Kwa mujibu wa kitengo cha tarjuma cha Shirika la Habari la Hawza, haishangazi tena kwamba Saudi Arabia, kwa sababu zisizo na mantiki na kwa kutumia vibaya ukimya wa serikali ya Iraq na kutojali kwa Wizara ya Mambo ya nje kuhusu haki za Wairaq wanaoishi nje ya nchi, hufanya ukamataji wa kivikundi, maafisa wa Kisaudia wamewakamata waumini vijana wa Iraq, ambao baadhi yao walikuwa wanafunzi, kwa sababu ya kupiga picha katika makaburi ya Maimamu wa Baqi na kuonesha picha za makamanda wa muqawama wakiwemo mashahidi Sayyid Hassan Nasrallah, Abu Mahdi al-Muhandis na Hajj Qasim Suleimani.
Jambo hili limevisukuma baadhi ya vyama vya kisiasa kudai haki za waliokamatwa hawa ambao karibu mwaka mzima sasa wapo gerezani, hata hivyo, msimamo rasmi wa serikali kuhusu suala hili nyeti bado hauonekani, na hali hii itapelekea maandamano kufanyika mbele ya ubalozi wa Saudi Arabia mjini Baghdad baada ya kumalizika safari ya kumbukumbu ya kufariki Mtume (s.a.w).
Husein al-Kar’awi, mwenyekiti wa kamati ya kuratibu harakati ya wananchi wa Iraq, alisema: Saudi Arabia kwa takriban mwaka mmoja sasa imewashikilia baadhi ya Wairaq waliokuwa wakitekeleza ibada ya Umra katika magereza yake, hili linathibitisha udhaifu wa utendaji wa Wizara ya Mambo ya Nje na kushindwa kwake kuwalinda raia wa Iraq walioko nje ya nchi, hususan katika Ufalme wa Saudia.
Aliongeza kuwa: Saud Arabia imewakamata Wairaq kwa sababu ya kubeba picha za mashahidi Sayyid Hassan Nasrallah, Qasim Soleimani na Abu Mahdi al-Muhandis katika magereza yake, Ukamataji huu utakuwa na athari mbaya, na serikali inapaswa kutekeleza wajibu wake wa kuwalinda wananchi wa Iraq.
Al-Kar’awi aliendelea kusema: Maandalizi yamefanywa kwa ajili ya kufanyika maandamano mbele ya ubalozi wa Saudia mjini Baghdad baada ya kumalizika safari ya kumbukumbu ya kufariki Mtume (s.a.w) ili kudai kuachiliwa kwa Wairaq waliokamatwa katika magereza ya Aal Saud.
Akasema wazi: Vijana waliokamatwa nchini Saudia wanahusisha madaktari na wanafunzi wa vyuo vikuu walio chini ya miaka 20, mmoja wa vijana hao ni mwanafunzi wa udaktari wa meno ambaye alikuwa ameambatana na bibi yake katika ibada ya Umra, maafisa wa Kisaudia walimkamata miezi 11 iliyopita kwa kosa la kupiga picha makaburi ya Maimamu wa Baqi (a.s).
Kwa upande mwingine, Ra’id al-Maliki, mbunge huru wa bunge la Iraq, alisisitiza kuwa maafisa wa Kisaudia mnamo Septemba 29, 2024 waliwakamata vijana watano Wairaq waliokuwa wameenda kutekeleza ibada ya Umra na waliokuwa Madina wakati wa kukamatwa, kwa sababu ya kutoa mkono wa pole kwa shahada ya Sayyid Hassan Nasrallah katika akaunti zao binafsi za mitandao ya kijamii, hadi leo wako gerezani Saudia bila kosa lolote.
Alibainisha kuwa waliokamatwa ni pamoja na wanafunzi na walimu wa vyuo vikuu, na familia zao ziliandaa mkusanyiko mdogo mbele ya Wizara ya Mambo ya Nje, lakini haikuwa na faida yoyote na hakuna kiongozi rasmi aliyewasiliana nao.
Maliki alitangaza juu ya kuwasilisha swali bungeni, ambapo kupitia hati, ameihoji Wizara ya Mambo ya nje: Hatua za wizara yako ni zipi kuhusu kuachiliwa kwa Wairaq 9 ambao kwa miezi kadhaa sasa wamefungwa Saudia bila kutangazwa mashtaka dhidi yao, bila kufikishwa mahakamani au kuteuliwa wakili wa kuwatetea?
Aliendelea kuuliza: Je, ni kweli kwamba maafisa wa Kisaudia wamewakamata mahujaji au waumini wa Umra wa Iraq kwa sababu ya kuwa na machapisho kwenye simu zao ambayo yanapingana na sheria za Ufalme, hata kama machapisho hayo yalitumwa kabla ya muumini kuingia Saudia? Je, makubaliano ya ushirikiano wa kiusalama na kisheria yaliyosainiwa baina ya nchi mbili yametumika katika kushughulikia suala la urejeshaji?
Katika muktadha huo huo, Muhammad al-Baldawi, mbunge wa “Mfumo wa Uratibu”, alifafanua kuwa serikali ya Iraq inalazimika kuwatetea wananchi wake, hususan kwa kuwa raia hawa 9 hawakufanya uvunjaji wowote wa sheria wala makosa dhidi ya Ufalme au wananchi wake, bali walitekeleza tu ibada za kidini wanazoziamini, kwa kuwa kumshikilia mmoja wao kwa zaidi ya miezi 11 ni hatua ya kiholela iliyo wazi.
Aliongeza: Hasa ikizingatiwa kwamba mahujaji kutoka Saudia na nchi nyingine ndani ya Iraq wanatekeleza ibada zao kwa uhuru kamili bila zuio lolote, basi ukimya wa muda mrefu wa Wizara ya Mambo ya Nje hauna uhalali wowote na lazima ukome mara moja.
Al-Baldawi aliiomba Wizara ya Mambo ya nje ya Iraq kufuatilia suala hili kwa umakini na haraka kupitia njia rasmi za kidiplomasia na kuhakikisha kuachiliwa kwa waliokamatwa na kurejea kwao kwenye familia zao.
Maoni yako