Jumatatu 23 Novemba 2026 - 07:34
Ayatullah Araki Aonya Kuhusu Madhara ya Makabiliano Kati ya Utawala wa Kidikteta wa Bahrain na Wananchi

Hawza/ Mjumbe wa Baraza Kuu la Hawza amelaani kutolewa hukumu dhidi ya kundi la wanazuoni na watu mashuhuri nchini Bahrain, huku akionya kuhusu madhara yanayoweza kusababishwa na makabiliano kati ya utawala wa kidikteta wa Bahrain na wananchi wake.

Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Hawza, Ayatullah Araki, ambaye ni mjumbe wa Baraza la Kutambua Maslahi ya Mfumo na mjumbe wa Baraza Kuu la Hawza za Kielimu, ametoa taarifa akilaani kutolewa hukumu dhidi ya kundi la wanazuoni na watu mashuhuri nchini Bahrain, huku akionya kuhusu matokeo ya makabiliano kati ya utawala wa kidikteta wa Bahrain na wananchi.

Maandishi kamili ya taarifa hiyo ni kama ifuatavyo:

Kwa jina la Mwenyezi Mungu, Mwingi wa rehema, Mwenye kurehemu.

Watawala wa Bahrain wametoa hukumu ya dhuluma dhidi ya idadi kubwa ya watu mashuhuri na wasomi wa nchi hiyo, huku hukumu hiyo ikiwajumuisha pia wanazuoni wengi mashuhuri zaidi wa Bahrain; wanazuoni ambao ni vinara katika unyenyekevu, kumcha Mwenyezi Mungu, kujali maslahi ya taifa lao na kulinda maslahi ya wananchi huru na wenye heshima wa Bahrain.

Kutolewa hukumu hii ya dhuluma kunamaanisha kuingia katika makabiliano hatari kati ya utawala wa kidikteta na wananchi wote wa Bahrain. Makabiliano hayo yanawalazimisha wanamageuzi na watu wapenda uhuru wa taifa hili kubwa kuingia katika mapambano ya msingi dhidi ya utawala huo. Makabiliano hayo hayatakwisha isipokuwa kwa kuondolewa mfumo huu wa kidikteta, kujinasua kutoka katika utawala wake na kufunguliwa njia ya ustawi, maendeleo na maisha katika mazingira salama yenye uhuru, kujitawala na uadilifu kwa wananchi wa Bahrain.

Ni wajibu kwa watawala wa Bahrain kuitikia vyema matakwa ya wananchi wa nchi hiyo kabla mambo hayajafikia hatua ambayo haitakuwa rahisi kuyadhibiti, na kusikiliza nasaha za wanazuoni wanaolijali taifa hili, wakiongozwa na kiongozi wao mkuu wa kidini, Sheikh Isa Qasim. Hakika, Mwenyezi Mungu daima anawangojea madhalimu na madikteta.

Muhsin Araki

Lebo

Maoni yako

You are replying to: .
captcha