Jumamosi 10 Oktoba 2026 - 09:30
Kumdhukuru Mwenyezi Mungu ni Sifa ya Waumini wa Kweli

Hawza/ Maulana Sheikh Hemed Jalala Mwakindenge, Sheikh Mkuu wa Jumuiya ya Mashia Tanzania (TIC) na Imam Mkuu wa Msikiti wa Ghadir, uliopo Kigogo Post, jijini Dar es Salaam, amewahimiza waumini kudumisha utamaduni wa kumdhukuru Mwenyezi Mungu na kumtakia rehema na amani Mtume Muhammad (s.a.w.w), akisisitiza kuwa kumdhukuru Mwenyezi Mungu ni miongoni mwa sifa muhimu za waumini wa kweli na ibada yenye fadhila kubwa mbele ya Mola.

Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Hawza, Sheikh Jalala aliyasema hayo katika hotuba ya Swala ya Ijumaa iliyoswaliwa tarehe 9 Oktoba 2026 (17 Mehri 1405), katika Msikiti wa Ghadir, uliopo katika Makao Makuu ya Jumuiya ya Mashia Tanzania, Kigogo Post, jijini Dar es Salaam. Katika mwanzo wa hotuba yake, alisoma aya ya 142 ya Suratul Nisaa, inayozungumzia baadhi ya sifa za wanafiki, hususan uzembe wao katika Swala na uchache wa kumdhukuru Mwenyezi Mungu.

Mwenyezi Mungu anasema katika Qur’ani Tukufu:

{إِنَّ ٱلۡمُنَـٰفِقِينَ يُخَـٰدِعُونَ ٱللَّهَ وَهُوَ خَـٰدِعُهُمْ وَإِذَا قَامُوا إِلَى ٱلصَّلَوٰةِ قَامُوا كُسَالَىٰ يُرَاءُونَ ٱلنَّاسَ وَلَا يَذْكُرُونَ ٱللَّهَ إِلَّا قَلِيلًا}

“Hakika wanafiki wanadhani kuwa wanamhadaa Mwenyezi Mungu, na hali Yeye ndiye anayewalipa kwa hadaa yao. Na wanaposimama kwa ajili ya Swala, husimama kwa uvivu, wakijionesha kwa watu, wala hawamdhukuru Mwenyezi Mungu ila kwa uchache.”

[Suratun Nisaa: 142]

Katika kuielezea aya hiyo, Sheikh Jalala alisema kuwa: Miongoni mwa alama za wanafiki ni kutokuwa na mazoea ya kudumu ya kumdhukuru Mwenyezi Mungu. Alifafanua kuwa; wanafiki ni watu wanaojitahidi kuonekana mbele ya watu kuwa wanamcha Mwenyezi Mungu, ilhali matendo yao hayaakisi hali hiyo. Kwa upande mwingine, kumdhukuru Mwenyezi Mungu mara kwa mara ni miongoni mwa sifa zinazowatambulisha waumini na kuonesha uhusiano wao na Mola wao.

Aidha, Sheikh Jalala alisisitiza kuwa; kumdhukuru Mwenyezi Mungu si jambo la kufanywa kwa nadra au kwa ajili ya kuonekana na watu, bali ni ibada inayopaswa kuwa sehemu ya maisha ya kila siku ya muumini. Alieleza kuwa Qur’ani Tukufu imehimiza dhikri kwa wingi na kuahidi msamaha pamoja na ujira mkubwa kwa wanaume na wanawake wanaomdhukuru Mwenyezi Mungu.

Katika kuthibitisha jambo hilo, alisoma aya ya 35 ya Suratul Ahzaab, ambayo Mwenyezi Mungu anasema:

{وَٱلذَّاكِرِينَ ٱللَّهَ كَثِيرًا وَٱلذَّاكِرَاتِ أَعَدَّ ٱللَّهُ لَهُم مَّغْفِرَةً وَأَجْرًا عَظِيمًا}

“Na wanaume wanaomdhukuru Mwenyezi Mungu kwa wingi, na wanawake wanaomdhukuru Mwenyezi Mungu kwa wingi, Mwenyezi Mungu amewaandalia msamaha na ujira mkubwa.”

