wenu ambaye amekuumbeni kutokana na nafsi moja, na akamuumba mke wake kutoka humo, na akaeneza kutoka kwao wanaume wengi na wanawake.”
(Surat an-Nisaa, Aya ya 1)
Mwanamke katika mtazamo wa Uislamu ni kiumbe wa kimungu, aliye sawa na mwanaume katika uumbaji na mwenza wake katika jukumu la kuunda na kuendeleza ubinadamu. Qur’ani inasisitiza kuwa wote wawili wameumbwa kutokana na “nafsi moja”: “Amekuumbeni kutokana na nafsi moja na akamuumba mke wake kutoka humo,”
ili kuonesha kuwa katika asili ya ubinadamu na uwezo wa kufikia ukamilifu, hakuna tofauti yoyote kati yao.
Dini tukufu ya Uislamu, kwa kumtambulisha Bibi Fatima Zahra (a.s) kama kielelezo cha mwanamke mwaminifu na mwenye fikra, imechora njia iliyo wazi ya heshima na utu wa mwanamke. Mwanamke huyo mtukufu, sambamba na haya na heshima, alikuwa kinara katika elimu, imani, ulinzi wa uongozi wa kiwilaya, na malezi ya kizazi cha waumini. Kwa njia hiyo, alionesha kwamba mwanamke anaweza kuwa mhimili wa uongozi na uamsho wa jamii.
Kwa upande mwingine, falsafa za kimaada na tamaduni za Magharibi, kwa kukata uhusiano na wahyi, maumbile halisi na akili safi, zimeipunguza hadhi ya mwanamke katika mipaka finyu ya starehe na manufaa, na kuinyang’anya familia utakatifu na maana yake ya kweli. Matokeo ya mtazamo huo ni kuporomoka kwa maadili na kudhoofika kwa msingi wa familia katika jamii za leo.
Kwa mujibu wa mafundisho ya Uislamu, wanawake wana nafasi ya msingi na yenye athari katika maisha ya kijamii. Wanaume na wanawake kwa pamoja ndio wanaotekeleza mahitaji ya jamii, na wote wawili wanapaswa kuhudumia jamii; ila nyanja za huduma hizo zinatofautiana.
Kukubali tofauti hizi na kuziheshimu kwa hekima ndiko kilele cha huduma bora kwa wote wawili, na ndiko haki ya kweli inakojidhihirisha.
Wito wa utafiti wa kina kuhusu utambulisho wa mwanamke na familia
Ayatullah Subhani amesisitiza kuwa katika zama hizi, ambapo kumekithiri mashambulizi ya kifikra na maswali mengi kuhusu masuala ya mwanamke na familia, jamii ya Kiislamu inahitaji kuliko wakati wowote ule kufanya uchambuzi wa kina wa kielimu na wa kimantiki kuhusu utambulisho na nafasi ya mwanamke na familia kwa mujibu wa mafundisho ya Qur’ani na akili safi.
Amesema kuwa kongamano la kitaifa “Mwanamke na Familia; Utafiti wa kiwahyi na kiakili” lililofanyika katika mji wa kielimu wa Kermanshah ni hatua yenye thamani na yenye kuleta matumaini kwenye mwelekeo huo.
Akasema: “Hakika mazungumzo ya kielimu na tafiti za kifikra, iwapo yataandaliwa kwa misingi ya wahyi na akili, yanaweza kuwa taa ya kuongozea jamii na mfano wa kuigwa kwa umma wa Kiislamu.”
Dua na shukrani
Ayatullah Subhani ametoa shukrani za dhati kwa wanazuoni, walimu, watafiti na hasa wanawake wasomi walioshiriki katika kongamano hilo, na akatarajia kuwa matokeo ya mijadala hiyo yatakuwa chanzo cha baraka za kielimu na kitamaduni kwa jamii ya Kiislamu.
Amemuomba Mwenyezi Mungu Mtukufu awape mafanikio zaidi wote waliohusika katika juhudi hii adhimu, na awateue katika huduma ya Qur’ani, kizazi cha Mtume (Ahlul Bayt), na thamani halisi za familia.
Wassalamu ‘alaykum wa rahmatullahi wa barakatuh
Ja‘far Subhani
Qum – Hawza ya Qum Iran.
Maoni yako