Ijumaa 16 Mei 2025 - 11:01
Rais wa Baraza la Maulamaa wa Kishia Pakistan: Israeli ni utawala wa kimabavu, usio halali na ni tishio kwa amani ya dunia

Hawza/ Hujjatul-Islam wal-Muslimin Sayyid Sajid Ali Naqvi, katika ujumbe wake kwenye mnasaba wa Siku ya Nakba (15 Mei), amelieleza utawala wa Kizayuni kuwa ni utawala wa kunyang’anya kwa nguvu na usio halali, na akautaja kuwa ni tishio kubwa kwa amani na usalama wa dunia.

Kwa mujibu wa ripoti ya idara ya tarjama ya  Shirika la Habari la Hawza, sambamba na kuwadia kwa tarehe 15 Mei, ambayo ni kumbukumbu ya "Siku ya Nakba", Hujjatul-Islam wal-Muslimin Sayyid Sajid Ali Naqvi, Rais wa Baraza la Maulamaa wa Kishia Pakistan, katika ujumbe wake akigusia kuasisiwa kwa utawala wa Kizayuni, alisema:

Israeli ni utawala wa kimabavu na usio halali, ambao hauna uhalali wa kihistoria wala wa kijiografia; bali umechoma kama kisu chenye damu katikati ya moyo wa Mashariki ya Kati na umeuweka hatarini usalama wa eneo hilo na wa dunia nzima.

Akaongeza kusema: Karne moja iliyopita, hakukuwa na jina wala athari ya Israili katika ramani za kisiasa za dunia. Wakati huo, ni asilimia mbili tu ya ardhi ya Palestina iliyokuwa makazi ya Wayahudi wachache sana. Lakini kwa kutolewa "Tangazo la Balfour" na kwa maamuzi ya kamati maalum ya Shirikisho la Mataifa, mchakato wa kuwahamisha Wayahudi kwenda Palestina ulianza, lakini kwa masharti kwamba makazi hayo yawe kwa ridhaa kamili na bila ya kulazimisha, na kwamba haki za kihistoria za watu wa Kiarabu wa Palestina ziheshimiwe.

Mwanachuoni huyu mashuhuri wa Kipakistani aliendelea kusema: Kwa kupita muda, si tu kwamba masharti hayo hayakuzingatiwa, bali kwa msaada wa wazi wa mabeberu wa kikoloni, Mayahudi wachache walio kuwepo eneo hilo wakageuka hatua kwa hatua kuwa utawala wa kimabavu na wenye kumwaga damu. Hadi kufikia mwaka 1948, kwa vitendo vya kikatili na vya uvamizi, ardhi ya Wapalestina ilinyakuliwa kutoka kwa wakaazi wake halisi, na ukazuka utawala ambao historia yake imejaa mauaji ya halaiki, maangamizi ya vizazi, uvunjaji wa wazi wa haki za binadamu na uhalifu wa kivita. Na hadi leo, katika mwaka huu wa 2025, utawala huu haramu ungali umeendelea kuwepo katika ramani ya dunia huku ukiwa na rekodi ya giza.

Rais wa Baraza la Maulamaa wa Kishia Pakistan alisisitiza kuwa: Israeli ni kama kisu chenye sumu na dhulma kilichochomwa katikati ya moyo wa Mashariki ya Kati ambacho si tu kwamba kinatishia mataifa ya eneo hilo, bali pia kimeiweka hatarini amani ya dunia nzima.

Akiashiria juhudi mpya za kuupatia uhalali utawala huu wa kunyang’anya kwa nguvu kupitia mikataba kama "Mapatano ya Ibrahimu", alisema: Inasikitisha kwamba wakati maafa makubwa yamewashukia watu wa Palestina na Gaza, baadhi ya watu – badala ya kusimama upande wa waliodhulumiwa – kwa ujasiri wa hali ya juu wanazungumza kuhusu haki ya kuishi kwa watu wa Ghaza, kana kwamba wameusahau mzizi wa suala hilo na kiini cha dhulma hiyo.

Mwishoni, "Hujjatul-Islam wal-Muslimin Sayyid Sajid Ali Naqvi" alisisitiza: Sisi tunalaani kila aina ya kuutambua utawala wa Israeli, na tunaona kuwa ni kushirikiana na dhulma na jinai. Kutetea Palestina na kuwaunga mkono waliodhulumiwa ni jukumu la kibinadamu, Kiislamu na kimaadili linaloyaemea mataifa yote, serikali zote na watu wote huru duniani.

Lebo

Maoni yako

You are replying to: .
captcha