Kwa mujibu wa taarifa ya Shirika la Habari la Hawza, Hujjatul-Islam wal-Muslimin Raji, alipokuwa akihutubia katika mkusanyiko wa maombolezo ya siku za kukumbuka shahada ya Bibi Fatima Zahra (amani iwe juu yake), katika Haram Tukufu ya Bibi wa Karama, alizungumzia mijadala ya siku zilizotangulia kuhusu sababu zilizosababisha kutokea matukio baada ya kufariki Mtume Mtukufu (rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake na Aali zake) na kuuwawa kishahidi Bibi Fatima Zahra (as).
Alisema: “Katika vikao vilivyopita, kwa kutegemea hotuba ya Bibi Fatima Zahra (as), tulieleza kwamba kupenda starehe, kuipenda dunia kupita kiasi, kujidhalilisha na kukosa kujiamini, woga, kuenea kwa ufisadi na uchafu, pamoja na kughafilika na adui, ni miongoni mwa vikwazo vinavyozuia kujengeka moyo wa muqawama na kusimama imara katika njia ya haki. Katika kikao hiki, tutachunguza sababu nyingine, nayo ni kujipatia mali na riziki kwa njia za haramu.”
Kujipatia Mali kwa Njia za Haramu: Mazingira Yanayochochea Kupambana na Kambi ya Haki
Ra'ji, akizungumzia tukio la siku ya Ashura na mazungumzo kati ya Imam Hussein (amani iwe juu yake) na jeshi la maadui, alisema: “Katika simulizi ya tukio hili imeelezwa kwamba Imam Hussein (as) alipolinasihi jeshi lililokuwa upande wa pili na kujitambulisha kwao, kelele zao zilizuia watu kusikia maneno yake. Katika mwendelezo wa simulizi hilo, Imam Hussein (amani iwe juu yake) alieleza kwamba sababu iliyowafanya wasikubali maneno ya haki ilikuwa ni matumbo yao kuchafuliwa na vitu vya haramu.”
Akiuliza jinsi baadhi ya watu walivyoweza, licha ya kuwa na historia ya kuandamana na Mtume Mtukufu (rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake na Aali zake) na kushiriki katika vipindi muhimu vya historia ya Uislamu, baadaye kujipanga dhidi ya Amirul-Muuminina Ali (as), aliongeza: “Miongoni mwa sababu zinazoweza kumtoa mwanadamu katika njia ya haki ni kuipenda dunia na kujipatia mali kwa njia za haramu. Mabadiliko ya hali ya kiuchumi ya baadhi ya Waislamu baada ya kipindi kigumu cha kuzingirwa katika ngome ya Abu Talib, pamoja na kupata utajiri na kubadilika kwa mtazamo wao kuhusu dunia, yalitengeneza mazingira ya wao kujitenga na maadili ya dini.”
Muumini Haiuzi Dini Yake kwa Mali au Maslahi ya Kidunia
Mhadhiri huyo wa Haram Tukufu, akizungumzia kisa cha Sharik bin Abdullah An-Nakha'i, mwanazuoni wa fiqhi na kadhi katika kipindi cha utawala wa Bani Abbas, alisisitiza jinsi mwanadamu anavyoweza kuathiriwa na mahusiano na maslahi ya kifedha, na kuongeza: “Mwanadamu anapaswa kuwa mwangalifu asije akaiuza dini yake na misingi yake kwa sababu ya kupokea mali au kupata manufaa fulani. Wakati mwingine, fursa ndogo ya manufaa inaweza kuwa mwanzo wa mtu kukubali majukumu na kufanya maamuzi ambayo hapo awali asingekuwa tayari kuyakubali.”
Ufisadi wa Kiasi Kikubwa Si Uhalalisho wa Wizi Mdogo
Akikosoa kuzoeleka baadhi ya ukiukaji wa sheria za kiuchumi katika jamii, alisema: “Hatupaswi kuuchukulia ukiukaji mdogo kuwa si jambo muhimu tunapolinganisha na ubadhirifu mkubwa wa fedha. Ikiwa mtu amefanya ubadhirifu wa maelfu ya mabilioni ya pesa, hilo halimpi mtu mwingine ruhusa ya kupandisha bei kwa udanganyifu, kupunguza vipimo vya bidhaa, kuiba au kupora haki za watu wengine.”
