Kwa mujibu wa ripoti ya Idara ya tarjuma ya Shirika la Habari la Hawza, Hujjatul-Islam Sayyid Ahmad Iqbal Ridhwi, Makamu wa Rais wa Bunge la Umoja wa Waislamu wa Pakistan, katika kujibu hali ya kusikitisha na ya hatari huko Ghaza, huku akionesha masikitiko makubwa kwa ukimya wa jamii ya kimataifa, ametangaza kuwa: Kifo cha makumi ya watoto wasio na hatia kwa sababu ya njaa huko Ghaza si janga la kibinadamu pekee; bali ni onyo kwa dhamira zilizonyamaza, ni kengele ya hatari inayolingania ubinadamu kuamka kabla ya kusimama kwa Qiyama.
Akinukuu ripoti rasmi ya Umoja wa Mataifa, amesema wazi kuwa: Utawala wa Kizayuni umezuia zaidi ya asilimia 80 ya misaada ya kibinadamu, hii ni hakika chungu na yenye ushahidi, si madai ya kisiasa, leo hii njaa inatumika makusudi kama silaha ya kivita dhidi ya raia wasio na hatia; kitendo ambacho kwa mtazamo wa mashirika ya kimataifa kama "Human Rights Watch" na "Amnesty International" ni mfano wa wazi wa “uhalifu wa kivita”.
Mwanachuoni huyu mashuhuri wa Kipakistani ameongeza kuwa: Nyuma ya jinai hizi, kuna msaada wa kifedha na kisiasa kwa Wizayuni nchini Marekani, Marekani siyo tu kwamba haijayanyamazia maafa haya, bali inaiunga mkono kila upande Israel, na imekuwa mshirika wa moja kwa moja wa dhulma hizi, wakati huo huo, nguvu kubwa za dunia na wanasiasa wao wanaendelea kutazama mauaji haya ya kizazi bila ya kutoa majibu yoyote.
Akiashiria wajibu wa kihistoria wa Pakistan, amesema: Nchi iliyoundwa kwa kauli ya tauhidi na kwa mwanga wa Kalimat Tayyibah, na mwanzilishi wake, Muhammad Ali Jinnah, aliyekuwa daima mtetezi wa haki za Wapalestina, leo hii inapaswa kueleza waziwazi kuwa inasimama wapi katika suala hili. Je, sisi ni watazamaji tu wa kufa kwa watoto kwa njaa au tutakuwa sauti yenye nguvu na mtetezi wa wanyonge?
Mwisho, Makamu wa Rais wa Bunge la Umoja wa Waislamu wa Pakistan amewataka viongozi wa nchi za Kiislamu wavunje ukimya wao na kutekeleza wajibu wao wa kidini, kibinadamu na kihistoria.
Ameonya kuwa: Iwapo leo Waislamu na watawala wao watanyamaza mbele ya janga hili, kesho historia na vizazi vijavyo havitasamehe udhaifu huu kamwe.
Maoni yako