Jumamosi 28 Novemba 2026 - 11:40
Kongamano Kuu la Vyama vya Kiarabu Lapinga Hukumu Dhuluma Dhidi ya Wanazuoni wa Bahrain

Hawza/ Sekretarieti Kuu ya Kongamano Kuu la Vyama vya Kiarabu imelaani na kupinga hukumu za dhuluma zilizotolewa na utawala wa Aal Khalifa dhidi ya wanazuoni wa dini na wanaharakati wanaotetea uhuru, ambao wameendesha harakati za kupinga hatua za kidhalimu za utawala huo.

Kwa mujibu wa Kitengo cha tarjama cha Shirika la Habari la Hawza, Sekretarieti Kuu ya kongamano hilo, katika taarifa yake, imesema: “Matakwa ya wananchi wa Bahrain yanategemea kupatikana haki ya kweli na ushirikishwaji. Wananchi wa taifa hili wameandaa maandamano, matembezi ya kupinga dhuluma na migomo mbalimbali kwa ajili ya kufikia lengo hilo. Hata hivyo, mapambano haya yanaendelea licha ya mauaji yaliyopangwa, kukamatwa kwa wingi viongozi wa makundi ya kimapinduzi, pamoja na maamuzi ya kuwapeleka uhamishoni viongozi wa kidini na viongozi wa kifikra.”

Kongamano hilo pia limepongeza msimamo thabiti wa harakati za wananchi wa Bahrain, likisisitiza kuwa harakati hizo, licha ya kukabiliwa na mbinu zote za ukandamizaji zinazopuuza haki za kiraia na haki za binadamu, hazijawahi kuingia katika mtego wa kutumia vurugu wala kuachana na njia yake ya amani.

Aidha, lilieleza kuwa wananchi wenye heshima wa Bahrain wanaendelea kusisitiza matakwa yao ya haki na kuendeleza harakati zao kwa ajili ya kufikia malengo yao halali na kudai haki zao za kijamii na kisiasa.

Sekretarieti Kuu ya Kongamano Kuu la Vyama vya Kiarabu, huku ikilaani hukumu za kisiasa zilizotolewa na mahakama za utawala huo, limetangaza mshikamano wake na wafungwa wa kimapinduzi. Vilevile, limeviomba vikosi vyote, makongamano, vyama na jumuiya za kutetea haki za binadamu kuchukua hatua kubwa zaidi za kuuwekea shinikizo utawala wa Aal Khalifa, ili kuulazimisha kuwaachilia huru wanazuoni wa dini na wafungwa wengine wa dhamiri.

Taarifa hiyo, huku ikieleza kuwa wafungwa hao wanakabiliwa na aina mbaya zaidi za dhuluma, ukandamizaji na kunyang'anywa uhuru, ambayo yanakinzana na Mikataba ya Haki za Binadamu pamoja na sheria za kimataifa zinazohusu uhuru wa kujieleza, uhuru wa itikadi na kutoa maoni, imesisitiza tena kuwaunga mkono wapambanaji hao mashujaa na wananchi wa Bahrain, ambao wako tayari kujitoa kwa kila kitu chenye thamani kwa ajili ya kulinda heshima, utu na uhuru wao.

Lebo

Maoni yako

You are replying to: .
captcha