Mhadhiri huyo wa Haram Tukufu alieleza kwamba kila mtu anawajibika kulinda haki za watu kwa kadiri ya uwezo wake na nafasi aliyonayo, kwa kusema:
“Kutotekeleza majukumu ipasavyo kwa mtumishi wa umma, kuwachelewesha wananchi wanaokuja kupata huduma, kutotimiza wajibu kwa usahihi, kumdhulumu mpangaji au mwenye nyumba, kubadilisha tarehe ya mwisho wa matumizi ya bidhaa na kuuza bidhaa zilizokwisha muda wake wa matumizi, yote hayo yanaweza kuwa mifano ya kupora haki za watu.”
Raji aliongeza: “Haiwezekani kusema kwamba kwa kuwa mtu mwingine amefanya kosa kubwa zaidi, basi kosa letu dogo halina tatizo, kama ambavyo jinai kubwa haihalalishi jinai ndogo, vivyo hivyo, ubadhirifu wa kiasi kikubwa cha fedha hauwezi kuwa kisingizio cha wizi mdogo na ukiukaji wa sheria unaofanyika katika maisha ya kila siku.”
Akisisitiza umuhimu wa kuepuka kuzichukulia dhambi kuwa ni ndogo, alisema: “Hali ya hatari zaidi ni pale mwanadamu anapofanya jambo la haramu huku akiliona kuwa ni dogo na lisilo na umuhimu. Mtu anayeichukulia dhambi kuwa ni ndogo anaweza hata asifikirie kutubu na kurekebisha kosa lake.”
Mhadhiri huyo wa Haram Tukufu, akizungumzia aya za Qur'ani zinazohusu kupunguza vipimo na umuhimu wa kuheshimu haki katika biashara, alisisitiza kwamba; ukubwa au udogo wa kosa hauondoi wajibu wa mwanadamu kuwajibika. Hivyo, haki za watu zinapaswa kuzingatiwa katika miamala yote na mahusiano ya kijamii.
Kadiri Wajibu Unavyokuwa Mkubwa, Ndivyo Inavyohitajika Tahadhari Zaidi
Ra'ji, huku akisisitiza uzito wa wajibu wa viongozi na wenye nyadhifa, alisema kwamba; kadiri jukumu la mtu linavyokuwa kubwa, ndivyo umuhimu wa kulinda mali ya umma na haki za wananchi unavyoongezeka.
Alisema: “Mtu mwenye jukumu la umma hawezi kutumia nafasi yake kujitengenezea upendeleo usio wa haki au kujipatia manufaa binafsi.”
Akikosoa kuzoeleka rushwa katika baadhi ya mazingira ya kiutawala, alisema: “Wakati mwingine kunajengeka mtazamo kwamba ili jambo la mwananchi lifanyike, ni lazima alipe kiasi fulani cha fedha nje ya utaratibu wa kisheria. Mtu anayetoa au kupokea rushwa ili kutatua tatizo fulani hapaswi wakati huohuo kulaani ufisadi mkubwa wa kifedha huku akiwa hajali ukiukaji wa sheria alioufanya yeye mwenyewe.”
Ra'ji, akizungumzia pia suala la riba, alisema: “Baadhi ya matatizo yanaweza kusababishwa na kutofahamu hukumu za Sheria. Kwa hiyo, watu wanapaswa kuulizia na kupata ufafanuzi kutoka katika vyanzo vya kuaminika vya fiqhi na kwa wataalamu wa dini wanaofahamu masuala hayo, wanapofanya miamala na mikataba ya kifedha, hasa katika hali ambazo kuna uwezekano wa muamala huo kuwa na riba, ili wasije wakaingia katika jambo la haramu bila kukusudia.”