[Suratul Ahzaab: 35]

Akifafanua ujumbe wa aya hiyo, Sheikh Mkuu wa Mashia Tanzania alisema kuwa; kumdhukuru Mwenyezi Mungu kuna fadhila kubwa, kwani miongoni mwa malipo ambayo Mwenyezi Mungu amewaandalia wanadamu katika ibada hiyo ni msamaha na ujira mkubwa. Alieleza kuwa ahadi hiyo inadhihirisha umuhimu wa kumdhukuru Mwenyezi Mungu katika maisha ya mwanadamu na nafasi yake katika kumkaribisha mja kwa Mola wake.

Kumswalia Mtume Muhammad (s.a.w.w), miongoni mwa dhikri zenye fadhila kubwa

Katika kuendelea kufafanua umuhimu wa kumdhukuru Mwenyezi Mungu, Sheikh Jalala alibainisha kuwa; miongoni mwa dhikri adhimu ambazo waumini wanapaswa kudumu nazo ni kumswalia Mtume Muhammad (s.a.w.w), kwa kumtakia rehema na amani kutoka kwa Mwenyezi Mungu.

Akizungumzia fadhila za dhikri hiyo, alinukuu riwaya inayohusishwa na Mtume Muhammad (s.a.w.w), inayosema:

«إذا نسيتم شيئًا فصلُّوا عليَّ تذكروه إن شاء الله تعالى»

“Mtakaposahau jambo fulani, basi niswalieni mimi, na kwa mapenzi ya Mwenyezi Mungu Mtukufu mtalikumbuka.”

Katika kuielezea riwaya hiyo, Sheikh Jalala alisema kuwa inadhihirisha nafasi na fadhila za kumswalia Mtume Muhammad (s.a.w.w), huku akieleza kuwa riwaya hiyo inaashiria baraka zinazohusishwa na dhikri hii adhimu, kiasi cha kwamba mtu anapomswalia Mtume kwa nia ya kumdhukuru Mwenyezi Mungu, anaweza kupata msaada wa kukumbuka jambo alilokuwa amelisahau.

Alisisitiza kuwa; waumini wanapaswa kuifanya ibada ya kumswalia Mtume kuwa sehemu ya maisha yao ya kila siku, kwa kutambua nafasi yake katika kuimarisha uhusiano wao na Mwenyezi Mungu na kuonesha mapenzi yao kwa Mtume Wake.

Wosia wa Mtume kwa Abu Dharr kuhusu maisha na Akhera

Katika sehemu nyingine ya hotuba yake, Sheikh Jalala, ambaye pia ni Mkurugenzi wa Hawza ya Imam Swadiq (a.s), alizungumzia baadhi ya nasaha za Mtume Muhammad (s.a.w.w) alizompa swahaba wake, Abu Dharr al-Ghifari, huku akielezea umuhimu wa mwanadamu kujiandaa kwa ajili ya maisha ya Akhera na kutoyapa maisha ya dunia kipaumbele kinachomfanya asahau mwisho wa safari yake.

Katika kulielezea jambo hilo, alinukuu riwaya isemayo:

«يا أبا ذر، الكيس من دان نفسه وعمل لما بعد الموت، والعاجز من أتبع نفسه وهواها وتمنى على الله عز وجل الأماني»

“Ewe Abu Dharr! Mwerevu ni yule anayeichunguza na kuiwajibisha nafsi yake na kutenda kwa ajili ya maisha ya baada ya kifo. Ama mtu dhaifu ni yule anayeifuata nafsi yake na matamanio yake, kisha akawa na matumaini matupu kwa Mwenyezi Mungu Mtukufu.”

