Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Hawza, akizungumza katika khutba za Swala ya Ijumaa iliyoswaliwa siku ya jana katika Msikiti wa Ghadiir uliopo Kigogo Posti Jijini Dar es Salam, Sheikh Jalala alianza kwa kusoma aya ya 159 katika Suratul Aal-Imran, ambayo inazungumzia umuhimu wa upole, huruma, kusamehe na kushauriana katika mahusiano baina ya watu.
Mwenyezi Mungu (s.w.t.) anasema:
{ فَبِمَا رَحۡمَةࣲ مِّنَ ٱللَّهِ لِنتَ لَهُمۡۖ وَلَوۡ كُنتَ فَظًّا غَلِیظَ ٱلۡقَلۡبِ لَٱنفَضُّوا۟ مِنۡ حَوۡلِكَۖ فَٱعۡفُ عَنۡهُمۡ وَٱسۡتَغۡفِرۡ لَهُمۡ وَشَاوِرۡهُمۡ فِی ٱلۡأَمۡرِۖ فَإِذَا عَزَمۡتَ فَتَوَكَّلۡ عَلَى ٱللَّهِۚ إِنَّ ٱللَّهَ یُحِبُّ ٱلۡمُتَوَكِّلِینَ }
Basi ni kwa sababu ya rehema itokayo kwa Mwenyezi Mungu ndio umekuwa laini kwao. Na lau ungelikuwa mkali, mwenye moyo mgumu, bila ya shaka wangekukimbia. Basi wasamehe, na waombee maghfira, na shauriana nao katika mambo. Na ukishaamua, basi mtegemee Mwenyezi Mungu. Hakika Mwenyezi Mungu huwapenda wanaomtegemea.
(Suratul Aal-Imran: 159).
Akifafanua ujumbe wa aya hiyo, Sheikh Jalala alisema kuwa: neno "Rahmat" lililotumika katika aya hiyo linaweza kueleweka kwa maana ya huruma, malezi bora na maadili mema. Alieleza kuwa sifa hizo ndizo zilizokuwa miongoni mwa misingi iliyomfanya Mtume Muhammad (s.a.w.w.) kuwa mpole na kukubalika katika jamii.
Akisisitiza umuhimu wa kuwa na watoto wema katika jamii, Sheikh Mkuu wa Jumuiya ya Shia Tanzani, alisema kuwa: Mtoto mwema ndie msingi wa jamii yenye maadili, na jamii inapokuwa imara, taifa nalo hutengamaa, jambo linalochangia kuongoka umma kwa ujumla.
Uchaguzi wa mwenza wa ndoa ndio mwanzo wa malezi bora
Katika kuendelea na khutba yake, Sheikh Jalala alieleza kuwa: Miongoni mwa hatua muhimu zaidi katika kuhakikisha upatikanaji wa watoto wema ni uchaguzi sahihi wa mwenza wa ndoa. Alikumbushia kuwa, kama alivyobainisha katika khutba ya Ijumaa iliyotangulia, mtu anayetaka kuoa anapaswa kuzingatia familia anayotoka mwanamke anayemchagua, kwa kuhakikisha kuwa anatoka katika familia yenye misingi mizuri na mwenendo unaofaa.
Alifafanua kuwa baadhi ya familia zinaweza kuwa na matatizo na tabia zisizofaa zinazoweza kurithishwa kutoka kizazi kimoja kwenda kingine. Hivyo, mtu anapoamua kuoa katika familia yenye changamoto hizo, anapaswa kutambua uwezekano wa watoto wake kuathiriwa na baadhi ya tabia au matatizo yanayotokana na malezi na mazingira ya familia hiyo. Alisisitiza kuwa matatizo hayo si ya kimada pekee, bali yanaweza pia kuwa ya kimaadili na kimaanawi.
Aidha, Mkurugenzi wa Hawza ya Imam Swa'diq (as) aliielezea dini kuwa mojawapo ya nguzo muhimu zaidi zinazopaswa kuzingatiwa katika suala la ndoa. Alisema kuwa dini ni neema kubwa kutoka kwa Mwenyezi Mungu, na nyumba yoyote inayosimamiwa kwa misingi ya dini huwa imepata kheri na baraka. Alibainisha kuwa ndiyo sababu Mtume Muhammad (s.a.w.w.) amesisitiza sana umuhimu wa kuchagua mwanamke mwenye dini wakati wa kutafuta mwenza wa maisha.