Aliongeza: “Wakati mwingine, watu huingia katika miamala bila kujua hukumu yake ya kisheria, na huenda hata wakajivunia kupokea faida isiyo halali. Kwa hiyo, kujifunza hukumu zinazohusu miamala na kuuliza katika ofisi ya Maraji' wa Taqalidi ni njia ya kujikinga na makosa ya aina hiyo.”
Kuheshimu Haki za Watu: Kuanzia kwenye Foleni ya Kutafuta Rizki Hadi Mali ya Umma
Mhadhiri huyo wa Haram Tukufu alisisitiza umuhimu wa kuheshimu haki za wengine katika tabia za kila siku kwa kusema: “Wakati mwingine, kuheshimu haki za wengine hujitokeza katika hali zinazoonekana kuwa rahisi. Ni hali ambazo baadhi ya watu wanaweza kuziona kuwa ni ukali au masharti yaliyopitiliza, hata hivyo, kushikamana na haki na kuepuka kutumia vibaya rasilimali na huduma ni miongoni mwa sifa zinazopaswa kuzingatiwa katika maisha ya kila siku.”
Raji alisisitiza: “Kuheshimu haki za umma hakuhusu tu fedha nyingi na kesi kubwa za ufisadi, bali huanzia katika gharama ndogo na rasilimali ambazo watu wamekabidhiwa kuzitumia.”
Umuhimu wa Kutathmini Upya Taswira Iliyojengwa Kuhusu Nchi za Magharibi
Katika kuendelea na hotuba yake, Ra'ji alikosoa taswira ambayo wakati mwingine hujengwa katika akili za vijana kuhusu uadilifu wa kazi na utendaji wa nchi za Magharibi.
Alisema: “Hatupaswi kukubali utendaji wa nchi za kigeni bila kuuchunguza na kuukosoa, wala kudhani kwamba miradi na mikataba yao yote hutekelezwa kwa umakini na ubora unaotakiwa.”
Mhadhiri huyo wa Haram Tukufu alitoa mifano ya baadhi ya miradi ya kigeni katika nchi mbalimbali, ikiwemo ujenzi wa kituo cha kuzalisha umeme nchini Ufilipino na miradi ya miundombinu nchini Afghanistan. Aliongeza: “Katika baadhi ya miradi hiyo, udhaifu katika usanifu au utekelezaji ulisababisha matatizo makubwa.”
Raji pia alirejelea mfano wa mojawapo wa miradi iliyohusiana na eneo la Andimeshk katika kipindi cha utawala wa Pahlavi. Alitaja ufisadi wa kiuchumi na kupuuzwa miundombinu kuwa miongoni mwa sababu zilizosababisha hasara ambazo athari zake zimedumu kwa muda mrefu.
Alisisitiza kwa kusema: “Kuwa na uelewa halisi kuhusu nchi nyingine kunahitaji kuchunguza utendaji wake kwa kutegemea ushahidi na nyaraka. Hatupaswi kutoa taswira ya upande mmoja kuhusu ufanisi au ufisadi katika jamii mbalimbali.”
Kukabiliana na Kuzoeleka Ufisadi Katika Jamii
Katika kuhitimisha hotuba yake, Raji alisisitiza: “Jamii ambayo kujipatia mali kwa njia za haramu, rushwa, riba, kupunguza vipimo vya bidhaa na kupora haki za watu yanakuwa mambo ya kawaida ndani yake, hukabiliwa na madhara ya kimaadili na kijamii. Jamii ya aina hiyo inaweza kupoteza uwezo wa kusimama imara dhidi ya upotovu na ukosefu wa haki.”
Akizungumzia uhusiano kati ya uadilifu wa kiuchumi na kushikamana na maadili ya dini, alieleza: “Kupambana na ufisadi hakuishii katika kuchukua hatua dhidi ya ubadhirifu mkubwa wa fedha pekee, bali huanzia katika kuheshimu haki za wengine katika shughuli za kila siku, kutekeleza majukumu kwa uaminifu na kulinda mali ya umma.”
Maoni yako