Kwa mujibu wa Idara ya tarjama ya Shirika la Habari la Hawza, Mahakama ya Kimataifa, ambayo ndiyo mahakama ya juu zaidi ya Umoja wa Mataifa, imetoa hukumu kwamba maelfu ya mauaji pamoja na vitendo vya ukatili wa kingono vilivyofanywa kwa kiwango kikubwa na vikosi vya usalama vya Myanmar dhidi ya jamii ya Waislamu wa Rohingya, walio wachache nchini humo, mwaka 2017, vilikuwa ni mauaji ya kimbari yaliyofanyika kwa uungwaji mkono wa serikali.
Uamuzi huo umetolewa miaka saba baada ya Gambia, nchi yenye idadi kubwa ya Waislamu, kuwasilisha kesi hiyo mahakamani. Hii ni mara ya nne tu katika historia ambapo mahakama ya kimataifa imetoa hukumu kwamba mauaji ya kimbari yamethibitishwa kisheria. Aidha, hii ilikuwa mara ya kwanza kwa mahakama hiyo kuitangaza serikali kuwa na hatia ya kuhusika na mauaji ya kimbari.
Rais wa mahakama hiyo alisema: “Mahakama imebaini kuwa vikosi vya usalama vya Myanmar vimewaua maelfu ya raia wa kawaida wa Rohingya, vimetekeleza vitendo vya ukatili wa kingono kwa kiwango kikubwa, pamoja na vitendo vya ukatili dhidi ya watoto, na pia vimewashambulia Waislamu wa Rohingya waliokuwa wakikimbia.”
Majaji walibaini kuwa jeshi la Myanmar lilitekeleza mauaji ya halaiki dhidi ya wanaume na wavulana, lilifanya ubakaji na vitendo vya ukatili wa kingono kwa kiwango kikubwa dhidi ya wanawake wa Rohingya, na kuchoma moto au kusawazisha mamia ya vijiji wakati wa operesheni zilizotajwa kuwa za “usafishaji”. Pia walisema kuwa jeshi lilieneza kikamilifu chuki dhidi ya jamii ya Rohingya.
Mahakama imesisitiza kuwa hukumu hiyo ni ya mwisho na haiwezi kukatiwa rufaa.
Mauaji ya kimbari ni kosa ambalo ni nadra kuthibitishwa katika mahakama za kimataifa. Hii ni kwa sababu waendesha mashtaka wanapaswa kuthibitisha kuwa kulikuwa na nia maalumu ya kuangamiza, kwa ujumla au kwa sehemu, kundi fulani la watu kwa misingi ya utaifa, kabila, rangi au dini.
Chanzo: The Japan Times
Maoni yako