Kwa mujibu wa ripoti ya Kitengo cha tarjuma cha Shirika la Habari la Hawza, siku ya Jumanne serikali ya Chile ilitoa tamko rasmi ikiweka wazi wasiwasi wake mkubwa kuhusu kitendo kilichofanywa na utawala wa Kizayuni cha kuuzuia na kuukamata msafara wa kimataifa "Sumud”, uliokuwa unasafirisha misaada ya kibinadamu kwa wakazi wa Ghaza walioko chini ya vikwazo.
Tamko hilo lilibainisha kuwa meli za msafara wa Sumud zilikuwa zikielekea kufikisha msaada wa haraka kwa raia wa Ghaza, hasa wanawake na watoto waliokuwa waathirika wa mashambulizi na mzingiro. Kitendo cha utawala wa Kizayuni kimetajwa kuwa ni uvunjaji wa wazi wa uhuru wa usafiri wa baharini unaohakikishwa katika Mkataba wa Sheria za Bahari, na pia ni kinyume na misingi ya sheria za kimataifa na kibinadamu.
Serikali ya Chile ilisisitiza kwamba misingi ya sheria za kimataifa za kibinadamu inazilazimisha serikali zote kuruhusu na kuhakikisha upitishaji wa misaada ya kibinadamu bila vizuizi vyovyote kwa raia wasiohusika na vita. Iliongeza kuwa:
“Kukamatwa kwa msafara huu ni kitendo kisicho halali na ni uvunjaji wa majukumu yanayotambulika kimataifa.”
Chile pia ilitaka uhakikisho wa haraka wa usalama na afya ya waliojitolea na wahudumu wa msafara wa Sumud, pamoja na kuwezesha upatikanaji huru na wa haraka wa misaada ya kibinadamu kuelekea Ukanda wa Ghaza. Aidha, ilizitaka jumuiya za kimataifa kuchukua msimamo thabiti dhidi ya vitendo vya kinyume cha sheria kama hivyo.
Maoni yako