Jumamosi 28 Novemba 2026 - 09:40
Ayatullah Mudarrisi Awahimiza Wanafunzi wa Hawza Kusoma na Kuiga Mwenendo wa Wanazuoni Wacha Mungu

Hawza/ Ayatullah Sayyid Muhammad Taqi Mudarrisi, miongoni mwa wanazuoni wa Iraq, ameielezea elimu kuwa ndiyo njia ya kuikweza jamii na kufikia daraja ya juu. Aidha huku akisisitiza umuhimu wa kujituma katika kujifunza elimu ya Qur’ani na Ahlul-Bayt (as), amewahimiza wanafunzi wa Hawza kusoma mwenendo na historia ya maisha ya wanazuoni wacha Mungu na wenye kumuogopa Mwenyezi Mungu.

Kwa mujibu wa kitengo cha tarjama cha Shirika la Habari la Hawza, Ayatullah Sayyid Muhammad Taqi Mudarrisi, miongoni mwa wanazuoni wa Iraq, amesisitiza kuwa elimu ndiyo njia pekee ya kuikweza jamii na kufikia daraja ya juu, alipokuwa akitoa darsa yake ya maadili ya kila wiki kwa wanafunzi wa Hawza katika mji mtakatifu wa Karbala.

Alibainisha kuwa kutafuta elimu ni lengo kubwa ambalo linapaswa daima kuwa akilini mwa Waumini na kushika nafasi ya kwanza katika vipaumbele vya maisha yao.

Ayatullah Mudarrisi amesisitiza umuhimu wa kuwa na juhudi na bidii katika kujifunza elimu ya Qur’ani Tukufu na Ahlul-Bayt (as), pamoja na kuzitumia katika kuwahudumia waja wa Mwenyezi Mungu, kuendeleza na kuustawisha miji na nchi, na kutafuta radhi za Mwenyezi Mungu.

Aidha, aliwataka wanafunzi wa Hawza kusoma mwenendo na historia ya maisha ya wanazuoni wacha Mungu (wa zama za sasa na za kale), ili waige mbinu na mwenendo wao na kunufaika na uzoefu wao. Alisisitiza zaidi umuhimu wa kuwaiga wanazuoni waliopambana kwa juhudi kubwa na waliokuwa wakiyatekeleza kwa vitendo yale waliyojifunza, ambao wameacha athari za kudumu katika mwenendo na harakati za Umma. Wanazuoni hao walikuwa na mchango mkubwa katika kuleta mabadiliko ya kihistoria na kuitumikia jamii kupitia elimu zao na misimamo yao.

Ayatullah Mudarrisi pia, alipokuwa akielezea baadhi ya mifano ya mwenendo na historia ya maisha ya wanazuoni wa zamani, aliangazia sifa, maadili na misimamo mbalimbali waliyokuwa nayo. Alibainisha kuwa miongoni mwa wanazuoni hao walikuwapo waliobeba jukumu la kuuongoza Umma, waliosimama kidete dhidi ya madhalimu na watawala madhalimu, na walioshiriki katika kuasisi Hawza za kielimu ambazo zilikuwa na nafasi ya mstari wa mbele katika harakati za mageuzi.

Alieleza kuwa; Hawza hizo zilikuwa na mizizi iliyojikita kwa kina ndani ya jamii, na daima zilikuwa karibu na jamii, zikishiriki katika masuala yake na kujishughulisha na changamoto pamoja na sintofahamu zake.

Lebo

Maoni yako

You are replying to: .
captcha