Jumapili 24 Agosti 2025 - 22:45
Wanajeshi wa Sweida nchini Syria wametangaza kuundwa kwa “Gadi ya Kitaifa”

Hawzah/ Makundi ya kijamii katika mkoa wa Sweida nchini Syria, makazi ya Wadrusi, katika siku za hivi karibuni wametangaza kuungana kwao katika Gadi ya Kitaifa kwa lengo la kuunganisha jitihada za kijeshi

Kwa mujibu wa kitengo cha tarjama cha Shirika la Habari la Hawza, makundi ya kijamii katika mkoa wa Sweida nchini Syria, makazi ya Wadrusi, katika siku za hivi karibuni wametangaza kuungana kwao katika Gadi ya Kitaifa kwa lengo la kuunganisha jitihada za kijeshi.

Kwa mujibu wa kituo cha habari cha sehemu ya Sweida 24, vikundi kadhaa vilivyoko vitani nchini Syria vilitoa taarifa kuhusu kuungana kwao katika “jeshi moja,” na kubainisha kwamba hatua hiyo inalenga kuunda “nguvu thabiti na iliyo na mpangilio madhubuti itakayolinda na kutetea nchi na wananchi wake.”

Jana Jumamosi, viongozi kadhaa wa makundi hayo walifanya kikao katika makao ya “uongozi wa kiroho wa Wadrusi” kwa ajili ya kuunganishwa katika jeshi la Gadi ya Kitaifa.

Chanzo kutoka ndani ya uongozi wa Gadi ya Kitaifa kimesema sababu kuu za kuundwa kwa jeshi hilo na kuunganishwa kwa makundi yenye silaha ndani yake ni “kujaza pengo la kiusalama ili kuhakikisha eneo halingii katika machafuko baada ya kukosekana taasisi rasmi, kuunganisha safu kwa kuzikusanya pande zote za eneo hilo chini ya amri moja badala ya migawanyiko na mashindano, kudhibiti silaha ili kuzuia machafuko yanayosababishwa na kuenea kiholela kwa silaha, na kulinda vijiji dhidi ya mashambulizi yoyote.”

Chanzo hicho kimeongeza kuwa jukumu la Gadi ya Kitaifa linajumuisha “kupambana na ugaidi na kukabiliana na makundi yoyote yenye misimamo mikali yanayojaribu kuenea Sweida, hususan Daesh na makundi mengine yanayofanana nayo.”

Chanzo hicho pia kimeashiria kuwa malengo haya yanajumuisha “mawasiliano na ushirikiano wa kikanda na kimataifa na muungano wa kimataifa katika nyanja za kubadilishana taarifa na operesheni za kijeshi dhidi ya makundi ya kigaidi.”

Chanzo hicho kimebainisha kuwa Gadi ya Kitaifa itajitahidi kulinda na kudhibiti mipaka upande wa jangwa la Badiya ili kuzuia kuingia kwa wanamgambo au silaha za magendo na dawa za kulevya, na kuiona hatua hii kuwa ni njia ya kuelekea kuunganishwa kwa makundi ndani ya mfumo wa kitaasisi ili “kudhamini uwepo wao ndani ya mfumo wa dola ya baadaye na sheria.”

Chanzo hicho kimeeleza kwa Sweida 24 kwamba Gadi ya Kitaifa itajitokeza kama chombo cha kijeshi cha eneo hilo na nguvu ya kimuundo ambapo wakaazi wote wa Sweida watashiriki ndani yake kwa ajili ya kulinda mji na kushiriki katika vita dhidi ya ugaidi pamoja na washirika wa kikanda na kimataifa.

Lebo

Maoni yako

You are replying to: .
captcha