Kwa mujibu wa taarifa ya Shirika la Habari la Hawza kutoka Kerman Iran, Ayatullah Sayyid Ahmad Kha'tami, jana jumanne alipokuwa akizungumza na wanafunzi na wanazuoni wa dini katika madrasa ya Amirul-Muuminina (amani iwe juu yake), iliyoko katika wilaya ya Rudbar-e Kusini, mkoani Kerman Iran, alizungumzia matukio nyeti ya hivi karibuni na kusema: “Kuchaguliwa Ayatullah Sayyid Mujtaba Khamenei ilikuwa ni kazi ya Mwenyezi Mungu na matokeo ya mapenzi Yake. Imam Shahidi alisema kwamba wananchi watafuata chaguo la Baraza la Wanazuoni Wataalamu wa Uongozi, na imani ya Ayatullah Khamenei ilikuwa sahihi. Kwa hiyo, mara tu baada ya Kiongozi kuchaguliwa, vikosi vyote, taasisi, Bunge na wananchi walimuunga mkono, na wataendelea kumuunga mkono kwa uthabiti.”
Simulizi Kuhusu Vitisho vya Wazayuni na Kasi ya Kufanya Maamuzi
Mwakilishi wa wananchi wa Kerman katika Baraza la Wanazuoni Wataalamu wa Uongozi, akifichua njama za utawala wa Kizayuni katika siku ambazo Baraza lilikuwa likifanya maamuzi, alisisitiza: “Israel ilikuwa imetangaza waziwazi kwamba italishambulia Baraza la Wanazuoni Wataalamu wa Uongozi ili kuzuia kuchaguliwa Kiongozi, walishambulia sekretarieti ya Baraza iliyoko Qum na kuwaua watu tisa, ambao walipata shahada.
Katika mazingira yale ya kutisha, huku kukiwa na uwezekano mkubwa wa kushambuliwa kwa mabomu, mimi kama mwanafunzi wa elimu ya dini nilisema: Huu si wakati wa kuafiki au kupinga; tunapaswa kumchagua Kiongozi haraka. Hata kama watatushambulia na kutuua, hilo si muhimu; lakini kulishambulia Baraza la Wanazuoni Wataalamu wa Uongozi ni sawa na kuushambulia mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu.
Baada ya kutoa hotuba ya dakika moja tu na kusema kwamba kwa uchaguzi huu Trump atakata tamaa, wajumbe wa Baraza walipiga takbira, na jambo hilo likakamilika.”
Hatua za Upigaji Kura na Jibu kwa Barua ya Pongezi
Mjumbe wa Baraza la Wanazuoni Wataalamu wa Uongozi, akifafanua hatua za upigaji kura, alisema: “Upigaji kura wa maandishi ulifanyika mara mbili kutokana na kushambuliwa kwa makombora sekretarieti ya Baraza. Mara ya tatu, upigaji kura ulifanyika kwa kukutana ana kwa ana kwa takribani wajumbe 60, ambapo karibu wajumbe 50 walipiga kura kwa wingi wa wazi kumuunga mkono Ayatullah Sayyid Mujtaba Khamenei.”
Aliongeza: “Baada ya kumwandikia barua ya kumpongeza kwa nafasi hii, yeye alijibu kwa kuandika kwamba: ‘Kwa kweli, hatukuwa tukitafuta kabisa jukumu hili, na hata sikuwa napenda kufuatilia mazungumzo yaliyokuwa yakiendelea.’
Amelelewa kwa miongo kadhaa chini ya usimamizi wa Imam. Ni kiongozi mwenye uwezo wa kusimamia mambo na kufanya maamuzi yenye busara, na msimamo wake ni msimamo wa mapambano ya kupinga uonevu na wa mashahidi.”
Onyo Dhidi ya Makundi ya Wanaotaka Maridhiano na Maadui, na Uwezo wa Iran
Ayatullah Kha'tami, akisisitiza kwamba msimamo wa uongozi ni msimamo wa kujitolea mhanga kwa ajili ya Wilaya alionya: “Makundi yanayotaka kufanya maridhiano na maadui, pamoja na wale wanaoisaliti nchi yao, ambao wana historia chafu kama ile ya mauaji ya Sheikh Fadhlullah Nuri, hayapaswi kuruhusiwa kuitawala nchi.
Maadui walitaka kuigawa nchi katika sehemu saba, lakini kutokana na uwezo wa makombora na uwepo wa wananchi, mipango yao ilifeli na wakapata pigo kubwa. Tutaendelea kusimama imara katika medani hii mpaka tuipigishe magoti Marekani.”
Maoni yako