Kwa mujibu wa ripoti ya Shirika la Habari la Hawza, mfululizo wa tafiti kuhusiana na Mahdawiyyah zikiwa na anuani isemayo “Kuielekea Jamii Bora”, zimetolewa kwa lengo la kueneza mafundisho na elimu zinazohusiana na Imam wa Zama (aj) kwenu nyinyi wasomi adhimu.
Fikra ya “Mahdawiyyah” katika Uislamu ina mizizi katika Qur’ani, na Kitabu hiki cha mbinguni kwa yakini kimewapa wanadamu wote bishara ya ushindi wa mwisho wa Haki juu ya Batili.
Qur’ani imezungumzia kwa ujumla juu ya kudhihiri na kisimamo cha Imam Mahdi (aj) na imeeleza bishara ya kuundwa serikali ya uadilifu wa kimataifa na ushindi wa watu wema. Wafasiri wa Kishia na baadhi ya wafasiri wa Kisunni wamezihusisha aya hizi na Imam Mahdi (aj) kwa kuzingatia riwaya za Ahlul-Bayt (as) na mitazamo ya wanazuoni wa Kiislamu.
Katika fursa hii, kutoka jumla ya aya za Qur’ani zinazohusiana na masuala ya Mahdawiyyah na ambazo zina uwazi zaidi kuhusu mada hii, tutanukuu na kuchambua aya chache tu.
Kwa kuanza bahthi hii, ni muhimu kufahamu maana ya baadhi ya maneno yafuatayo:
1. Tafsiri
Neno “tafsiri” limetokana na kitenzi “fasara” (فَسَرَ) likimaanisha kufafanua na kuweka wazi. Kwa istilahi, tafsiri ni “kuondoa utata kutoka kwenye neno gumu” na pia “kuondoa utata uliomo katika dalili ya maneno”.
Tafsiri inahitajika pale ambapo kuna aina fulani ya utata katika neno, hali ambayo husababisha utata katika maana na dalili ya usemi, na kuondoa hali hii kunahitaji juhudi kubwa.
Kwa kuwa baadhi ya aya za Qur’ani hazieleweki wazi kwa watu wa kawaida, kuna haja ya ufafanuzi na kubainishwa kwake, jambo ambalo ni jukumu la wale wenye sifa, uwezo na waliothibitishwa na Mwenyezi Mungu Mtukufu.
2. Ta’wil (تأویل)
Ta’wil imetokana na neno “a-w-l” (أول) likimaanisha kurejea kwenye asili. Ta’wil ya kitu ni kukirudisha kwenye mahali na chanzo chake cha asili; na ta’wil ya neno lenye utata ni kulitafsiri kwa namna ambayo linafikia maana yake halisia na ya msingi.
Neno hili limetumika katika Qur’ani kwa maana tatu:
Kueleza maana ya neno au kitendo chenye utata kwa njia sahihi inayokubalika kiakili na kulingana na maandiko. (Sura Āl ʿImrān: 7)
Maelezo ya ndoto, ambapo ta’wil kwa maana hii imetumika mara nane kwenye Surat Yūsuf.
Mwisho au matokeo ya jambo, yaani kile ambacho jambo hilo huishia kuwa nacho. (Sura al-Kahf: 78)
Maana ya nne - ambayo haipo katika Qur’ani lakini inapatikana katika maneno ya wanazuoni wa zamani — ni kutoa maana pana kutoka kwenye aya iliyoteremshwa kwa tukio maalum. Ta’wil kwa maana hii wakati mwingine huitwa “batn” (maana ya ndani iliyofichika ambayo haionekani wazi katika maandishi ya aya), kinyume cha “ẓaahr” (maana ya nje inayoeleweka moja kwa moja kutokana na matumizi ya maneno).
Maana hii ina upeo mpana unaohakikisha kuenea ujumbe wa Qur’ani katika zama zote, kwa sababu kama maana pana zisingetolewa kutoka kwenye matukio maalum, aya nyingi za Qur’ani zingebakia bila manufaa zaidi ya thawabu ya kuisoma na kurudia tu.
Hakika ndani ya Qur’ani kuna aya mutashaabih ambazo lazima zifanyiwe ta’wil, lakini hakuna anayeijua ta’wil yake isipokuwa Mwenyezi Mungu na wale walio waliozama katika elimu. (Āl ʿImrān: 7)
Ta’wil ina masharti na vigezo maalum ambavyo vimeelezwa katika vitabu husika.
3. Tatb'iq (تطبیق)
Katika aya za Qur’ani, kuna mambo mengi yaliyoelezwa kwa lafudhi ya jumla, ambayo yanaweza kutumika kwa watu mbalimbali katika zama tofauti. Wakati mwingine, maneno ya aya ni maalum, lakini maana yake ni ya jumla na inajumuisha pia wale wanaofanya matendo yanayofanana na yaliyoelezewa katika aya.
Kwa kuzingatia nukta hizi, baadhi ya aya zinazomhusu Imam Mahdi (aj) na mapinduzi ya kimataifa atakayoyaongoza zitawekwa mezani kwa ajili ya kufanyiwa utafiti.
Utafiti huu unaendelea…
Imenukuliwa kutoka kwenye: Kitabu kiitwacho “Darsnāmeh-ye Mahdawiyyat” kilichoandikwa na Khodamrad Salimiyān, huku ikifanyiwa mabadiliko kiasi.
Maoni yako