Kwa mujibu wa ripoti ya kitengo cha tarjama cha Shirika la Habari la Hawza,, Ishaq Dar, Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Mambo ya Nje wa Pakistan, katika kikao cha Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kilichohusu hali ya Mashariki ya Kati na suala la Palestina alisema: Ghaza imegeuka kuwa makaburi ya ubinadamu na dhamiri ya ulimwengu, sasa ni wakati wa jamuiya ya kimataifa kufanya uamuzi wa kithabiti, kulinda heshima ya kibinadamu, kusimamisha uadilifu na kuhakikisha utaratibu wa kuwawajibisha wahusika.
Akiashiria hali ya kutisha ya Palestina, aliongeza: Wapalestina wasio na ulinzi wanakumbwa kila siku na hasara kubwa za kibinadamu zisizoweza kurekebishwa. Nyumba zao, mitaa na miundombinu imebomolewa, na kwa kusambaratika mfumo wa kijamii, maisha yao ya kila siku yameporomoka.
Ishaq Dar, huku akirejelea takwimu za kutisha, alitangaza: Hadi sasa zaidi ya Wapalestina 64,000 wameuawa kishahidi na zaidi ya watu laki moja kujeruhiwa. Ghaza ipo ukingoni mwa njaa kali na maisha ya karibu watu 500,000 yako hatarini kwa sababu ya njaa. Aidha, watu 300,000 wamekuwa wakimbizi na tishio la kupoteza makazi kwa watu wengine milioni moja ni kubwa.
Akiendelea na kusisitiza kwamba haki za binadamu huko Ghaza zinavunjwa vikali, alisema: Israel haijafanya tu uhalifu wa kibinadamu bali pia imevunja waziwazi sheria za kimataifa. Ujenzi wa vitongoji haramu katika Ukingo wa Magharibi na utekelezaji wa miradi yake ni mfano wa wazi wa ukiukaji wa moja kwa moja wa sheria za kimataifa.
Naibu Waziri Mkuu wa Pakistan akiwahutubia wajumbe wa Baraza la Usalama aliongeza: Wakati wa maneno umepita; sasa ni wakati wa vitendo. Jumuiya ya kimataifa lazima iifikishe Israel kwenye meza ya haki na kuzuia kuendelea kwa jinai hizi.
Mwisho, alibainisha kuwa: Pakistan inaendelea kusisitiza msimamo wake wa dhati na wa kudumu wa kuwaunga mkono wananchi wa Palestina na inakaribisha mkutano wa pamoja wa Pakistan, Saudi Arabia na Ufaransa kuhusu suluhisho la mataifa mawili kwa Palestina. Tunahakikisha kwamba uungaji mkono wa dhati kwa dhana ya Palestina utaendelea hadi pale haki na uhuru vitakapopatikana.
Maoni yako