Shirika la Habari la Hawza - Mohsen Mahdawi, mwenye asili ya Kipalestina na mmiliki wa Kadi ya Kijani (Green Card), akiwa ni mkazi halali kwa zaidi ya miaka kumi nchini Marekani, alikamatwa na Idara ya Uhamiaji na Forodha (ICE) mnamo Aprili 14. Katika kikao chake cha kwanza mahakamani siku ya Jumatano, jaji alitoa amri ya kuendelea kumzuia kwa muda, na akaamuru aendelee kuzuiliwa katika kituo cha jimbo la Vermont hadi kikao kingine kitakachofanyika wiki ijayo.
Mawakili wa Mahdawi wanasema kuwa alikamatwa sababu ya matamshi yake ya kutetea haki za binadamu za Wapalestina.
“Kile ambacho serikali imewasilisha hadi sasa kinathibitisha kuwa msingi pekee wa kumkamata kwa namna hiyo ni hotuba yake halali,” alisema wakili Luna Droubi baada ya kikao hicho. “Tunatarajia kurejea baada ya wiki moja kwa ajili ya kumkomboa Mohsen.”
Katika hati yake ya kisheria iliyopelekwa mahakamani hivi karibuni, serikali ilisisitiza kuwa kuzuiliwa kwa Mahdawi kunazingatia misingi ya katiba, na kwamba suala la kupitia muda na taratibu za kuanzisha kesi za uhamisho wa raia lipo nje ya mamlaka ya mahakama za wilaya.
Kwa mujibu wa mawakili wa Mohsen Mahdawi, kabla ya kukamatwa kwake, alijibu maswali yote na kusaini hati iliyoonesha wazi kuwa amejitolea kutetea katiba na sheria za Marekani. Hata hivyo, maafisa waliovaa barakoa kutoka ICE waliingia ghafla katika chumba cha mahojiano, wakamfunga pingu bila kuonesha sababu yoyote ya kisheria, kisha wakampeleka kizuizini.
Wakili wa kesi hiyo alitoa onyo kwa waandishi wa habari kwa kusema: Kuwakamata wanafunzi wa daraja la juu wasio na rekodi ya kihalifu ni ukiukaji wa wazi wa haki za kiraia. Hakuna kifungu hata kimoja katika sheria za uhamiaji za Marekani kinachohalalisha kitendo hiki cha kiholela.
Mwezi uliopita, waziri wa mambo ya nje Marco Rubio alisema kuwa wizara ya mambo ya nje ilikuwa inabatilisha viza za wageni waliokuwa wakienda kinyume na maslahi ya taifa, wakiwemo baadhi ya waliokuwa wakipinga vita ya Israel dhidi ya Ghaza.
Kwa mujibu wa mawasilisho ya mahakamani, Mahdawi alizaliwa katika kambi ya wakimbizi huko ukingo wa magharibi (West Bank) na alihamia Marekani mwaka 2014. Hivi karibuni alikamilisha masomo yake chuoni Columbia na alitarajiwa kuhitimu mwezi Mei kabla ya kuanza masomo ya shahada ya uzamili katika chuo hicho kipindi cha vuli.
Akiwa mwanafunzi, Mahdawi alikuwa mkosoaji mkubwa wa operesheni ya kijeshi ya Israel huko Ghaza na aliandaa maandamano chuoni hadi mwezi Machi 2024.
Siku ya Jumanne, baadhi ya wabunge wa Congress kutoka jimbo la Massachusetts walielekea Louisiana kukutana na Ozturk pamoja na mwanafunzi wa Columbia Mahmoud Khalil. Seneta wa Marekani Ed Markey na Wawakilishi wa Marekani Ayanna Pressley na Jim McGovern walieleza wasiwasi wao katika mkutano na waandishi wa habari siku ya Jumatano kwamba wanafunzi hao, pamoja na wengine waliokamatwa, wananyimwa chakula chenye lishe, usingizi, na blanketi katika vituo vyenye baridi.
Kulingana na ujumbe huo wa wabunge, Khalil na Ozturk hawajafanya uhalifu wowote wanazuiliwa kinyume cha sheria kwa kutumia haki yao ya uhuru wa kujieleza.
“Wanashambuliwa na kufungwa kwa sababu ya mitazamo yao ya kisiasa,” alisema McGovern.
Maoni yako