Jumatatu 12 Mei 2025 - 13:50
Umri wa Imamu wa zama (a.s)

Hawza | Kwa mujibu wa itikadi ya wafuasi wa dini zote za mbinguni, vitu vyote ulimwenguni viko chini ya mamlaka ya Mwenyezi Mungu, na athari zitokanazo na vitu hivyo zinategemea matakwa Yake. Iwapo Yeye hataki, vitu hivyo hupoteza athari zake. Na pia Yeye huumba na kupatisha vitu bila ya kuwepo sababu ya kiasili au ya kimaumbile.

Shirika la Habari la Hawza - Miongoni mwa mijadala kuhusu maisha ya Imamu Mahdi (as) ni suala la umri wake mrefu. Kwa baadhi ya watu, swali hili huibuka: inawezekanaje mtu kuwa na umri wa muda mrefu kiasi hiki?!

Sababu ya kuulizwa swali hili ni kuwa kwa mujibu wa hali ya kawaida iliyozoeleka katika dunia ya leo, maisha ya binadamu huwa mafupi na yenye kikomo. Hivyo basi, baadhi ya watu wanapokutana au kusikia habari kuhusu maisha marefu ya mtu, huona ni vigumu kuamini jambo hilo. Lakini ukweli ni kuwa maisha marefu si jambo lisilowezekana kwa akili au elimu ya mwanadamu. Watafiti na wanasayansi, kwa kuchunguza viungo vya mwili wa mwanadamu, wamefikia hitimisho kwamba inawezekana binadamu kuishi kwa muda mrefu mno na hata asipatwe na uzee au uchakavu wa mwili.

Juhudi za wanasayansi kutafuta njia za kushinda uzee na kufikia maisha marefu ni ishara tosha ya uwezekano wa jambo hili. Na kwa kweli, hatua kadhaa za mafanikio zimekwishapigwa katikasuala hili.

Katika vitabu vya mbinguni na vya kihistoria, kumetajwa wanadamu wengi kwa majina yao na maelezo ya maisha yao, ambao walikuwa na maisha marefu zaidi kuliko binadamu wa leo.

Katika Qur'ani Tukufu, kuna aya ambayo haizungumzii tu maisha marefu bali pia inathibitisha uwezekano wa maisha ya milele. Aya hiyo inamhusu Nabii Yunus (as), ambapo Mwenyezi Mungu anasema:

«فَلَوْلَا أَنَّهُ کَانَ مِنَ الْمُسَبِّحِینَ، لَلَبِثَ فِی بَطْنِهِ إِلَی یَوْمِ یُبْعَثُونَ.»

Na lau kuwa yeye hakuwa miongoni mwa wanaomtakasa (Mwenyezi Mungu), basi bila shaka angalikaa ndani ya tumbo la samaki mpaka Siku watakapofufuliwa. (Surat: swafat, ay: 143-144)

Kwa hivyo, kwa mujibu wa Qur’ani, maisha marefu mno kutoka zama za Nabii Yunus (as) hadi Siku ya Kiyama, jambo ambalo wanabiolojia huliita “maisha ya milele” yanawezekana kwa mwanadamu na hata kwa samaki.

Qur’ani Tukufu pia inasema kuhusu Nabii Nuh (‘alayhis-salām):

«وَلَقَدْ أَرْسَلْنَا نُوحًا إِلَیٰ قَوْمِهِ فَلَبِثَ فِیهِمْ أَلْفَ سَنَةٍ إِلَّا خَمْسِینَ عَامًا فَأَخَذَهُمُ الطُّوفَانُ وَهُمْ ظَالِمُونَ.»

Na kwa yakini, tulimtuma Nuh kwa watu wake, naye akakaa kati yao miaka elfu ila hamsini; kisha Gharika ikawapata nao walikuwa madhalimu. (surat: Ankabut, aya: 14)

Kinachotajwa katika aya hiyo tukufu ni muda wa ujumbe wa kinabii wa mtukufu huyo. Kwa mujibu wa baadhi ya riwaya, jumla ya umri wake ilikuwa miaka 2450.