Hatua za kukabiliana na mmomonyoko wa maadili
Katika sehemu nyingine ya khutba yake, Sheikh Jalala alisema kuwa: Mojawapo ya sababu kubwa zinazochangia kuzorota maadili katika jamii ya leo ni kutokuzingatia misingi sahihi ya ndoa na uchaguzi usiozingatia vigezo muhimu vya kujenga familia bora. Akizungumzia changamoto za kimaadili zinazoikabili jamii, alieleza kuwa jamii imekumbwa na matatizo mbalimbali, yakiwemo yale yanayohusiana na mapenzi ya jinsia moja.
Alisema kuwa: Hapo awali suala hilo ilikuwa ni aibu kulizungumzia hata katika mimbari, lakini kwa sasa limeanza kuchukuliwa na baadhi ya watu kama jambo la kawaida. Kutokana na hali hiyo, alisisitiza umuhimu wa kuchukua hatua za haraka na madhubuti ili kukabiliana na changamoto hiyo.
Vijana wahimizwa kuzingatia familia wanazotoka kuoa
Katika muendelezo wa khutba yake, Mkurugenzi wa Hawza ya Imaam Swaadiq (a.s.), aliwahimiza vijana wanaotarajia kuoa kuhakikisha wanachagua wanawake wanaotoka katika familia zenye misingi mizuri ya malezi na maadili. Alisisitiza kuwa uchaguzi usiozingatia ubora wa malezi na mazingira ya familia anayohusika nayo mwenza wa ndoa unaweza kuwa na athari kubwa kwa maisha ya ndoa na mustakabali wa kizazi kitakachozaliwa.
Akili na ulingano wa tamaduni ni vigezo muhimu katika ndoa
Katika kuendelea kuelezea vigezo vya uchaguzi sahihi wa mwenza wa ndoa, Sheikh Jalala aliutaja upeo wa kiakili kuwa ni miongoni mwa mambo muhimu ambayo vijana wanapaswa kuyazingatia. Alieleza kuwa: Mwanamke mwenye akili na busara huwa na uwezo mzuri wa kulea watoto, kusimamia masuala ya familia na kumsaidia mumewe katika kukabiliana na changamoto mbalimbali za maisha ya ndoa.
Kwa mujibu wa Sheikh Jalala, mwanamke mwenye upeo mzuri wa kiakili anaweza kuwa msaada mkubwa katika kuijenga familia yenye utulivu, maelewano na malezi bora kwa watoto. Vilevile, alisisitiza umuhimu wa kuzingatia ulingano wa tamaduni baina ya wanandoa, akieleza kuwa kufanana kwa tamaduni kunaweza kurahisisha maisha ya ndoa na kuwasaidia wanandoa kuelewana katika mambo mengi ya kila siku.
Alifafanua kuwa: Wanandoa wanapotoka katika mazingira yanayofanana kitaduni, huwa rahisi kuelewana katika baadhi ya masuala bila kuhitaji maelezo marefu, kwa sababu kila mmoja huwa na uelewa wa kawaida kuhusu mila na desturi za mwenzake.
Hata hivyo, alionya kuwa tofauti kubwa za kitamaduni zinaweza kuleta changamoto katika maisha ya ndoa, kwani jambo ambalo mwanamke analichukulia kuwa la kawaida kutokana na utamaduni aliolelewa nao, huenda kwa upande wa mume wake likaonekana kuwa si sahihi. Hali hiyo inaweza kusababisha kutokuelewana na kuleta ukakasi katika maisha yao ya ndoa.
Kwa ujumla, ujumbe wa Sheikh Jalala ulilenga kuonesha kuwa; ujenzi wa kizazi chenye maadili mema hauanzi baada ya mtoto kuzaliwa, bali huanzia katika uchaguzi sahihi wa mwenza wa ndoa, misingi ya kidini, ubora wa malezi na maandalizi ya kujenga familia yenye misingi imara.
Hivyo, vijana wanaotarajia kuingia katika maisha ya ndoa wanapaswa kutambua kuwa uchaguzi wanaoufanya leo una nafasi kubwa katika kuamua mustakabali wa familia zao na kizazi kijacho.
Maoni yako