Akifafanua riwaya hiyo, Sheikh Jalala alisema kuwa; mtu mwenye hekima ni yule anayejitambua, anayejichunguza katika matendo yake na anayekumbuka kuwa maisha ya dunia yana mwisho. Alieleza kuwa mwanadamu hapaswi kuyapa mambo ya kidunia nafasi inayomfanya asahau wajibu wake kwa Mwenyezi Mungu na maandalizi ya maisha ya Akhera.

Hata hivyo, alifafanua kuwa kukumbuka kifo hakumaanishi kuacha kufanya kazi, kujitafutia riziki au kutekeleza majukumu ya kifamilia na kijamii. Badala yake, mwanadamu anatakiwa kufanya juhudi katika kutafuta riziki halali kwa ajili yake na familia yake, huku akiendelea kumkumbuka Mwenyezi Mungu na kujiandaa kwa maisha ya baada ya kifo.

Alionya kuwa si jambo jema kwa mwanadamu kujishughulisha mno na mambo ya dunia kiasi cha kusahau kuwa siku moja ataondoka katika maisha haya na kukutana na matokeo ya matendo yake. Kwa msingi huo, alihimiza waumini kuweka uwiano kati ya kutafuta mahitaji ya maisha ya dunia na kutekeleza wajibu wao wa kiroho.

Uaminifu na unyenyekevu, miongoni mwa sifa muhimu za waumini

Katika kuendelea na mawaidha yake, Sheikh Jalala aligusia kipengele kingine cha wosia wa Mtume Muhammad (s.a.w.w) kwa Abu Dharr al-Ghifari, kinachozungumzia umuhimu wa uaminifu na unyenyekevu mbele ya Mwenyezi Mungu.

Alinukuu riwaya isemayo:

«يا أبا ذر، إن أول شيء يرفع من هذه الأمة: الأمانة والخشوع، حتى لا تكاد ترى خاشعًا»

“Ewe Abu Dharr! Hakika jambo la kwanza litakaloondolewa katika umma huu ni uaminifu na unyenyekevu, kiasi kwamba itakuwa vigumu sana kumpata mtu mwenye unyenyekevu.”

Katika kuelezea riwaya hiyo, Sheikh Jalala alisema kuwa uaminifu ni miongoni mwa maadili muhimu ambayo waumini wanapaswa kuyazingatia katika maisha yao ya kila siku. Alifafanua kuwa mtu anapokabidhiwa amana, anawajibika kuitunza na kuifikisha kwa mwenye haki au sehemu iliyokusudiwa, bila ya kufanya udanganyifu au kuitumia vibaya dhamana hiyo.

Aliongeza kuwa uaminifu ni sifa muhimu katika kujenga mahusiano mema baina ya watu na kuimarisha misingi ya jamii yenye maadili. Alikumbusha kuwa Mtume Muhammad (s.a.w.w) alijulikana kwa uaminifu wake hata kabla ya kutimilizwa Utume wake, jambo linaloonesha nafasi kubwa ya sifa hiyo katika mwenendo wa Kiislamu.

Aidha, alieleza kuwa; unyenyekevu mbele ya Mwenyezi Mungu ni sifa inayopaswa kuambatana na ibada za waumini. Kwa mujibu wake, muumini anatakiwa kutekeleza ibada kwa moyo wenye unyenyekevu, kutambua ukuu wa Mwenyezi Mungu na kujiepusha na matendo ya kujionesha mbele ya watu.

Mwisho wa hotuba yake, Sheikh Jalala alimuomba Mwenyezi Mungu Mtukufu aharakishe kudhihiri Imam wa Zama, Imam Mahdi (a.j.f), na awawezeshe waumini kuwa miongoni mwa wafuasi wa kweli watakaoshikamana na mafundisho ya dini na kutekeleza wajibu wao kwa uaminifu, ikhlasi na unyenyekevu.

Lebo

Maoni yako

You are replying to: .
captcha