Jumatatu 23 Novemba 2026 - 15:00
Imamu wa Swala ya Ijumaa Baghdad Atoa Onyo Kali kwa Waziri Mkuu wa Iraq

Hawza/ Ayatullah Sayyid Yasin Mousavi, Imamu wa Swala ya Ijumaa mjini Baghdad, ameionya serikali ya Iraq dhidi ya kujifunga na mataifa yenye nguvu duniani, huku akiitaka ichukue sera ya kutofungamana na upande wowote kwa mtazamo chanya, na kuilinda nchi dhidi ya kuingizwa katika makabiliano na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, Hizbullah na mhimili wa Muqawama, au kulenga vikosi vya Hashd al-Shaabi.

Kwa mujibu wa Idara ya Kimataifa ya Shirika la Habari la Hawza, Ayatullah Sayyid Yasin Mousavi, Imamu wa Swala ya Ijumaa mjini Baghdad na mmoja wa walimu mashuhuri wa Hawza ya kielimu ya Najaf Ashraf, ameitaka serikali ya Iraq kufuata sera ya kutofungamana na upande wowote kwa mtazamo chanya na kulinda uhuru wa maamuzi ya kitaifa.

Aidha, ameonya dhidi ya kuingizwa Iraq katika makabiliano na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, Hizbullah na mhimili wa Muqawama, au kuilenga Hashd al-Shaabi kwa kisingizio cha kuhodhi silaha mikononi mwa serikali pekee.

Imamu huyo wa Swala ya Ijumaa Baghdad amezungumzia mabadiliko ya kimataifa na kikanda, mustakabali wa mamlaka ya kitaifa ya Iraq, pamoja na wajibu wa serikali katika kuilinda nchi dhidi ya migogoro ya nje na tofauti za ndani.

Ayatullah Mousavi, akibainisha kuwa Iraq imepata mafanikio muhimu tangu mwaka 2003, alisisitiza kuwa nchi hiyo bado haijafikia uhuru kamili na inaendelea kukabiliwa na vikwazo vya nje pamoja na utegemezi katika masuala ya kifedha, kiuchumi na kiusalama.

Alieleza kuwa mikutano ya mataifa yenye nguvu duniani inaakisi ushindani wa kulinda maslahi na maeneo ya ushawishi. Marekani, Urusi na China, kila moja hutenda kwa kuzingatia hesabu na maslahi yake maalumu. Kwa hiyo, haiwezekani kutegemea taifa lolote kati ya hayo katika kuweka maslahi ya Iraq mbele ya maslahi yake yenyewe.

Imamu huyo wa Swala ya Ijumaa Baghdad alisisitiza kuwa nguvu za kisiasa nchini Iraq zinapaswa kuelewa kwamba uhuru hauwezi kupatikana kwa kutegemea matakwa ya mataifa ya nje, bali unahitaji kuimarisha uwezo wa kitaifa na kufanya maamuzi kwa kuzingatia maslahi ya wananchi wa Iraq.

Iran na mhimili wa Muqawama vimebadilisha mizania ya kisiasa katika eneo

Ayatullah Mousavi aliitaja Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kuwa ni mfano wa uhuru wa kisiasa, akibainisha kuwa nchi hiyo, katika miongo iliyopita, imeendelea kulinda uhuru wake wa kufanya maamuzi licha ya shinikizo za mara kwa mara kutoka Marekani, iwe katika kipindi cha tawala za chama cha Democratic au Republican.

Akieleza kuwa Iran, licha ya kutoshiriki katika mkutano wa kimataifa, bado ni nchi inayojitegemea katika maamuzi yake, aliongeza kuwa mataifa yenye nguvu duniani, yakiwemo Urusi na China, pia hushirikiana na Iran kwa kuzingatia hesabu na maslahi yao maalumu.

Alibainisha kuwa Marekani, licha ya kuwa na nguvu kubwa za kijeshi pamoja na uwezo wa kiuchumi na kisiasa, imeshindwa kuuangusha mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.

Alisema kuwa mabadiliko ya hivi karibuni yameweka wazi mipaka ya uwezo wa Marekani katika kulazimisha matakwa yake katika eneo hili, huku kambi za kijeshi za Marekani pia zikikabiliwa na shinikizo na mashambulizi katika muktadha wa makabiliano na Iran.

Ayatullah Mousavi alibainisha kuwa; mabadiliko hayo yamezifanya baadhi ya nchi za eneo hili kutathmini upya hesabu zao, kwa sababu zimebaini kuwa kuishinda Iran kijeshi si jambo linalowezekana kwa urahisi. Aidha, imekuwa wazi kuwa utulivu wa eneo unahitaji kujenga mahusiano yanayotegemea urafiki, maelewano na ushirikiano, badala ya kutegemea uungwaji mkono wa Marekani au kushiriki katika mipango inayolenga kuishambulia Tehran.