Cha kushangaza ni kwamba katika riwaya moja kutoka kwa Imamu Sajjad (as) amenukuliwa akisema:

«فِی اَلْقَائِمِ مِنَّا سُنَنٌ مِنَ اَلْأَنْبِیَاءِ ... فَأَمَّا مِنْ آدَمَ وَ نُوحٍ فَطُولُ اَلْعُمُرِ.»

kuna katika mwenye kusimama kati yetu (Imamu wa zama) suna za Manabii... Ama suna yake kutoka kwa Adam na Nuh ni maisha marefu. (Kamal ad-Dīn, juz. 1, uk. 321)

Qur'ani Tukufu pia inasema kuhusu Nabii Isa (‘alayhis-salām):

«وَمَا قَتَلُوهُ وَمَا صَلَبُوهُ وَلَٰکِنْ شُبِّهَ لَهُمْ ... بَلْ رَفَعَهُ اللَّهُ إِلَیْهِ.»

Wala hawakumuua wala hawakumsulubisha, bali iliwadhihirikia hivyo... bali Mwenyezi Mungu alimwinua kwake. (Surat: Nisaa, Aya:157-158)

Mbali na Qur’ani, hata katika Taurati na Injili, suala la maisha marefu limezungumziwa.

Katika Taurati imeandikwa:

“Siku zote za maisha ya Adam zilikuwa miaka mia tisa na thelathini, naye akafa. Na Shethi aliishi miaka mia na tano, akamzaa Enoshi. Na baada ya kumzaa Enoshi, Shethi aliishi miaka mia nane na saba, akazaa wana na binti. Na siku zote za Shethi zilikuwa miaka mia tisa na kumi na miwili, naye akafa... Siku zote za Lameki zilikuwa miaka mia saba na sabini na saba, naye akafa. Na Nuhu alikuwa na umri wa miaka mia tano, ndipo akawazaa, Hamu na Yafethi.”  (Kitabu cha Mwanzo, Sura ya Tano, Aya 5–32)

Kwa hiyo Taurati inakiri waziwazi kuwepo kwa watu waliokuwa na maisha marefu sana (zaidi ya miaka 900).

Katika Injili pia kuna maelezo yanayoonyesha kuwa Nabii Isa (as) baada ya kusulubiwa, alifufuka na kupaa mbinguni, na atashuka tena katika siku za mwisho. Ni wazi kuwa hadi sasa, umri wake umeshazidi miaka elfu mbili.

Kwa hivyo, ni wazi kuwa wafuasi wa dini mbili —Uyahudi na Ukristo— kwa mujibu wa imani yao katika vitabu vitakatifu, wanapaswa pia kuamini uwepo wa maisha marefu.

Zaidi ya hayo, maisha marefu yanakubalika kielimu(1) na kiakili, na yamethibitishwa kihistoria mara nyingi. Kadhalika, yanathibitishwa katika muktadha wa uwezo usio na mipaka wa Mwenyezi Mungu. Kwa mujibu wa imani ya wafuasi wote wa dini za mbinguni, chembe zote za ulimwengu ziko chini ya mamlaka ya Mwenyezi Mungu, na athari zote za visababishi na sababu zinategemea matakwa Yake. Na hata bila sababu za kawaida au za kiasili, Anaweza kuumba na kupatisha chochote Atakacho.

Yeye ni Mungu ambaye alitoa ngamia kutoka katika jabali, akaufanya moto wenye kuwaka kuwa baridi na salama kwa Nabii Ibrahim (as), na akaikausha bahari kwa ajili ya Musa na wafuasi wake, akawapitisha kati ya kuta mbili za maji. Je, itawezekana kwa Yeye kushindwa kumpa maisha marefu mtu aliye kiini cha Manabii na Mawalii, akiba ya mwisho ya Mungu, tumaini la waumini wote wema, na mtimizaji wa ahadi kuu ya Qur’ani?!

----------------------------------------------

(1) Kinachokusudiwa katika “uwezekano wa kielimu” ni kuchunguza iwapo jambo fulani, japo halijatekelezwa kwa teknolojia ya sasa, halipingani na sheria za kielimu. Wanasayansi mashuhuri kama "Weizmann" (mwanasayansi Mjerumani), "Floker" (mwanaphysikia), Dkt. "Kaylor DeHows" (Mmarekani), Profesa "Ettinger" na "Diamond W. Beryl" kutoka Chuo Kikuu cha Johns Hopkins wamekubaliana kwamba maisha ya binadamu yanaweza kurefuka hadi kufikia hata mamia ya miaka.
 

Utafiti huu unaendelea...
Imenukuliwa kutoka kitabu “Negin-e Āfarinish” huku ikifanyiwa marekebisho kiasi

Lebo

Maoni yako

You are replying to: .
captcha