Jumamosi 28 Novemba 2026 - 12:40
Ayatullah Saidi Atoa Ujumbe wa Kulaani Hukumu za Kifungo cha Maisha Dhidi ya Wanazuoni wa Bahrain

Hawza/ Msimamizi wa Haram Tukufu ya Bibi Fatimah Ma’asumah (sa), katika ujumbe wake, akizungumzia kutolewa hukumu za kifungo cha maisha kwa idadi kubwa ya wanazuoni, viongozi wa dini na wananchi wa Kishia, ameandika: “Kwa upande wangu, huku nikilaani vikali hukumu hizi, ninaziomba taasisi za kimataifa na za kutetea haki za binadamu, jumuiya za kidini pamoja na wapigania uhuru duniani wasikae kimya mbele ya ukiukwaji wa haki na uhuru wa kidini wa wananchi wa Bahrain, na zichukue hatua madhubuti za kufutwa hukumu zisizo za haki, kusitishwa ukandamizaji wa kidini na kuachiliwa huru mara moja wafungwa bila masharti yoyote.”

Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Hawza, Ayatullah Sayyid Muhammad Saidi, kupitia ujumbe wake, amelaani kutolewa hukumu za kifungo cha maisha dhidi ya wanazuoni wa Bahrain na vyombo vya mahakama vya nchi hiyo.

Matini kamili ya ujumbe huo ni kama ifuatavyo:

Kwa jina la Mwenyezi Mungu, Mwingi wa rehema, Mwenye kurehemu.

Mtume wa Mwenyezi Mungu (saww) amesema:

«مَنْ أَهَانَ لِی وَلِیّاً فَقَدْ أَرْصَدَ لِمُحَارَبَتِی»

“Yeyote anayemdhalilisha mmoja wa wapenzi wangu, kwa hakika amejitayarisha kupambana nami.”

Wanazuoni wa dini wamebeba jukumu zito la kulinda mafundisho ya Mwenyezi Mungu, kuiongoza jamii na kuhifadhi tunu za kidini. Kwa msingi huo, kuvunja heshima yao na kuzuia shughuli zao za kidini na kijamii si suala linalohusu kushughulika na watu binafsi pekee, bali ni uvamizi dhidi ya hadhi ya elimu, fikra na uhuru wa kidini.

Hatua isiyo ya haki iliyochukuliwa hivi karibuni na vyombo vya mahakama ya Bahrain ya kutoa hukumu za kifungo cha maisha kwa idadi kubwa ya wanazuoni, viongozi wa dini na wananchi wa Kishia, bila kuzingatia masharti ya mwenendo wa haki wa mashauri ya mahakama na haki zao za msingi za kutetea haki zao halali, zikiwemo haki ya uhuru wa kujieleza na uhuru wa dini, ni hatua ya kusikitisha na yenye kuibua wasiwasi mkubwa. Hatua hiyo inakinzana na misingi ya Sharia, sheria za ndani na sheria za kimataifa.

Historia ya Uislamu inashuhudia kwamba wanazuoni wa dini daima wamekuwa wakibeba jukumu la kuielimisha jamii, kutetea haki na kuiongoza jamii kiakili na kiroho, hata katika mazingira magumu zaidi. Haiwezekani kupuuza matakwa ya kiitikadi na kijamii ya taifa kwa kuwanyima wanazuoni hao uhuru wao, kuwawekea shinikizo au kuwazuia kufanya shughuli zao za kidini.

Uzoefu pia umeonesha kwamba kutumia mbinu kali dhidi ya imani na utambulisho wa kidini wa wananchi si njia ya kutatua tofauti zilizopo, bali huongeza tu ukosefu wa uaminifu na kupanua pengo kati ya wananchi na mamlaka za utawala. Kwa hiyo, inatarajiwa kwamba viongozi wa Bahrain, badala ya kutumia hatua za adhabu na kiusalama, watachukua njia ya mazungumzo, kuheshimu haki za kisheria na kutambua tofauti za kidini na kiitikadi zilizopo ndani ya jamii.

Kulinda heshima ya wanazuoni wa dini ni kuhifadhi heshima ya elimu na mafundisho ya Mwenyezi Mungu. Hakuna jamii yoyote itakayoweza kufikia amani na utulivu wa kudumu bila ya kuwepo uadilifu na kuheshimiwa kwa uhuru unaotambuliwa kisheria.

Kwa upande wangu, huku nikilaani vikali hukumu hizi, ninaziomba taasisi za kimataifa na za kutetea haki za binadamu, jumuiya za kidini pamoja na wapigania uhuru duniani wasikae kimya mbele ya ukiukwaji wa haki na uhuru wa kidini wa wananchi wa Bahrain. Aidha, ninaziomba zichukue hatua madhubuti za kufutwa hukumu zisizo za haki, kusitishwa kwa ukandamizaji wa kidini na kuachiliwa huru mara moja kwa wafungwa bila masharti yoyote.

Wassalaam Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh.

Msimamizi wa Haram Tukufu ya Bibi Fatimah Ma’asumah (sa) na Imam wa Swala ya Ijumaa ya Qum,

Sayyid Muhammad Saidi

Lebo

Maoni yako

You are replying to: .
captcha