Jumatatu 5 Mei 2025 - 09:11
Hakuna manufaa yoyote kwa Umma wa Kiislamu yaliyo juu zaidi kuliko umoja

Kiongozi Mkuu wa Mapinduzi ya Kiislamu, katika kikao na waandaaji wa Hija pampja na kundi la mahujaji wa Nyumba Tukufu ya Mwenyezi Mungu, alisema kuwa lengo la Mola kwenye ibada ya Hija ni kuwasilisha kielelezo kamili na chenye mwelekeo wa kuiongoza jamii ya wanadamu, na akasisitiza: Leo hii, manufaa makubwa zaidi kwa Umma wa Kiislamu ni “umoja na kuunganisha nguvu” kwa ajili ya kutatua matatizo katika ulimwengu wa Kiislamu. Kama kungekuwa na umoja huo, masuala kama ya Ghaza na Yemen yasingetokea.

Kwa mujibu wa  Shirika la Habari la Hawza, Ayatollah Sayyid Ali Khamenei, Kiongozi Mkuu wa Mapinduzi ya Kiislamu, leo asubuhi katika kikao na waandaaji wa Hija na kundi la mahujaji wa Nyumba Tukufu ya Mwenyezi Mungu, alitaja kuwa kuelewa na kutambua malengo na vipengele mbalimbali vya Hija ni utangulizi wa utekelezaji sahihi wa ibada hii adhimu, na kwa kunukuu aya nyingi za Qur'ani Tukufu, aliongeza: Kutumika kwa neno (watu) katika aya nyingi zinazohusiana na Hija kunaonyesha kuwa Mola Mtukufu ameweka ibada hii kwa ajili ya kusimamia mambo ya wanadamu wote, kwa hiyo; kuendesha Hija katikaa njia sahihi ni kuhudumia ubinadamu.

Katika kufafanua vipengele vya Hija, alitaja kuwa hiyo ni ibada ya pekee ambayo sura na muundo wake ni ya kisiasa kwa asilimia mia moja; kwa kuwa kila mwaka inawakusanya watu katika mahali na wakati mmoja kwa malengo maalum, jambo ambalo kiasili lina asili ya kisiasa.

Ayatollah Khamenei aliongeza kuwa: Mbali na muundo wa kisiasa wa Hija, maudhui ya kila sehemu ya ibada hiyo ni ya kiroho na ya kiibada kwa asilimia mia moja, na kila moja ina ishara ya mfano na mafundisho yenye kuhusiana na masuala na mahitaji tofauti ya maisha ya mwanadamu.

Katika kufafanua ishara hizi, alitaja somo la “Tawafu” kuwa ni ulazima wa kuzunguka kwenye mhimili na sehemu ya Tawhidi (kumpwekesha Mwenyezi Mungu), na akaongeza kusema: Tawafu inamfundisha mwanadamu kuwa serikali, maisha, uchumi, familia na kila jambo la maisha linapaswa kujengwa juu ya msingi wa Tawhidi, na iwapo itakuwa hivyo, basi hakuna tena ukatili huu, mauaji ya watoto na tamaa zisizo na mipaka, bali dunia itakuwa kama bustani ya maua.

Kiongozi wa Mapinduzi alitaja “Sa’i kati ya Safa na Marwa” kuwa ni ishara ya ulazima wa mtu kufanya juhudi daima kati ya milima ya matatizo, na kamwe asisimame wala kusita.

Ayatollah Khamenei alitaja “kuelekea Arafah, Muzdalifah (Mash’ar) na Mina” kuwa ni somo la kuendelea kusonga mbele na kuepuka kusimama au kupooza, na akaongeza kuwa: Sadaka ya kuchinja mnyama ni ishara ya mfano wa ukweli kwamba mara nyingine mtu hulazimika kuacha hata wapendwa wake zaidi, kutoa sadaka au hata kujitoa muhanga mwenyewe.

Aidha, alieleza kuwa “kurusha mawe kwenye Jamarat” kuwa Mola anasisitiza lazima mtu awatambue mashetani majini na watu, na popote atakapomkuta shetani, ampige na amuangamize.

Kiongozi wa Mapinduzi pia alieleza kuwa “kuvaa Ihram” ni alama ya unyenyekevu na usawa kwa wanadamu mbele ya Mola, na akaongeza: Matendo yote haya ni kuyaelekeza maisha ya wanadamu katika njia sahihi.

Kwa kunukuu aya ya Qur'ani Tukufu, Kiongozi wa Mapinduzi alieleza kuwa lengo la “mkusanyiko” wa Hija ni kufahamu na kufikia aina mbalimbali za manufaa ya kibinadamu, na akasema: Leo hii hakuna manufaa yaliyo juu zaidi kwa Umma wa Kiislamu kuliko umoja, na iwapo kungekuwa na umoja, mshikamano na kuunganisha nguvu kwa Umma wa Kiislamu, maafa yanayoendelea Ghaza na Palestina yasingetokea, wala Yemen isingewekwa katika hali hii ya mashinikizo.

Ayatollah Khamenei alieleza kuwa, kutengana na kugawanyika kwa Umma wa Kiislamu kunatoa nafasi kwa mustakbali wa wakoloni, Marekani, utawala wa Kizayuni na wenye tamaa kupita kiasi kutawala mataifa, na akaongeza kusema: Kwa umoja wa Umma, usalama, maendeleo, kuunganisha nguvu kati ya nchi za Kiislamu, na kusaidiana baina yao kunawezekana, na fursa ya Hija inapaswa kutazamwa kwa mtazamo huo.

Lebo

Maoni yako

You are replying to: .
captcha