Kwa mujibu wa Idara ya tarjama ya Shirika la Habari la Hawza, inatarajiwa kuwa Waislamu watakuwa kundi kubwa zaidi la kidini duniani ifikapo mwaka 2035, na hivyo kuwapita Wakristo ambao kwa muda mrefu wamekuwa wakishikilia nafasi hiyo. Endapo mwenendo wa sasa utaendelea, tofauti ya idadi ya watu kati ya makundi hayo mawili itaendelea kuongezeka katika miongo ijayo. Inakadiriwa kuwa ifikapo mwaka 2070, idadi ya Waislamu duniani inaweza kufikia watu bilioni 3.64, ikilinganishwa na Wakristo bilioni 2.96.
Makadirio haya yametokana na utafiti mpana uliofanywa na Kituo cha Utafiti cha Pew, kwa kutumia takwimu za sensa na tafiti zinazohusu mambo mbalimbali, yakiwemo viwango vya uzazi, uhamiaji, vifo, umri na kile kinachoitwa “mabadiliko ya dini”.
Tafiti za kituo hicho cha Magharibi zinasema kuwa sababu kuu ya hali hii ni kuhamasishwa wanawake Wakristo kupata elimu na kuajiriwa katika kazi zenye saa nyingi za kufanya kazi na kipato kikubwa. Hali hiyo imesababisha wanawake wengi walioelimika kutokuwa na shauku ya kupata na kulea watoto, badala yake wameelekeza fikra zao katika kuongeza kipato na kupata fursa bora zaidi za kiuchumi.
Hata hivyo, tunaona kuwa Waislamu wanapohamia katika nchi za Magharibi, viwango vyao vya uzazi pia hupungua na kuanza kufuata mwenendo huo. Gharama kubwa za maisha katika miji mikubwa pia ni miongoni mwa sababu zinazochangia hali hiyo, kwani wanandoa wote hulazimika kufanya kazi, jambo linalowapunguzia wanawake fursa ya kulea watoto.
Katika nchi ambazo Waislamu ni wengi, kwa kawaida utamaduni uliopo ni kwamba mmoja wa wanandoa, ambaye mara nyingi huwa ni mwanaume, hufanya kazi kwa bidii, huku mwanamke akijishughulisha zaidi na malezi ya watoto. Hali hiyo yenyewe huchangia kuongezeka kwa idadi ya Waislamu ikilinganishwa na Wakristo.
Kwa mujibu wa maoni ya wataalamu wa Magharibi, njia ya Ukristo kukabiliana na mwenendo huu ni kutekeleza sera za kuwahamasisha wanawake Waislamu kutafuta fursa za kiuchumi, hata kama zitakuwa chache, ili kupunguza kasi ya ongezeko la idadi ya watu katika nchi hizo.
Takwimu za Pew katika kipindi cha miaka mitano iliyopita zimeonyesha kuwa wanawake Waislamu wamekuwa na wastani wa watoto 3.1 kwa kila mwanamke, kiwango ambacho ni cha juu zaidi ikilinganishwa na makundi mengine yote ya kidini.
Kwa upande mwingine, ingawa wanawake Wakristo walikuwa na kiwango cha pili kwa juu cha uzazi katika kipindi hicho hicho, wastani wa watoto wao ulikuwa 2.5 kwa kila mwanamke, idadi ambayo ni ndogo kwa kiasi kikubwa ikilinganishwa na wanawake Waislamu.
Chanzo: time.com
Maoni yako