Pia alieleza kuwa harakati za kikanda za kuimarisha mahusiano na Pakistan, Uturuki, China na Urusi zinaonesha jitihada za kupanua wigo wa uhuru dhidi ya Marekani. Kwa mujibu wake, mabadiliko ya hivi karibuni yamezipa nchi za eneo hilo fursa zaidi ya kufanya maamuzi yanayolingana na maslahi yao ya kitaifa.

Imamu huyo wa Swala ya Ijumaa Baghdad, katika sehemu nyingine ya mazungumzo yake, alizungumzia hali ya Hizbullah ya Lebanon, Ansarullah ya Yemen na makundi mengine ya mhimili wa Muqawama, akisisitiza kuwa jitihada za Marekani na utawala wa Kizayuni za kuyadhoofisha makundi hayo hazijafikia malengo yake yote.

Akizungumzia kuuawa kwa Sayyid Hassan Nasrallah, Katibu Mkuu wa Hizbullah ya Lebanon, pamoja na operesheni za kijeshi za utawala wa Kizayuni, alisema kuwa hatua hizo hazikupelekea mwisho wa shughuli za Hizbullah. Alibainisha kuwa Hizbullah bado ina uwezo wa kuathiri mizania ya kisiasa na kiusalama, huku ikiendelea kulinda uhuru wake wa kufanya maamuzi.

Ayatullah Mousavi pia, akizungumzia mabadiliko ya Yemen, alieleza kuwa uimara wa Ansarullah na kuendelea harakati hiyo kusimama imara ni ishara ya ugumu wa kuzisalimisha nguvu za kikanda kwa kutumia nguvu za kijeshi pekee.

Alisema kuwa jitihada za kukata uhusiano wa kikanda wa Iran, kuanzia Syria hadi Lebanon na Yemen, zinafanyika ndani ya mkakati wa Marekani wa kudhoofisha nafasi ya Iran. Hata hivyo, hatua hizo hazijaweza kuhitimisha nafasi na mchango wa mhimili wa Muqawama.

Imamu huyo wa Swala ya Ijumaa Baghdad alionya kuwa; kuingizwa Iraq katika makabiliano na Iran au Hizbullah hakutakuwa na manufaa yoyote ya kitaifa kwa nchi hiyo, bali kutaiweka katika hatari zinazozidi uwezo na rasilimali zake.

Akihoji sababu za kuchukua misimamo ya uadui dhidi ya Hizbullah na Mashia wa Lebanon, au kuingilia mizania ya kikanda inayozidi uwezo wa Iraq wa kuwa na ushawishi, alisisitiza kuwa; sera za namna hiyo zinaweza kuiweka nchi hiyo katika makabiliano na nguvu ambazo haina nyenzo na uwezo unaohitajika wa kukabiliana nazo.

Kupinga kulengwa vikosi vya Hashd al-Shaabi

Ayatullah Mousavi, katika sehemu nyingine ya mazungumzo yake kuhusu masuala ya ndani ya Iraq, alisisitiza kuwa kanuni ya kuhodhi silaha mikononi mwa serikali si jambo linalobishaniwa, lakini akaonya dhidi ya kutumiwa vibaya kauli hiyo kwa lengo la kuvilenga vikosi vya Hashd al-Shaabi.

Alikumbusha kuwa Hashd al-Shaabi ni sehemu ya muundo rasmi wa vyombo vya usalama vya Iraq, na kwamba pamoja na vikosi vya jeshi la nchi hiyo, walikuwa na nafasi muhimu katika kuukomboa mji wa Mosul na maeneo mengi yaliyokuwa chini ya uvamizi wa kundi la kigaidi la Daesh (ISIS).

Imamu huyo wa Swala ya Ijumaa Baghdad pia alionya dhidi ya kuchochea mvutano unaoweza kusababisha mapigano kati ya Mashia wenyewe kwa wenyewe, huku akisisitiza kuwa hali kama hiyo itahatarisha mafanikio yaliyopatikana Iraq.

Alimwomba Waziri Mkuu wa Iraq kuelekeza nguvu katika mageuzi ya kiuchumi, utoaji wa huduma kwa wananchi na kuboresha hali ya maisha ya raia, huku akiepuka maamuzi ya haraka na kauli zinazochochea mvutano.

Ayatullah Mousavi pia alisisitiza kuwa serikali ya Iraq haipaswi kusalimu amri mbele ya shinikizo za nje, wala kuingilia masuala ya Lebanon kwa namna itakayoifanya nchi hiyo iingie katika makabiliano na Hizbullah.

Lebo

Maoni yako

You are replying to: .
captcha